PRESS SECRETARY TO THE PRESIDENT

 

Fax. No. 255-22 2113425                                              The State House,                                  

Tel: 255-22-2116539/2116913                                      P.O. Box 9120,

                                                                                       DAR ES SALAAM.

E-mail:  press@Ikulu.go.tz

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

 

Kikwete akutana na wafanyakazi wa IKULU

 

 

Rais Jakaya  Kikwete amemuagiza Katibu Mkuu Kiongozi, Bw. Philemon Luhanjo kuhakikisha kwamba anasimamia na kuboresha mazingira ya kazi  na  maslahi ya  wafanyakazi wa Ofisi ya Rais Ikulu, na watumishi wote wa serikali.

 

Rais alitoa agizo hilo hapo jana wakati alipokutana rasmi  na kwa mara ya kwanza na wafanyakazi wa Ofisi ya Rais Ikulu, katika hafla  iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu.

 

“Sasa maarifa yale uliyotumia Mambo ya Nje hadi wakakupenda sana, unatakiwa  sasa uzidishe, kwa hapa Ikulu. Lakini sasa wewe unayo dhamana ya serikali nzima  basi hakikisha mazingira ya watumishi wa serikali zima yako katika hatua nzuri.Waangalieni wafanyakazi ili  waweze kutusaidia ili tuweze kupata mafanikio”. Akasisitiza Rais, kauli iliyoshangiliwa sana na wafanyakazi hao.

 

Rais Kikwete akabainisha kwamba, wafanyakazi wanapokuwa na furaha wanakuwa fursa na uwezo  wa kutumia uwezo wao wote walionao kufanya kazi. Lakini kama hawafurahi  wanabania  zile nguvu zao kwa sababu wanaziona kuwa hazina faida.

 

Akasisitiza kuwa masuala yanayohusu kuwawezesha wafanyakazi wa  Ofisi ya Rais Ikulu, anamwachia Katibu Mkuu Kiongozi, Bw. Luhanjo, na Katibu Mkuu Ikulu Bibi Rose Lugembe ambao wote aliwaelezea kuwa hana mashaka na utendaji wao.

 

Katika hafla hiyo ambayo Mke wa Rais Mama Salma alihudhuria, Rais aliwahakikishia wafanyakazi hao kwamba yeye kama kiungo anaahidi kuyatimiza  yale anayostahili kuyatimiza kwao. Ili nao wamsaidie aweze kutimiza wajibu  anaotarajiwa kuutimiza kwa wananchi wa Tanzania.

 

“Tunao wajibu mkubwa, tunayo matarajio makubwa kwa wananchi, lakini wajibu huo sio wangu miye peke yangu, wajibu huo ni wangu miye pamoja na nyie. Kwa hiyo kufanya kazi kwenu na kufanikiwa katika kazi, ndiko kutakako niwezesha na miye kufanikiwa”, akasisitiza.

 

Akaongeza kuwa ikiwa wafanya kazi hao watatekeleza majukumu yao vizuri basi sifa zitakuwa ni za kwake Rais, lakini kama watafanya vibaya lawama  atapata yeye na hiyo ndio maana ya dhamana.

 

Aidha  Rais alisema kuwa amefurahi na kuridhishwa na mapokezi mazuri na kwa msaada mkubwa alioupata kutoka kwa wafanyakazi wa Ofisi ya Rais tangu aliposhika madaraka ya nchi.

 

Akabainisha kuwa  wafanyakazi hao ni wachapakazi hodari  ni watu ambao wana uwezo mkubwa.

 

Awali akimkaribisha Rais katika hafla hiyo, Katibu Mkuu Bibi Rose Lugembe alimweleza Rais kwamba, Ofisi ya Rais Ikulu, ina wafanyakazi 364. Kati ya hao 270 wapo Makao Makuu na 94 wako katika Ikulu ndogo zilizoko mikoani.

 

Akasema kuwa Ofisi ya Rais Ikulu ina idara nne na vitengo vitatu. Idara hizo ni Huduma za Ikulu, Ofisi Binafsi ya Rais, Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri na Idara ya Mawasiliano. Kwa upande wa vitendo ni Uratibu na Utawara Bora, Fedha na Uhasibu na Ukaguzi wa ndani.

 

Wafanyakazi hao wa Ofisi ya Rais Ikulu, waliahidi kwamba, watamsaidia na kumwezesha Mhe. Rais ili aweze kuongoza taifa kwa ufanisi  na ustawi mkubwa. Pamoja na kujitahidi kuwa mfano bora katika kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.

 

Na kuongeza kuwa watahakikisha  kunakuwa na ufanisi wa usimamizi wa shughuli za Ikulu, kuwezesha Baraza la Mawaziri, kuhakikisha utaratibu mzuri wa shughuli za utawala bora na kuwasilisha kwa uhakika na kwa wakati maamuzi ya Rais kwa wahusika wote.

 

Naye Mwenyekiti wa  Tawi la Wafanyakazi (TUGHE), Ikulu, Bw. Norbert Ntilema, akizungumza kwa niaba  ya wafanyakazi, alimshukuru Rais kwa kutenga muda wake ili aweze kukutana na kufahamiana na wafanyakazi hao.

 

Akasema hatua hiyo inaonyesha ni namna gani anavyowathamini na kutambua kazi wanazozifanya. Na kuahidi ushirikiano, uadilifu na uaminifu katika utendaji wao wa kazi.

 

Mwisho

 

Ikulu

 

7 Februari, 2006