THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

 

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY TO THE PRESIDENT

 

Fax. No. 255-22 2113425                                                  The State House,                           Tel: 255-22-2116539/2116913                                      P.O. Box 9120,

                                                                                           DAR ES SALAAM.

E-mail:  press@ikulu.go.tz                                             

 

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

 

TANZANIA NA TRINIDAD NA TOBAGO KUSHIRIKIANA KATIKA GESI.

 

 Viongozi wa Tanzania, Trinidad na Tobago wamekubaliana kushirikiana  katika kutafiti na kuendeleza gesi hapa nchini.

 

Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Trinidad na Tobago wamekubaliana hayo wakati wa mazungumzo yao leo katika Ikulu ya Dar-es-Salaam.

 

Tanzania ina hifadhi ya gesi katika maeneo matatu hadi sasa, maeneo hayo ni Songosongo, Mnazi Bay na Mkuranga eneo ambalo limegundulika hivi karibuni.

 

“Kuna maeneo mengine kadhaa ambayo yanasemekana yana hifadhi ya gesi, bado utafiti unaendelea katika gesi na petroli pia,” Rais Kikwete amemueleza Waziri Mkuu wa Trinidad na Tobago Mheshimiwa Patrick Manning.

 

“Gesi ni kitu cha thamani sana, Trinidad na Tobago tumefanikiwa  kupunguza matatizo ya umeme kwa ajili ya gesi  na pia ni chanzo kizuri sana cha kukuza sekta ya viwanda, sisi imetusaidia sana na tuna uzoefu sana nayo kwa hiyo tuko tayari kuwasaidia katika stadi mbalimbali kuhusu gesi,” Bwana Manning amemwambia Rais Kikwete. Na kueleza kuwa Tanzania itapiga hatua kubwa kiuchumi ikiitumia gesi yake vizuri.

 

Nchi ya Trinidad na Tobago imefanikiwa kiuchumi kutokana na sekta ya nishati hususan gesi na petroli ambapo mwaka 2006 uchumi wake ulikuwa hadi asilimia 12 kutoka asilimia 8 mwaka 2005 na pato la taifa kutokana na sekta ya nishati ni asilimia 41.2.

 

Trinidad na Tobago ina watu wapatao milioni 1.3  wakiwemo  wenye asili  ya Afrika, India,  Ulaya, China, Mashariki ya Kati na watu wenye asili mchanganyiko.

 

Waziri Mkuu wa Trinidad na Tobago yuko nchini kwa ziara ya siku tatu kufuatia mwaliko wa Rais Kikwete.

 

Kesho (02.Feb. 07) Bwana Manning atatembelea Zanzibar kabla ya kuelekea Manyara. Jumamosi (03 Feb. 07) ataelekea Bagamoyo kutembelea maeneo ya kihistoria na baadaye kuondoka nchini.

 

Baada ya Mazungumzo yao, Rais na mgeni wake walishirika dhifa ya kitaifa, iliyoandaliwa kwa heshima ya Bwana Manning.

 

Mwisho.

 

 

Imetolewa na Premi Kibanga,

Ikulu-Dar-es-Salaam

1 Feb, 07