TATHMINI YA ZIARA YA RAIS YA KUTEMBELEA MASOKO YA NAFAKA YA DAR ES SALAAM

 

 

Tarehe 6/2/2206, Mhe. Rais alifanya ziara ya ghafla ya kutembelea masoko yanayouza nafaka katika jiji la Dar es Salaam.  Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kujionea hali halisi ya chakula ilivyo pamoja na bei zake.

 

Masoko ambayo Mhe. Rais aliyatembelea ni Tandale, Tandika na Kariakoo.

 

Baada ya Ziara hiyo, Katibu wa Rais aliitisha mkutano wa wasaidiza wa Rais kwa lengo la kufanya tathimini ya ziara hiyo.

 

Wajumbe waliohudhuria mkutano huo

 

1.     D. Jairo                           - Mwenyekiti

2.     F. Kuzilwa                      - Mjumbe

3.     R. Luhwavi                     - Mjumbe

4.     S. Kamhanda                  - Mjumbe

5.     Col. Simule                     - Mjumbe

6.     Col. Kimarao                  - Mjumbe

7.     M.Mwingira                    - Mjumbe

8.     Col. N.  Kaisi                 - Mjumbe

 

Akifungua mkutano huo, Katibu wa Rais aliwataka wajumbe kuchangia kwa maana ya kuitathimini Ziara ya Mhe, Rais katika masoko yale, na kutoa mapendekezo ya kumshauri Mhe.

 

·        Kwa ujumla wajumbe waliridhika kwamba ziara hiyo ilikuwa ya mafanikio, kwani ilikidhi matarajio ya Mhe. Rais ambayo yalikuwa ni kujionea hali halisi ya chakula ilivyo katika masoko hayo.

 

 

·        Wajumbe walikubaliana kwamba hali ya chakula katika masoko hayo hususani nafaka haikuwa mbaya wala nzuri. Kwamba kulikuwa na nafaka ingawa si kwa kiwango cha kuridhisha.

 

·        Baadhi ya maeneo ambayo hutumika kuhifadhi nafaka wakati wa neema yalikuwa matupu, ni sehemu chache tu ndizo zilikuwa na magunia machache ya nafaka.

 

·        Aidha bei za nafaka hizo pia ilikuwa inatofautiana kutoka kwa muuzaji moja hadi mwingine.

 

·        Baadhi ya nafaka kama vile unga wa sembe uliuzwa kilo shilingi 480, mchele uliuzwa shilingi 650 hadi 800 kwa kilo. Bei hii pia ilikuwa ni tofauti kwa masoko ya Kariakoo ambako kilo ya mchele ilikwenda  hadi shilingi 1000.

 

·        Kupanda kwa bei za nafaka kulielezwa na wachuuzi hao kwamba kulitokana na  uhaba wa nafaka zenyewe, gharama za usafirishaji na ubora wa nafaka kulingana na maeneo inakotoka.

 

·        Katika masoko yote matatu, kilio cha wananchi kilikuwa ni bei kubwa ya nafaka hizo, na walimwomba Mhe. Rais kuingilia kati.

 

·        Wajumbe waliridhika pia kwamba gharama za nafaka zinasimamiwa zaidi na soko huru kwa vile serikali ilikuwa imejitoa katika udhibiti wa bei, hivyo kila mchuuzi alijipangia bei kulingana na mazingira ya wakati ule.

 

·        Wajumbe walielezwa pia kwamba hata nafaka ambazo zilikuwa zimeingizwa nchini na wafanyabiashara ambao wameondolewa ushuru na serikali, nazo zilikuwa zikiuzwa kwa bei ya juu, kinyume na matarajio ya serikali kwamba nafaka hizo zingeuzwa kwa bei nafuu.

 

·        Katika kukabiliana na hili wajumbe walipendekeza kwamba, utafiti zaidi ufanyike, kwanza wa kupata taarifa kutoka ofisi ya Waziri Mkuu- Idara ya Maafa kuhusu utaratibu mzima   ikiwa ni pamoja na makubaliano yaliyopo kati ya serikali na wafanyabiashara hao. Jukumu hili alipewa Mshauri Mkuu wa Rais, Col. Kaisi.

·         Aidha wajumbe walipendekeza pia kuwa ipatikane kutoka  kwa watu wa masoko bei halisi za nafaka katika masoko hayo hususani katika kipindi hiki ambako kuna uhaba mkubwa wa nafaka.

 

·         Aidha ilikubalika pia kwamba pawepo na usimamizi kamili wa kusimamia tangu pale meli inayoleta chakula inapoingia bandarini, upakuaji wake,  usafirishaji wa chakula hicho hadi usambazaji wake.

 

·        Wajumbe walipendekeza hili lifanyike, ili kuwabana  baadhi ya wafanyabiashara  wasio waaminifu ambao wanaweza  kuhujumu  juhudi za serikali katika kukabiliana na balaa hili la njaa.

 

·        Wajumbe pia waligundua kuwa  licha ya wafanyabiashara wa masoko hayo kulipa ushuru, hali ya masoko hayo hususani Tandale na Tandika ilikuwa mbaya, uchafu uliotapakaa kila mahali, na barabara za kuingia na kutoka kwenye masoko hayo zilikuwa mbovu.

 

Mwisho