PRESS SECRETARY TO
THE PRESIDENT
Fax. No. 255-22 2113425 The State House, Tel: 255-22-2116539/2116913 P.O. Box 9120,
DAR ES SALAAM.
E-mail: press@ikulu.go.tz
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
Jakaya Kikwete leo amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Balozi Akrasi
Amatayakul wa Thailand.
Pamoja na kuwasilisha hati zake, Balozi Amatayakul pia aliwakilisha kwa Rais salaam kutoka ka Mfalme wa Thailand na salaam za Waziri Mkuu.
Katika mazungmzo yao, Balozi huyo ambaye ofisi zake ziko Nairobi – Kenya, alisema nchi yake inafikiria kuanzisha ubalozi mdogo hapa nchini.
Akasema ufunguzi wa ubalozi huo utasaidia sana kuratibu kwa karibu uhusiano na ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.
Akielezea maeneo ambayo Thailand na Tanzania zinaweza kushirikiana, aliyaeleza kuwa ni ubadilishanaji wa utaalam na teknolojia katika sekta za kilimo, maji, utaalam wa ufundi na nafasi za masomo kwa wanafunzi wa Kitanzania kwenda kusoma Thailand.
Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete aliitaka Serikali ya Thailand kuangaliwa uwezekano wa wafanya biashara wakubwa hususan katika sekta za nguo kuja nchini kuwekeza.
Akasema ikiwa hilo litatekelezeka, basi wafanya biashara wengi kutoka Tanzania na nchi nyingine za Afrika hawatakuwa na sababu ya kwenda Bangkok kununua bidhaa hususan nguo.
Rais alisema uwekezaji katika viwanda vya nguo pia kutawasaidia sana wakulima wa pamba kupata soko la uhakika la zao hilo.
Aidha Rais alielezea kiu yake ya kutaka Watanzania na hasa wakulima wajifunze kutoka Thailand ukulima wa kisasa wa zao la muhogo na namna ya kuliongezea thamani ili liweze kuuzwa nje ya nchi.
Hivi sasa Thailand ni moja ya nchi zinazouza muhogo kwa wingi katika nchi za ulaya na kujipatia fedha za kigeni.
Mwisho
Ikulu
14 Februari, 2006