THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

 

 

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY TO THE PRESIDENT

 

Fax. No. 255-22 2113425                                                      The State House,             

 Tel: 255-22-2116539/2116913                                             P.O. Box 9120,

                                                                                               DAR ES SALAAM.

E-mail:  press@ikulu.go.tz                                             

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

 

WAFANYA BIASHARA WAWEZA KUKUZA KILIMO CHA AFRIKA NA

MISAADA NI MUHIMU KWA MAENDELEO.

 

PREMI KIBANGA,

JAN 26, (DAVOS, USWIS)

 

 Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema wafanyabiashara wana uwezo mkubwa wa kuleta mapinduzi ya kilimo na kukifanya kiwe chenye tija zaidi kiasi cha kuleta maendeleo na kubadili maisha ya watu wa Bara la Afrika.

 

“Wafanyabiashara waweza kufanya hivyo wenyewe, kwa kushirikiana na serikali au hata kwa kushirikiana na wakulima wenyewe popote walipo barani Afrika”

 

Rais amesema hayo jana (25.Jan.07) mwanzo wa moja ya vikao vya Baraza la Uchumi Dunian (World Economic Forum) linaloendelea Davos Uswis. Rais Kikwete alikuwa mwenza wa kikao hicho akishirikiana na Bw. Antony Burgamans, Mwenyekiti wa Uniliver huko Uholanzi.

 

“Kilimo Afrika bado ni duni wakati asilimia sabini ya watu wake wanakitegemea, hakitumii teknolojia ya kisasa na pia kinategemea sana mvua na siyo umwagiliaji na pia miundo mbinu yetu bado ni duni” amesema na kuongeza kuwa hapa ndipo wafanyabiashara wanapoweza kutumia nafasi hii kukuza na kuongeza tija katika kilimo.

 

Amesema wafanyabishara wanaweza wakaja Afrika kuanzisha mashamba makubwa ya umwagiliaji, wanaweza kujenga viwanda vyenye muelekeo wa kilimo kwa ajili ya mbolea, mbegu na hata pembejeo na pia kuweka mfumo mzuri wa masoko.

 

Ametoa mfano wa Tanzania kwamba  imeanzisha programu ya kukuza kilimo ambayo inatilia mkazo kilimo cha kisasa kwa kuhimiza umwagiliaji, mbolea na mbegu bora.

 

“Nina hakika kama tukihimiza na kukazania kilimo cha kisasa Afrika itaweza kukua kwa hivyo wafanyabishara angalieni na kwa makini sekta ya kilimo na faida zake na wekezeni kwa wingi katika Kilimo, hakika Afrika itapiga hatua ya kimaendeleoamesema.

 

Naye  Rais wa Liberia Ma Ellen Johnson Sirleaf  amewaambia washiriki kuwa Mapinduzi ya Kilimo ya nchi za Asia (maarufu kama Green Revolution) pia yanaweza kurudiwa barani Afrika ikiwa kilimo hicho kitafanyiwa utafiti wa kisayansi kwani kwa sasa bado kilimo cha Afrika ni cha matumizi kutosheleza tu na hakuna ziada na pia miundo mbinu iimarishwe na haya yote Afrika haiwezi kufanya peke yake inahitaji msaada.

 

“Afrika inawasubiri, vikwazo vyote vilivyokuwepo kama hali mbaya ya usalama na  rushwa vimeondoka na msingi wa kuanza kufanya mapinduzi ya kilimo cha Afrika umewadiaamesema Rais Ellen-Johnson Sirleaf.

 

Washiriki wa kikao hiki wametoka nchi za Afrika Kusini, Kenya, Marekani, Mexico, Msumbiji, Uholanzi, Urusi na Uingereza wakiwa ni wafayabishara, wanasiasa na viongozi wa jumuiya za kiraia.

 

Rais Kikwete pia amekuwa miongoni mwa wana jopo saba  katika mdahalo wa wazi kuzungumzia hali ya misaada inayotolewa kwa Afrika na nini matokeo yake.

 

“Misaada ni muhimu kwa Afrika, imetusaidia katika elimu, afya, maji na nishati na miundo mbinu,  tunaihitaji kwa maendeleo zaidi katika kilimo na afya”, amesema ila ameshauri kuwa wanaopewa misaada washirikishwe zaidi kwani wao ndiyo wanaojua mahitaji yao zaidi.

 

Washiriki mbalimbali walibainisha mapungufu na matatizo ya misaada kwa Afrika huku wengine wakisema inahitaji kuwepo na mfumo wa kuwajibika zaidi kwa misaada inayotolewa.

 

Baraza la Uchumi la Dunia hapa Davos, mwaka huu linazungumzia mambo ambayo ni muhimu sana kwa Afrika ikiwa ni pamoja na Afya, Elimu, Kilimo na misaada, ambapo Rais Kikwete anatumia nafasi hii kuendeleza na kuzungumzia zaidi diplomasia ya kiuchumi zaidi kwa lengo la kuvutia uwekezaji na wenza katika biashara na uchumi ili Afrika, hususan Tanzania ijikwamue kutoka kwenye umaskini.

 

Mwisho.