TUMSAIDIE RAIS KIKWETE KWA KUFANYA KAZI- ASKOFU ELIOPHOO SIMA

 

Na Maura Mwingira

Singida

16.1.2006

 

 

 

Askofu Eliophoo Sima wa Kanisa la Kiinijili la Kilutheri Dayosisi ya Kati Singida amewahimiza Watanzania kufanya kazi kwa bidii ili kumwongezea nguvu za kiutendaji Rais Jakaya Kikwete.

 

          Alitoa kauli hiyo jana baada ya kuwekwa Wakfu na kusimikwa kazini, katika ibada iliyofanyika katika viwanja vya Kanisa Kuu la Imanuel Mkoani Singida, ambapo Rais Jakaya Kikwete alikuwa mgeni rasmi.

 

          “Ikiwa kila mmoja wetu atafanya wajibu wake vyema, kwa nguvu zake zote na kwa akili zake zote bila shaka wewe uliye kiongozi wetu utakuwa na nguvu nyingi sana,” alisema Askofu Sima.

 

          Na kuongeza, “Huwezi kuwa Rais mwenye nguvu kama sisi raia wako tutashindwa kutumia vipaji vyetu ipasavyo, na tukafikiria kuwa matunda yote  yanatoka Ikulu, tutazitafuna sana nguvu zako na utakuwa dhaifu.”

 

          Askofu Eliophoo Yohana Sima ambaye aliwekwa Wakfu na kuingia kazini kuwa Askofu wa Dayosisi ya Kati Singida alichaguliwa kushika nafasi hiyo katika mkutano mkuu wa Sinodi uliofanyika Juni 20 mwaka jana.

 

          Alisisitiza kwamba, kila mwanadamu mahali alipo anaouwezo wa  kutosha na kumfanya aishi bila ya matatizo.

 

Hata hivyo akasema kuwa upo uzembe unaofanya  na baadhi ya wanadamu, uzembe wa kutotaka kutumia vipaji vyake, uwezo wake  na hazina ya maarifa  ya kuyamudu maisha yake na hatimaye kujikuta akiwa amezungukuwa na taabu nyingi.

 

          “Iko tabia mbaya ya watu wengi, na hii ni tabia mbaya sana, watu wasiotaka kuwajibuka, wanapenda kula matunda ya wengine, tena wanakula bila utaratibu, au wanakula na kuharibu watu hawa ni wabinafsi na ambao maadili yao hayawezi kuwa mazuri.

 

          Askofu huyo akaongeza kuwa Tanzania inahitaji viongozi walio wastaarabu, viongozi wenye uwezo wa kuona vizuri na kwamba wananchi wanakuwa na mashaka makubwa pale wanapoona viongozi wao wanashindwa kuona mambo yaliyodhahiri.

 

          Akamwomba Rais Kikwete na Watanzania wote kuifanya Tanzania kuwa mahali pazuri  kwa  kila mtu kufanya kazi.

 

          Akasema maswali yote hujibiwa kwa kazi nzuri, wenye kazi wana maneno machache. Na kwamba kazi nzuri, kazi halali ni ufunguo wa mafanikio.

 

Hata hivyo Askofu Sima amesema kuwa ili kila mtu afanye kazi, mfumo wa elimu unastahili kuboreshwa zaidi.

 

Akasema kuwa mfumo uliopo sasa umepungukiwa sana uwezo wa kuwafanya watoto wawe wabunifu.

 

“Elimu inayotolewa sasa inawafanya watoto wetu wasiwe wabunifu, mtoto anayemaliza kidato cha nne, vijana wanaomaliza kidato cha sita na chuo kikuu, bila ya kuajiriwa na serikali au na mashirika mengine wanashindwa kabisa kupiga mbizi katika bahari  hii yenye mawimbi”.

 

Akapendekeza kuwa itakuwa vyema kama elimu ya kilimo, biashara na elimu ya ujasiliamali zitatiliwa mkazo mashuleni ili kupunguza kero kubwa  itakayoendelea kulikumba taifa.

 

 

Akasisitiza kuwa mafaniko yaliyopo hivi sasa yanatokana na raia waaminifu, ambao siku zote wamekuwa wakiamini kuwa bila kuhenya huwezi kupata mafanikio.

 

Akatahadharisha kwa kusema “nguvu zao, muda wao na kwa  fadhila zao, wamejitolea kwa uaminifu kwa nchi hii, mafanikio hayo yasitumiwe ovyo na watu wasio na huruma. Kwani kwa kufanya hivyo kunawakatisha tamaa watu wengine kutumikia kwa uaminifu, wakati wengine wakisubiri kuyatafuna bila huruma matokeo mema ya kazi hiyo au kuyaharibu”.

 

MWISHO.