PRESS SECRETARY TO THE PRESIDENT

 

Fax. No. 255-22 2113425                                   The State House,                        

Tel: 255-22-2116539/2116913                        P.O. Box 9120,

                                                                              DAR ES SALAAM.

E-mail:  press@ikulu.go.tz

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

 

NORWAY KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA TANZANIA                   …………. 1

 

Na Mwandishi Maalum

CAPE TOWN

AFRICA YA KUSINI

1/6/2006

 

 

Norway imeelezea nia yake ya kuendeleza ushirikiano wake na Tanzania, licha ya kuwa  nchi hiyo ina serikali mpya.

 

Udhibitisho huo umetolewa jana na Waziri  wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway, Bw. Erick Solheim, wakati alipomtembelea Rais Jakaya Kikwete  na kisha kuwa  na mazungumzo  naye, mazungumzo yaliyolenga katika kukuza na kuendeleza  uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano  wa kimaendeleo kati ya mataifa hayo mawili. Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa na Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Bw.Juma Ngasongwa.

 

Bw. Solheim ambaye yuko hapa Cape Town kuhudhuria mkutano wa uchumi katika Afrika, alimweleza Rais ambaye naye ni miongoni mwa maraisi wachache walioalikwa kushiriki mkutano huo wa siku tatu, kwamba, licha ya kuwa hivi sasa nchi yake  ina serikali mpya, lakini sera za ushirikiano kati yake na Tanzania hazijabadilika.

 

Na kwa sababu hiyo,alisisitiza kuwa  serikali yake itaendelea ushirikiano wake na Tanzania, ushirikiano utakaolenga kuleta maendeleo endelevu kati ya mataifa hayo mawili.

 

Alisema kuwa Norway inaridhishwa na hatua mbalimbali ambazo Rais Kikwete amekuwa akizitekeleza katika maeneo mbalimbali ya ukuzaji wa uchumi, kuwaletea maendeleo wananchi na vita dhidi ya rushwa.

 

Kuhusu Rushwa, Waziri huyo wa maendeleo ya kimataifa, alisema serikali yake inatiwa moyo sana na namna Rais Kikwete alivyolivalia njuga  tatizo hilo na

NORWAY KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA TANZANIA                   …………. 2

 

 

kumhakikishia ushirikiano wa kutosha katika kukabiliana nalo, ingawa inahitajika kazi kubwa katika kukabiliana na rushwa.

 

Aidha alimpongeza Rais Kikwete kwa uamuzi aliouchukua wa kushughulikia hali ya kisiasa katika visiwa vya Zanzibar na kusisitiza kuwa wapo pamoja naye.

 

Bw. Solheim alisema kuwa nchi yake itakuwa tayari kutoa msaada wa wataalam wenye uzoefu katika fani mbalimbali, kuja nchi Tanzania na kutoa uzoefu wake pale watakapohitajika. Na kuongeza kuwa wanaunga mkono vipaumbele alivyoamua kuvipa umuhimu wa pekee.

 

Kwa upande wake Rais Jakaya Kikwete aliishukuru  serikali ya Norway kwa misaada yake ya kimaendeleo ambayo imekuwa ikiipatia Tanzania kwa takribani miaka 40 ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

 

Alisema kuwa yeye binafsi ni mmoja wa wananchi walionufaika na misaada ambayo Norway imeipatia Tanzania hususani katika sekta ya elimu, ambapo Rais alisoma katika shule ya Sekondari ya Kibaha ambayo ni matunda ya msaada wa Norway.

 

Rais aliyataja baadhi ya maeneo ambayo alisema kuwa atahitaji ushirikiano wa karibu katika kuyatekeleza.

 

Baadhi ya maeneo hayo ni ujenzi wa chuo kikuu kipya,ambacho alisema kuwa kinahitajika kujengwa ili kutoa nafasi kwa maelfu ya watoto wa Kitanzania ambao licha ya kufanya vizuri katika mitihani yao, lakini wanakosa nafasi ya kujiunga na elimu ya juu.

 

Alisema kuwa hatachoka kuomba msaada wa kusaidiwa kujenga chuo kikuu kipya, ili kuepuka kuwa na taifa litakalokuwa na wananchi walioishia na elimu ya sekondari tu.

 

Eneo jingine ambalo alisema kuwa atahitaji kusaidiwa katika utekelezaji ni eneo la Sekta ya Afya hususani katika kukabiliana na tatizo kubwa la vifo vya wanawake vinavyotokana na uzazi.

 

Alisema kuwa kutokana na uwezo mdogo wa usambazaji wa huduma hiyo muhimu kwa wananchi walio wengi,  kumekuw na ongezeko kubwa la idadi ya wanawake wanaofariki dunia kutokana na matatizo ya uzazi.

 

Aliongeza kuwa serikali imeweza kukabiliana vema na kupunguza idadi ya vifo vya watoto wadogo wanaofariki dunia chini ya umri wa miaka mitano, lakini hali ni kinyume  kwa upande wa wanawake hali aliyosema inamtia hofu sana na hivyo mikakati ya makusudi inatakiwa kuchukuliwa ili kunusuru maisha ya wanawake hapa nchini.

 

Kuhusu suala la Rushwa,  Rais alisema kuwa serikali yake inafahamu vema ukubwa na ugumu wa kukabiliana na tatizo hilo.

NORWAY KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA TANZANIA                   …………. 3

 

 

 

Alibainisha kuwa juhudi zake hizo, zinalenga hasa katika kuwaelimisha wananchi kuichukia na kukataa rushwa, na siyo kuangalia ni watu wangapi wamefungwa kwa rushwa.

 

"Tunataka kupunguza idadi ya watu wanaopokea na kutoa rushwa, kwa kuwaelimisha kuwa rushwa ni mbaya, ni uovu," alisisitiza.

 

Alisema kuwa anachoomba kutoka kwao  ni  kuona kuwa ushirikiano  kati ya mataifa hayo mawili unaendelea kustawi na kuwa endelevu  na utakaokuwa na manufaa kwa pande zote mbili.

 

Mwisho