PRESS SECRETARY TO THE PRESIDENT

 

Fax. No. 255-22 2113425                                                  The State House,                        

Tel: 255-22-2116539/2116913                                           P.O. Box 9120,

                                                                                           DAR ES SALAAM.

E-mail:  press@ikulu.go.tz

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

 

 

TANZANIA KUPELEKA JESHI POLISI 77  KULINDA AMANI LEBANON

 

  • Wamo Wanawake 10
  • Ni kufuatia ombi la Umoja wa Mataifa
  • JK awaasa kuzingatia nidhamu

 

Na Maura Mwingira

IKULU

12/12/2006

 

Rais Jakaya Mrisho  Kikwete na Amiri Jeshi Mkuu leo amekagua maandalizi ya kikundi cha Polisi Jeshi 77  (Military Police) ambao wamekamilisha mafunzo na maandalizi  ya vifaa mbalimbali tayari kwenda nchini Lebanon kushiriki zoezi la kulinda amani nchi humo.

 

Polisi Jeshi hao ambao ni maafisa 11 na askari 66 wanatoka katika Kombania ya 603 ya   Jeshi Polisi katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) iliyoko Ukonga jijini Dar es Salaam. Kati  yao wapo  wanawake 10 Afisa mmoja na askari 9

 

Akizungumza na maafisa na askari hao mara  baada ya kuona zoezi fupi  la majukumu wanayokwenda kufanya huko, pamoja na kukagua vifaa; Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete alisema kuwa  maafisa na askari hao, ni vema wakatambua kwamba wamepewa heshima kubwa ya kwenda kuiwakilisha Tanzania na Jeshi lao  katika kazi ya kulinda amani.

 

 

“Kuna mambo matatu ambayo nataka myatambue, kwanza mmepewa heshima kubwa nyinyi binafsi ya kwenda kushiriki zoezi hili, na mkifanya vizuri mtapata sifa wenzenu watawasifia na kusema kumbe Watanzania ni wazuri”.  alisema

 

Na kuainisha jambo la pili kwamba kwa kwenda kwao kushiriki zoezi hilo  ni heshima kwa Jeshi la  Wananchi wa Tanzania,  ambalo kwa muda mrefu limekuwa likiombwa kwenda kushiriki shughuli za kulinda amani. Na kwamba utendaji kazi mzuri utatoa fursa zaidi kwa JWTZ kushiriki katika mazoezi hayo.

 

“Na jambo la tatu mtambue kwamba mnabeba heshima ya Tanzania nzima na  hili si jambo geni kwenu. Sina wasiwasi kwamba  mtafanya kazi vizuri na nchi itapata heshima na jeshi litapata heshima  nawatakia kazi njema”.

 

Akitoa nasaha  hizo mbele ya Mkuu  wa Majeshi  General George Waitara , Naibu Waziri wa  Wizara ya Ulinzi na JKT, Mhe. Omar Yussuf Mzee na maafisa wengine wa JWTZ, Rais aliwasisitiza maafisa na askari hao  kwamba wanakwenda nchi ya watu  na ugenini na hivyo ni lazima wakaishi vizuri na askari kutoka nchi nyingine.

 

Aliwataka  pia askari hao kuishi vizuri na raia wa Lebanon  huku wakichukua tahadhari kubwa ya kutoingia mitaani na kuanza kufanya urafiki na raia au kufanya miradi itakayoleta aibu kwa   jeshi na  nchi na kwamba hilo ni jambo la msingi sana.

 

Amiri Jeshi Mkuu alisema kuwa  uamuzi wa Tanzania kutoa kikundi hicho cha Jeshi Polisi kwenda  kulinda amani nchini Lebanon umetokana na maombi yaliyowasilishwa kwake na Umoja wa Mataifa ya kuitaka Tanzania kushiriki katika shughuli za kulinda amani.

 

Alibainisha kwamba kwa muda mrefu Umoja wa Mataifa umekuwa ukiiomba Tanzania kutoka vikosi vyake, lakini Tanzania pamoja na nia nzuri na ahadi ya kushiriki katika shughuli hizo ilishindwa kufanya hivyo kutokana na ukwasi.

 

Alisema kuwa Tanzania inapewa nafasi na heshima kubwa na inaaminiwa  kuwa ni nchi makini ambayo inapaswa kushiriki katika shughuli za kulinda amani Duniani.

 

Aliwahakikishia  maafisa na askari hao na JWTZ kwamba serikali itafanya kila lililo ndani ya uwezo wake kuwapatia mahitaji yote wanayohitaji ili kurahisisha utendaji wa majukumu  yao wawapo nchni Lebanon.

 

Akitoa taarifa fupi ya maandalizi ya kikundi hicho, Mkuu wa Majeshi, Jeneral George Waitara, alimweleza Amiri Jeshi Mkuu, kwamba JWTZ  pamoja na kutoa maafisa na askari hao 77 pia limeandaa na kutoa malori manne yenye uzito wa tani tano yakiwa yamefungwa vifaa vyote vya mawasiliano na kupakwa rangi nyeupe na nembo ya UN.

 

 

“Amiri Jeshi Mkuu ulituagiza  tuandae kikundi cha kwenda Lebanon kushiriki zoezi la kulinda amani, ninayo furaha kukueleza kuwa agizo lako tumelitekeleza na maandalizi yote yamekamilika na maafisa na askari  na vifaa viko tayari”, akasema Waitara.

 

 

Alieleza kwamba  JWTZ pia  imetoa magari 17 aina ya Landrover, mbwa wawili  kwa ajili ya shughuli za kunusa mabomu, vifaa vya malazi, burudani na fedha za awali za kujikimu kwa maafisa na askari hao.

 

Jenerali Waitara allisema kuwa gharama zote za maandalizi ya maafisa askari na vifaa hizo zimetolewana Jeshi lenyewe, na kwamba zitarejeshwa na Umoja wa Mataifa.

 

Alieleza kuwa hii ni mara ya kwanza kwa JWTZ kupeleka askari wake nje wa bara la Afrika na kwamba hatua hiyo ni changamoto kubwa wa Jeshi.

 

Aidha alisema kuwa wakaguzi kutoka Umoja wa Mataifa wameridhishwa na maandalizi ya maafisa na askari hao, pamoja na vifaa vilivyotolewa na jeshi hilo.

 

Polisi Jeshi hao 77 moja ya jukumu lao kuu litakuwa ni kutoa ulinzi kwa askari wenzao wapatao 9,000 kutoka nchi sita ambao wako  tayari nchi Lebanon.

 

Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania   kupeleka vikosi yake kulinda amani kwa vitendo, baada ya kusimamisha zoezi hilo katika miaka ya 90, mara ya mwisho askari walipelekwa Liberia ambako walipata matatizo kadhaa yakiwamo  ya kutolipwa fedha zao.

 

Tangu wakati huo, Tanzania ilikuwa ikipeleka askari wake katika nafasi ya utazamaji. (Observation) tu.

 

Mwisho.