PRESS SECRETARY TO THE PRESIDENT

 

Fax. No. 255-22 2113425                                            The State House,                  

Tel: 255-22-2116539/2116913                                     P.O. Box 9120,

                                                                                     DAR ES SALAAM.

E-mail:  press@ikulu.go.tz

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

 

BALOZI  WA TANZANIA   ATEULIWA KUWA KATIBU MTENDAJI UKANDA WA MAZIWA MAKUU

 

 

Na Maura Mwingira

15/12/2006

Nairobi Kenya

 

Tanzania imetoa Katibu Mtendaji  wa kwanza kuongoza  Sekretarieti ya Ukanda wa Maziwa Makuu.

 

Aliyeteuliwa na kupitishwa kwa kauli mmoja, ni Balozi Liberata Mulamula kutoka Tanzania akiwa ni mwanamke wa kwanza kushika  wadhifa  huo kwa kipindi cha miaka minne.

 

Tanzania, tumepewa nafasi ya kutoa Katibu Mtendaji (Executive Secretary), na kwa sababu jambo hili ni la haraka, ninamleta kwenu mwanadiplomasia maarufu, mwenye uzoefu na sifa zote, naye ni Balozi Liberata Mulamulaakatangaza  Rais Jakaya Kikwete.

 

Mara baada ya tangazo hilo,  ukumbi mzima uliojaa wajumbe waliokuwa wakihudhuria mkutano wa siku mbili wa  Kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu ulilipuka kwa shangwe na vigeregere hali iliyodhihirisha kukubaliwa kwa uteuzi wa Rais Jakaya Kikwete.

 

Shangwe hii inadhihirisha kukubaliwa kwa mteule wetuakasema Kikwete hali iliyoamusha shangwe tena kutoka kwa wajumbe wakiwamo kutoka Tanzania.

 

 Uteuzi huo ulidhibitishwa na kupokelewa kwa kauli moja na  viongozi wakuu wa nchi na serikali ambao ni wanachama wa Ukanda wa Maziwa Makuu.

 

Mara baada ya kutangazwa kwake  ya wajumbe waliokuwa wakifanya kazi kwa karibu na  Balozi Mulamula tangu kuanzishwa kwa Mchakato wa Ukanda wa Maziwa makuu, baada ya mkutano wa kwanza uliofanyika Dar es salaam mwaka 2004, walijipanga moja baada ya mwingine kumpongeza kwa furaha kubwa.

 

Baadaye  Balozi Liberata Mulamula akiwa amejawa na machozi ya furaha, alipita mbele ya viongozi wakuu wa nchi na serikali na kushikana nao mikono.

 

Akizungumza katika hotuba yake fupi ya kushukuru na kukubali uteuzi huo, Balozi Mulamula alisema kuwa amejawa na furaha kubwa na isiyokuwa na kufani na amefarijika sana kwa uungwaji mkono kutoka kwa viongozi na wajumbe wa mkutano huo.

 

Alisema  anaahidi kufanya kazi kwa juhudi na maarifa na kwamba atashirikiana kwa karibu na viongozi wakuu  wa nchi na serikali wa Ukanda wa Maziwa Makuu katika kuhakikisha kwamba amani, utulivu na maendeleo yanatawala katika eneo hili.

 

Aliwashukuru viongozi hao kwa imani kubwa walionyesha kwake, na hususani Rais wake Jakaya Mrisho Kikwete kwa kumteua na kwamba hiyo ni heshima kubwa sana kwake na kwa Tanzania nzima na kwamba hatawaangusha katika utekelezaji wa majukumu yake hayo makubwa.

 

Kabla ya Uteuzi huu, Balozi Liberata Mulamula alikuwa mkuu wa kitengo cha Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa Katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

 

Aliteuliwa  na kuwa balozi mwezi mwaka 2003 na Rais Benjamin Mkapa.

