PRESS SECRETARY TO THE PRESIDENT

 

Fax. No. 255-22 2113425                                                  The State House,                        

Tel: 255-22-2116539/2116913                                           P.O. Box 9120,

                                                                                           DAR ES SALAAM.

E-mail:  press@ikulu.go.tz

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

 

JK KUHUDHURIA MKUTANO WA KIMATAIFA WA MAZIWA MAKUU

 

Rais Jakaya Kikwete anaondoka nchini kesho mchana (13 Desemba, 2006) kwenda Nairobi, Kenya ambako atashiriki katika mkutano wa siku mbili wa  Kimataifa Kuhusu Maziwa Makuu.

 

 Katika  mkutano huo, ambao utafanyika siku ya Alhamisi na Ijumaa Rais Jakaya Kikwete atamkabidhi uenyekiti wa mkutano huo, Rais Mwai Kibaki wa Kenya.

 

Mkutano wa kwanza  wa Kimataifa kuhusu Maziwa Makuu ulifanyika nchini Tanzania Novemba 20, 2004 ambapo Tanzania ilikuwa mwenyeji. Mkutano huo ulitoka na tamko la Dar es Salaam kuhusu amani, utulivu, demokrasia na maendeleo katika eneo la maziwa makuu.

 

Aidha Waziri wa Mambo ya Nje  na Ushirikiano wa Kimataifa Asha-Rose Migiro anatarajiwa  katika nafasi yake kama Mwenyekiti wa RIMC anayemaliza muda wake  kuwasilisha taarifa ya utekelezaji. Atawasilisha taarifa hiyo katika kikao cha ndani.

 

Mkutano huo  wa Nairobi, unatarajiwa kuhudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka  nchi za msingi (core) 11 ambazo ni Angola, Burundi, Afrika ya Kati, Jamhuri ya Congo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda  na Zambia. Nyingine ni Botswana, Ethiopia, Malawi, Msumbiji, Nambia, Afrika ya Kusini na Nigeria.

 

Aidha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayemaliza muda wake, Bw. Koffi Annan anatarajiwa kuzungumza katika mkutano huo.  Wengine watakaozungumza ni  Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika,  Rais Denis Sassou-Nguesso wa Kongo.

 

Washiriki wengine ni kutoka  nchi za Afrika ambao ni wajumbe wa  kundi la nchi rafiki,  kundi la nchi marafiki wa maziwa makuu zikiongozwa na wenyeviti wenza ambao ni Canada na Uholanzi, Pamoja na wawakilishi mbalimbali kutoka Asasi za Umoja wa Mataifa, Jumuia ya Ulaya, NEPAD na ADB.

 

Mkutano huu umeandaliwa kwa  ushirikiano wa Umoja wa Mataifa na Jumuia ya Afrika.

 

 Rais na Ujumbe wake anatarajiwa kurejea nyumbani mara baada ya mkutano huo.

 

Mwisho

 

Ikulu

12/12/2006