PRESS SECRETARY TO THE PRESIDENT

 

Fax. No. 255-22 2113425                                              The State House,                                  

Tel: 255-22-2116539/2116913                                      P.O. Box 9120,

                                                                                           DAR ES SALAAM.

 

E-mail:  press@ikulu.go.tz

 

 

 

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

 

Balozi Andrew Young azungumza na Rais Kikwete …. 1

 

Mwenyektii wa Mfuko wa kuendeleza biashara katika nchi za Kusini mwa Afrika (SAEDF), Balozi Andrew Young amemhakikishia Rais Jakaya Kikwete kwamba mfuko huo uko tayari kumsaidia katika uwezeshaji  wa wafanyabiashara   wadogo na wa kati hapa nchini.

 

Balozi Andrew Young ameyasema hayo leo Ikulu jijini wakati yeye na ujumbe wa mfuko huo walipomtembelea Rais Kikwete na kuzungumza naye.

 

Tueleze wapi  unataka tukusaidie, na sisi tuko tayari kukusaidia, tutafungua miradi zaidi hapa Tanzania”, akasisitiza Balozi Young

 

Mfuko wa kuendeleza biashara katika nchi za Kusini mwa Afrika, ulianzishwa na Rais mstaafu wa Marekani Bill Clinton mara baada ya kuzaliwa Afrika Kusini huru mwaka 1994.

 

Madhumuni hasa ya mfuko huo ni katika kuwawezesha Waafrika hasa weusi ( black empowerment) ili nao waweze kushiriki katika umiliki wa uchumi kwa kuendesha viwanda vidogo na vya kati.

 

Balozi Andrew Young amemueleza Rais ya kuwa mfuko huo unataka kujielekeza sasa katika kuwawezesha Watanzania kimitaji, kimenejimenti na katika mbinu za upembuzi yakinifu zitakazowawezesha kuanzisha na kuendeleza viwanda vidogo vidogo na vya kati.

 

Mwenyekiti huyo akasisitiza umuhimu wa Waafrika hususan wazalendo  kuwa na uwezo wa kumiliki taasisi za kifedha tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo alisema ni Waafrika wachache sana wenye uwezo huo ikilinganishwa na Waasia au Wazungu.

 

Aidha Balozi Young alipongeza msimamo wa Tanzania wa kutoingilia mambo ya ndani katika nchi ambazo zimesaidiwa na Tanzania katika kumaliza matatizo yao ya kisiasa.

 

 

 

Balozi Andrew Young azungumza na Rais Kikwete ….2

 

 

Akazitaja nchi hizo kuwa ni Rwanda, Burundi na Jamhuri ya  Demokrasia ya Congo (DRC).

 

Katika mazungumzo hayo Rais Kikwete alimweleza Mwenyekiti huyo wa SAEDF kwamba mfuko huo umekuja katika  wakati  muafaka ambapo serikali inajipanga vema katika mbinu na mikakati ya kuwawezesha Watanzania walio wengi kumilikia uchumi na kuupiga vita umaskini.

 

Akasema juhudi hizo za serikali zinakwamishwa na uwezo mdogo wa kifedha na vile vile katika uandaaji wa sera na mikakati ya uwezeshaji na ndio maana mifuko kama hiyo inakaribishwa ili iweze kusaidiana na serikali.

 

Miongoni mwa wajumbe wa Bodi ya mfuko huu ni pamoja na Balozi mstaafu Ami Mpungwe.

 

SAEDF inaendesha shughuli zake katika nchi 10 ambazo ziko katika Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

 

Mwisho

 

Ikulu

13 Februari, 2006