 

Katika Mkutano huo, Rais Jakaya Kikwete alisema kuwa Tanzania inaahidi kutoa Dola za Kimarekani 259,366 kwa ajili ya kusaidia utendaji kazi wa sekretarieti ya Ukanda wa Maziwa Makuu na Dola  500,000 kwa ajili ya mfuko maalum wa Ustawishaji na Maendeleo.

 

Ofisi za Sekretariati ya Ukanda wa Maziwa Makuu itakuwa Bujumbura, Burundi.

 

Katika siku ya mwisho ya mkutano wa  pili wa kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu, viongozi wakuu wa n hi na serikali waliohudhuria mkutano huo,  walitia saini Mkataba wa Usalama, Amani na Maendeleo katika Ukanda wa Maziwa Makuu.

 

Mkataba huo unaeleza kwamba wakuu wa nchi na serikali wanachama wa mkutano wa kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu, wanatambua haja ya kuheshimu demokrasia na utawala bora, misingi  muhimu iliyoainishwa ndani ya mkataba wa Umoja wa Mataifa na Mkataba wa kuanzishwa Umoja wa Afrika, ambayo ni kuheshimu mipaka ya nchi, uhuru wa nchi kujiamulia mambo yake bila ya kuingiliwa na nchi nyingine na kuondokana na  vitendo vya uchokozi, kukataa nchi mwanachama kuruhusu matumizi ya ardhi yake kama ngome ya uvamizi au kuhujumu nchi nyingine mwanachama.

 

Viongozi hao pia wamesema wanatambua haja ya kuwa na utashi  thabiti na madhubuti wa kisiasa katika kutafuta suluhu za migogoro kwa njia ya amani na  hususan kwa kuheshimu ahadi zetu  katika  hali ya kuaminiana.

 

Vile vile viongozi hao wamesisitiza dhamira ya kujenga uhusiano kati ya nchi zao kwa kufuata misingi iliyoainishwa katika hati za kisheria za kimataifa na kanuni na misingi inayokubalika duniani, vipaumbele vya kisiasa na kufuata misingi  kama ilivyoelekezwa katika  Azimio la  Dar es Salaam, pamoja na kubadilisha Ukanda wa Maziwa Makuu, kwa kusudio la pamoja, kuelekea kuwa na eneo la amani na usalama wa kudumu, eneo tulivu kisiasa na kijamii, pia kuwa na eneo lenye uchumi unaokua na maendeleo ya pamoja kupitia ushirikiano katika sekta mbalimbali kwa manufaa ya watu wao.

 

Aidha katika Mkataba huo, viongozi hao wanasema kuwa wamedhamiria kuhakikihsa utekelezaji wa misingi ya sheria za kimataifa za kibinadamu, hususani zile zinazohusiana na kulinda na kusaidia wanawake, watoto, wakimbizi na watu waliolazimika kuyahama makazi yao ambapo ukiukwaji wa wa sheria hizo  huwa na  athari mbaya kwa jamii husika.

 

Wamesema kuwa wanasisitiza uamuzi waliochukua Dar es salaam wa kuutangaza Ukanda wa maziwa Makuu kuwa  Eneo Maalum la Ustawi na Maendeleo na kwa pamoja kukabiliana na changamoto za ustawi  na maendeleo  kwa kuhakikisha ushiriki wa  wote, hususani kwa kushirikisha jumuia za kiraia, vijana, wanawake, sekta binafsi, mashirika ya dini na kwa kushirikiana kwa karibu na jumuia  muhimu za kikanda, umoja wa Afrika, umoja wa Mataifa, na Jumuia ya Kimataifa.

 

Ndani ya Mkataba huo wenye  ibara 35 viongozi hao wamedhamiria kupitisha na kutekeleza kwa pamoja mipango ya utekelezaji wa Itifaki na mifumo ya kutafsiri kwa vitendo vipaumbele vya kisiasa na kanuni elekezi za Azimio la Arusha.

 

Mwisho