PRESS SECRETARY TO THE PRESIDENT

 

Fax. No. 255-22 2113425                                              The State House,                                  

Tel: 255-22-2116539/2116913                                      P.O. Box 9120,

                                                                                           DAR ES SALAAM.

 

E-mail:  press@Ikulu.go.tz

 

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

 

KUNA MATUMIZI MABAYA YA FEDHA KATIKA HALMASHAURI-KIKWETE                                                                     

 

  • Awataka wakuu wa mikoa kusimamia kwa karibu
  • Awataka kwenda kwa wananchi
  • Awataka pia kuwabana  mabwana misitu

 

Na Mwandishi Maalum

Dodoma

 

 

10/2/2006

 

Rais Jakaya Kikwete  amesema  haridhiki na hali ya utendaji  kazi wa halmashauri nyingi za wilaya hapa nchini, na hususani katika matumizi ya fedha.

 

Ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na wakuu wa mikoa mara tu baada ya kuwaapisha katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu, Chamwino.

 

“Serikali inatoa fedha nyingi kwenye halmashauri, lakini matumizi ya fedha hizo yaharidhishi kabisa, kuna ubadhirifu mkubwa katika halmashauri, na nyinyi ndio wawakilishi wa Rais na ndio wasimamizi wa serikali, basi zisimamieni kwa  karibu halmashauri “ akasisitiza Rais.

 

Akaongeza kuwa hataka kama kuna maboresho ya  halmashauri za wilaya, lakini maboresho hayo hayazifanyi halmashauri  kuwa idara zinazojitegemea, bali ni wakala  katika kuisaidia serikali katika utekelezaji wa majukumu yake.

 

Akionyesha dhahiri kuchukizwa na matumizi mabaya ya fedha katika halmashauri hizo, Rais alisema   wakuu hao wana wajibu wa kuyatumia madaraka yao kikamilifu katika

 

usimamizi wa matumizi hayo ya fedha zinazopelekewa katika  halmshauri ikiwa ni pamoja na kujua  nini kinafanyika ndani ya halmashauri hizo.

 

“Halmashauri nyingi zinaendeshwa hovyo hovyo tu, lazima mjue wanafanya nini,  sisemi muwaingilie sana, lakini ni wajibu wenu kuwasimamia madiwani, msikae maofisini, mkiishia maofisini kwenu, watu huko chini wataendelea na kazi, lakini hawatafanya kile nyinyi mnachotaka  wafanye, watafanya mambo yao, tokeni maofisini kwenu”. Akasema Rais.

 

Kwa mujibu wa Rais, halmashauri za wilaya zimekuwa zikipokea mamilioni ya fedha, kutoka Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi, Mfuko wa Barabara, TASAF, Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari, fedha ambazo amesema kama matumizi yake yangekuwa mazuri kungekuwa na kasi kubwa ya maendeleo huko vijijini.

 

Katika mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na Makamu Rais, Dk  Ali Mohamed Sheni, Waziri Mkuu, Edward Lowasa na Waziri wa  Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa, Mizengo Pinda, Rais alisema kuwa amewateua wakuu hao wa mikoa kushika nyadhifa hizo kwa kuwa anawaamini.

 

Akawaambia “Nimewateua kwa sababu ninawaamini, na imani huzaa imani. Ningekuwa na wasiwasi nanyi nisingewateua, ni matumaini yangu mtaniwakilisha vizuri na hamtaniangusha”.

 

Rais Kikwete aliwataka pia wakuu hao wa mikoa, kuzingatia maadili ya uongozi na maadili ya kazi, na kuongeza kuwa uhusiano na urafiki  kati yake na wakuu hao utasimama katika utendaji wa kazi na matokeo ya kazi hizo.

 

“Jamani tukafanye kazi, sisi sote ni watu wazima, si vizuri kukumbushana juu wa wajibu wa majukumu yetu, sitegemei kufanya hivyo, lakini pale nitakapoona mambo yanakwenda ndivyo sivyo, basi nitakuwa sina njia nyingine bali kukubushana wajibu huo, lakini sitarajii tufikishane huko”, akasisitiza.

 

Akasema , Mkuu wa Mkoa ni kiongozi mkubwa sana, na kwa sababu hiyo matendo yake lazima yaendane na nafasi hiyo na lazima awe  mfano mbele ya jamii kwa kuwa  na maadili mema.

 

Aidha  Rais kama ilivyokuwa kwa  mawaziri, aliwaeleza wakuu hao wa mikoa kwamba wanakwenda kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, na kwa hiyo utendaji kazi wao lazima ulenge katika Ilani.

 

Amewataka watakapowasili katika vituo vyao vya kazi kupanga mikakati ya utekelezaji wa Ilani hiyo, ikiwa ni pamoja na kukusanya ahadi zote zilizotolewa wakati wa kampeni ili ziwekewa mikakati ya utekelezaji.

 

 

 

Kuhusu suala la ukame, njaa, na magao wa umeme, Rais aliwakumbusha wakuu hao wa mikoa kusimamia vema ugawaji wa chakula  kwa kuzingatia uwezo wa wananchi katika kukipata chakula hicho.

 

Na kusisitiza kuwa asingependa kusikia taarifa za watu waliokufa kwa kukosa chakula.

 

Aliwataka pia kusimamia mgao wa umeme na kuwakumbusha TANESCO kuheshimu ratiba zao za mgao.

 

Kuhusu suala la ulinzi na usalama, Rais alisema kwa kuwa wakuu wa mikoa ndio wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama, basi wanawajibu mkubwa wa kusimamia amani katika maeneo yao. Na kuwataka kuchukua hatua na kupambana na ujambazi.

 

Aidha Rais aliwataka pia wakuu hao wa mikoa kulisimamia kwa karibu  tatizo la utumiaji wa madawa ya kulevya kwa vijana. Amesema kuwa tatizo hilo hivi sasa linaelekea kuota mizizi na kuharibu maisha ya vijana wengi na kwamba tatizo hilo linahama katika  miji mikubwa na kwenda vijijini.

 

Kwa upande wa utunzaji wa mazingira, Rais aliwaagiza wakuu hao, kuhakikisha kuwa wanasimamia kwa karibu, upandaji wa miti, kusimamia ukataji wa miti pamoja na utunzaji wa vyanzo vya maji na uoto wa asili.

 

Akasema kuwa utunzaji wa mazingira ni ajenda kudumu na hivyo akawaasa kutoimba wimbo wa utunzaji wa mazingira bila ya kuweka mikakati madhubuti na ufuatiliaji wake.

 

Akawataka kuwasimamia kwa karibu, mabwana misitu ambao aliwaelezea kuwa wao ndio vinara katika suala zima la uharibifu wa mazingira kwani baadhi yao wanajihusisha na biashara za uchomaji wa mikaa, usafirishaji wa magogo na biashara ya mbao.

 

Akizungumza kwa  niaba ya wakuu wenzi wa mikoa, mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Yusuf Makamba, alimshukuru Rais kwa kuwateua na kwa kuwaamini kwamba wanaweza kumsaidia.

 

Akasema kwa upande wao watajitahidi kumsaidia Rais kwa kutekeleza majukumu yao kwa ukamilifu, umakini na kwa kasi mpya, na kwa kuzingatia maelekezo aliyowapata.

 

Mwisho.