PRESS SECRETARY TO THE PRESIDENT

 

 

Fax. No. 255-22 2113425                                           The State House,                               

Tel: 255-22-2116539/2116913                                     P.O. Box 9120,

                                                                                     DAR ES SALAAM.

E-mail:  press@ikulu.go.tz

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

 

 

JK-WANABUNDA UCHUKIENI UMASKINI

 

·        Asema wakiisubiri serikali watachelewa

 

Na Mwandishi Maalum

 

Rais Jakaya Kikwete ametoa changamoto kwa wananchi wa Wilaya ya Bunda kuichukia hali ya  wilaya yao kuwa ya  119 kwa umaskini nchini.

 

Nchi yetu iko nyuma sana, lakini wilaya ya Bunda ndiyo iko nyuma kuliko wote nchini. Mkuu wa wilaya aliposema wilaya yenu ni ya mwisho. Watu wa Bunda mliguna hapa. Lakini kwa hesabu, kwa viwango vya umaskini Bunda ni ya 119, hakuna wilaya nyingine iliyo nyuma ya Bundaalifafanua.

 

Alitoa changamoto hiyo jana usiku, wakati wa hafla ya chakula cha hisani ya kuchangia mfuko wa  Elimu wa Wilaya ya Bunda. Hafla hiyo ilifanyika katika hoteli ya Golden Tulip ambapo Rais Kikwete alikuwa mgeni rasmi. Alichangia 1.5 milioni.

 

AlisemaKama mnajiona tofauti basi mnajiangalia nyie mlioko mijini na suti zetu. Lakini kwa vipimo vya taifa, Bunda ni wilaya ya 119. Chukieni kuwa wa 119, msiwalaumu waliopiga  hesabu, jichukieni wenyewe kwa kufanya jitihada ili hesabu inayofuata muwe wa 102 au hata wa 10”

 

Rais Kikwete aliwaambia wageni waliohudhuria hafla hiyo wakiwamo wafanyabiashara, wawekezaji na wananchi kutoka wilaya ya Bunda na wilaya jirani,  na Mkuu wa Mkoa wa Mara Isidori Shirima, kwamba, elimu ndio jambo litakaloitoa wilaya hiyo ya Bunda hapo ilipo.

 

Alibainisha kuwa yeye (Rais) amekuwa mpiga debe mkubwa wa elimu na anafanya hivyo kwa kuamini kwamba elimu ndiyo itakayowaletea Watanzania, tofauti za  kuelekea kwenye maendeleo.

 

Rais alisema  hali ya umaskini inayoikabili wilaya hiyo si kwa sababu haina raslimali,  bali  kinachokosekana ni maendeleo ya raslimali watu watakaowezesha  raslimali zilizopo ziweze kutumika na kuleta tofauti ya maendeleo inayohitajika.

Alisema amefurahishwa sana na uamuzi uliochukuliwa na viongozi wa wilaya hiyo ya  Bunda na wananchi wake ya kuaanda hafla ya kuchangia  maendeleo ya elimu katika wilaya yao.

 

Uamuzi huu mliofanya ndio uamuzi wenyewe, mkingojea serikali mtachelewa, haya tunayofanya sisi leo hii,  wenzetu wengine waliyagundua mapema, wakajenga shule ndio maana utasikia, profesa fulani, daktari bingwa  fulani, mwishoni mnasema  hawa wana ukabila, hapana, si ukabila, wamesomaakasema na kuwafanya washiriki kuangua kicheko.

 

Alisema kuwa  jambo la msingi ni kwa wale ambao nao wamezinduka na kutambua umuhimu wa elimu  kongeza jitihada  za kuchangia katika maendeleo ya elimu badala ya kuisubiri serikali.

 

Rais Kikwete aliongeza kuwa,  serikali inatoa mgao wa fedha kwa nchi nzima, hali aliyosema kwa wale wenye mahitaji maalum inakuwa si rahisi kwao kupata zaidi.

 

Hivyo akatoa ushauri wa  wale wenye mahitaji maalum kwenda kwa watu wenye fedha ambao wana moyo wa  kutoa na kuchangia katika shughuli za maendeleo ili mradi waridhike kwamba wewe unayekwenda kuomba unayo dhamira ya dhati ya kufanya kile unachoombea.

 

Awali akitoa maelezo kuhusu maendeleo ya elimu katika wilaya hiyo ya Bunda, Mkuu wa Wilaya Bibi Chuku Gallawa, alisema kuwa jumla ya  shilingi milioni 535 zinahitajika ili  kukamilisha  uboreshaji  wa shule 24 zilizopo katika kata 20 za wilaya hiyo.

 

Kati ya fedha hizo, shilingi milioni 201.8 tayari zimekwisha kupatikana kutoka kwa wananchi wa wilaya hiyo ya Bunda na wahisani mbalimbali.

 

Katika hafla hiyo ya jana, jumla ya  milioni 286,485 zikiwa ni fedha taslimu zilipatikana, na ahadi zikiwa ni shilingi milioni 156.9 na hivyo kufanya jumla ya michango yote kuwa shilingi milioni 443.385

 

Mkuu huyo wilaya alisema kuwa fedha hizo zitatumiwa kwa malengo yaliyokusudiwa na kwamba taarifa za matumizi zitawekwa wazi

 

Alisema  kukamilika kwa shule hizo kutatoa fursa kwa wanafunzi wote 5,579 waliofaulu katika mtihani wao wa darasa la  saba  mwaka jana kuendelea na elimu ya sekondari.

 

Watu wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na baadhi ya Mawaziri na Waziri Mkuu Mstaafu, Joseph Sinde Warioba.

 

Mwisho