PRESS SECRETARY TO THE PRESIDENT

 

Fax. No. 255-22 2113425                                              The State House,                                  

Tel: 255-22-2116539/2116913                                      P.O. Box 9120,

                                                                                           DAR ES SALAAM.

 

E-mail:  press@ikulu.go.tz

 

 

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

 Rais akutana na Bodi ya Wakurugenzi wa Milleniaum Challenge.... 1

 

Bodi ya wakurugenzi wa Millenium Challenge Corporation, imeridhia Tanzania kuwa moja ya nchi zitakazonufaika na misaada ya kifedha kutoka taasisi hiyo.

 

Hayo  yamesemwa  leo na kiongozi wa ujumbe wa Millenium Challenge Corporation, Bw. John Hewko, wakati yeye na ujumbe wake walipomtembelea Rais Jakaya Kikwete, Ikulu.

 

Katika mazungumzo hayo kiongozi  huyo alisema kuwa Bodi hiyo katika kikao chake  cha hivi karibuni ilikuwa imeridhia Tanzania kunufaika na misaada yake, baada ya kuwa imepita katika vigezo mbalimbali ambavyo nchi inayoomba hutathiminiwa na bodi hiyo.

 

Milleniumn Challenge Corporation ambayo ni taasisi inayomilikiwa  na serikali ya Marekani, hutoa misaada ya kifedha inayolenga katika kuiwezesha nchi  hasa zile zinazoendelea kutekeleza mipango ya kukuza uchumi na kuupiga vita umaskini.

 

Fedha ambazo  Tanzania  inatarajia kupata katika mpango mdogo wa awali  ujulikanao kama  ‘Threshold Country’  programu,  ni dola za kimarekani 11.5 milioni zitakazotumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali.

 

Miradi itakayonufaika na fedha hizo, ni ya uwezeshaji  katika sekta ya utawala bora, vyombo vya habari, asasi za kijamii, uboreshaji wa huduma za kisheria hapa nchini zikiwamo za ujenzi wa mahakama za mwanzo na mafunzo kwa mahakimu.

 

Katika mazungumzo hayo, Bw. John Hewko alimweleza Rais kwamba serikali ya Marekani chini ya uongozi wa Rais George Bush, inaridhishwa  sana na uboreshaji na  sera za kiuchumi pamoja na demokrasia na kwamba imedhamiria kufanya kazi  kwa karibu na serikali ya Tanzania ili kuwajenga maisha bora Watanzania.

 

Akasema kuwa mpango huo wa awali, utafuatiwa na mpango mkubwa zaidi wa kufadhili miradi ya maendeleo. Mpango huo unakadiriwa kutoa dola za Kimarekani milioni 700.

 

Rais akutana na Bodi ya Wakurugenzi wa Milleniaum Challenge.... 2

 

Akashauri kuwa kwa vile Tanzania imeshapitishwa kuwa moja kati ya nchi zitakazonufaika, ni vema serikali ikaanza kutafakari  na kupanga miradi ya kipaumbele itakayofadhiliwa yenye  kutoa tija inayolenga katika kuupiga vita umaskini na kuinua uchumi. Akapendekeza kipindi cha miezi sita hadi tisa inatosha kwa kazi hiyo.

 

Akasisitiza kuwa ni vema serikali ikachagua miradi michache ya kipaumbele na kwamba pale serikali itakapokuwa tayari, basi wao watatuma  wataalamu wao watakaokaa na wataalam Tanzania kuichambua miradi hiyo ili utekelezaji wake uweze kuanza.

 

Aidha Bw. Hewko akizungumza kwa niaba ya ujumbe wake alimpongeza Rais Kikwete kwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na namna Watanzania walivyo na  imani na matumaini makubwa juu yake.

 

Akiishukuru serikali ya Marekani kwa uamuzi wake wa kuiridhia Tanzania kuwa mnufaika wa mfuko huo, Rais alisema kuwa fedha hizo  zitachangia sana katika juhudi za serikali za kupambana na umaskini.

 

Akasema kuwa  habari hizo njema zimekuja wakati muafaka, na kwamba serikali  itakaa na wataalamu wake na kupanga miradi ya kipaumbele mapema iwezekanavyo.

 

Hata hivyo akaitaja baadhi ya miradi ambayo ni ya kipaumbele kwa serikali. Miradi hiyo  ni pamoja na utoaji wa huduma bora ya maji safi na salama kwa umbali mfupi na hasa kwa wananchi wa kijiji.  Barabara za vijijini, uboreshaji wa huduma za afya.

 

Akautaja mradi mwingine kuwa ni uboreshaji wa elimu na mkazo ukitiliwa zaidi katika kumwezesha mtoto wa kike kupata elimu hiyo hadi ukomo wake.

 

Rais Kikwete akaishukuru pia serikali ya Marekani kwa kuonyesha utayari wake wa kushirikiana na serikali yake katika uboreshaji wa maisha ya Watanzania.

 

Akatumia nafasi hiyo kutoa shukrani zake kwa Rais George Bush kwa salamu za pongezi alizomtumia  baada ya kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa kwa upande wa Tanzania na Katibu Mkuu Kiongozi, Bw. Philemon Luhanjo, Katibu Mkuu wa Hazina, Bw. Gray Mgonja na Bw. Bernad Said Mchomvu.

 

Mwisho.

 

Ikulu

1 Februari, 2006