THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

 

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY TO THE PRESIDENT

 

Fax. No. 255-22 2113425                                                     The State House,

Tel: 255-22-2116539/2116913                                              P.O. Box 9120,

                                                                                              DAR ES SALAAM.

E-mail:  press@ikulu.go.tz                                             

 

 

JK-TANZANIA KUFUNDISHA MAAFISA KADETI WA JESHI LA SOMALIA

 

Na Maura Mwingira

29/01/07

ADDS ABABA

ETHIOPIA

 

Tanzania imeahidi kutoa mafunzo kwa maafisa kadeti kutoka jeshi la serikali ya mpito nchini  Somalia.

 

Ahadi hiyo imetolewa leo na Rais Jakaya Kikwete wakati alipokutana na kufanya mazungumzo Rais wa Serikali ya Mpito ya Somalia, Mhe. Abdullahi Yusufu Ahmed. Viongozi hao wawili wapo hapa Addis Abba kuhudhuria mkutano wa Nane wa Umoja wa Afrika.

 

Rais Kikwete alisema kuwa uamuzi wa Tanzania kutoa mafunzo wa askari wa nchi hiyo kunafuatia ombi lililotolewa na Mjumbe maalum wa Rais Mwai Kibaki kwake ambaye aliiomba Tanzania kuchangia katika ulinzi wa amani nchini Somalia.

"Ninapenda kuhakikisha Mhe. Rais, kwamba sisi Tanzania, katika udogo wetu tunatoa ahadi ya kutoa mafunzo maafisa kadeti wa jeshi lako, tuambie mahitaji yako na sisi tutakusaidia'. Alisema Kikwete.

 

Aliongeza kwamba Tanzania haiwezi kupeleka kisosi cha kulinda amani kwa kuwa tayari kimeshapeleka kikosi chake nchini Lebanon. Na kufafanua kwamba ingawa ina askari wa kutosha lakini haina vifaa kama vile magari ya kivita, silaha na zana nyingine.

 

Rais Kikwete alibainisha kwamba, Jeshi la wananchi wa tanzania liko tayari kutoa mafunzo hayo, nchi Tanzania pale somalia itakapo kuwa tayari kutoa askari wake.

Kikwete aliongeza kuwa kwa kuwa mahitaji ya Somalia ni ya haraka, mafunzo hayo yatatolewa katika mtindo wa programu maalum ambapo yatafanyika katika kipindi cha miezi sita badala ya mwaka mmoja kama ilivyo kawaida ya mafunzo ya maafisa kadeti.

 

"Leo hii nitazungumza na mkuu wangu wa majeshi ili aandae timu ya wataalamu watakaokuja Somalia na kukaa na wataalamu wenu ili waweze kujadiliana kwa kina na kuandaa programu hiyo.

 

Katika mazungumzo hayo ambayo pia yalihudhuriwa na Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Membe, Rais Kikwete alimweleza Rais wa serikali ya Mpito ya Somalia, kwamba achague pia maafisa ambao watapewa mafunzo kwa lengo la kwenda kuwafundisha wenzao.

 

Aidha Rais Kikwete alishauri kwamba kwa kuwa serikali hiyo ya mpito iko katika mpango wa kuliunda upya jeshi lake, itakuwa vizuri askari watakaochaguliwa kwenda kuchukua mafunzo hayo wawe ni vijana wasiozidi miaka 35.

Alisema kuwa uwezo wa JWTZ katika utoaji wa mafunzo hayo ni kwa askari kati ya 100 hadi 200.

 

Rais Kikwete pia alimpongeza Rais huyo wa serikali ya mpito nchini Somalia kwa juhudi kubwa anazofanya za kurejesha hali ya amani na utulivu nchini Somalia.

Kwa upande wake, Kiongozi huyo wa serikali ya mpito ya somalia, Abdullahi Yusuf Ahmed, alimshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa mchango huo.

"huu ni mchango mkubwa sana na muhimu kwetu, utatusaidia sana hasa ikizingatiwa kwamba ni miaka mingi wanajeshi wetu hawajapata mafunzo, kiasi kwamba wengine wameshasahau baadhi ya mambo" alisema.

 

Aliongeza kwamba, kwa kuanzia wangependa askari wao 1000 wapatiwe mafunzo hayo yakiwamo yale ya kujikumbusha, (refresher course).

 

Tayari Tume ya Umoja wa Afrika imekwisha kutaarifiwa juu ya mchango huo wa Tanzania katika mchakato mzima wa kurejesha hali ya amani na utulivu nchini Somalia.

 

Awali akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huu wa nane, Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Bw. Alpha Konare, alisema kuwa Nchi za umoja huo ni lazima zipeleke kwa haraka vikosi vya kulinda amani nchini humo.

 

Alibainisha kwamba kama umoja huo hautafanya hivyo haraka iwezekanavyo, hali nchini Somalia itazidi kubwa mbaya, kiasi cha kuziathiri nchi nyingine.

 

Akiongea kwa uchungu, Bw. Konare alisema kuwa nchi za Afrika zifikie mahali ziachane na utegemezi wa kutegemea mataifa mengine ya nje kuja kusadia ulinzi wa amani katikaAfrika, ingawa misaada yao inahitajika.

 

Alisema jumla ya askari 8000 wanahitajika haraka Somalia, na kwamba hadi sasa ni nchi za Uganda, Malawi, Nigeria na Ghana ndizo zimeahidi kutoa askari wake, huku Algeria ikiahidi kutoa msaada wa kusafirisha askari hao kwenda Somalia.

 

"Ndugu zangu hatuwezi kuendelea kutegemea mataifa ya nje yatusaidie, natoa wito tena nchi zote za Afrika kutenga raslimali za kuisaidia Somalia", alisisitiza.

Hata hivyo Bw. Konare alisema haitoshi kupeleka vikosi vya kulinda amani huko Somalia, bali lazima pia pawepo na suluhisho la kisiasa kati ya serikali ya mpito na vikundi vinavyopingana la sivyo majeshi hayo yatakuwa kama vile yamekwenda kuikalia Somalia.

 

"Somalia wenyewe wawe na suluhu la kisiasa, na wawe tayari kujadiliana na kikundi cha kiislamu kinachotumia vikundi vyenye silaha kuchukua madaraka. ili Somalia ipate utulivu" alisema Konare.

 

Mwisho