PRESS SECRETARY TO THE PRESIDENT

 

Fax. No. 255-22 2113425                                                  The State House,                               

Tel: 255-22-2116539/2116913                                           P.O. Box 9120,

                                                                                           DAR ES SALAAM.

E-mail:  press@ikulu.go.tz

 

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

 

Premi Kibanga,

Addis Ababa,Ethiopia

25 April, 07

 

Mapungufu yaliyo dhahiri katika sekta isiyo rasmi,  ni changamoto kubwa kwa nchi za Afrika katika kutekeleza ajenda yake ya kuwa na ajira zenye hadhi kwa watu wake.

 

Rais Jakaya Kikwete amewaeleza washiriki wa mkutano wa 11wa Kanda ya Afrika wa shirika la kazi duniani (ILO), jana katika hotuba yake ya ufunguzi unaozungumzia ajira zenye hadhi barani.

 

“Kama mjuavyo wananchi wengi wanafanya kazi katika sekta isiyo rasmi kwa kutopenda kwa vile hakuna ajira mbadala ya kuwawezesha kujikimu kimaisha,  sekta hii huwa  mkombozi wao kwa vile ina masharti mepesi kujiunga nayo kama vile elimu ndogo, haihitaji ujuzi, teknolojia na mtaji wake ni mdogoamesema na kueleza kuwakutokana na hilo, kazi katika sekta isiyo rasmi mara nyingi hazina hadhi sana na hii ndiyo changamoto kubwa kwa nchi za Afrika na jambo kuu la kuzungumzia na kutafuta ufumbuzi wake na kuhakikisha tunatetea na kulinda wananchi walioko katika sekta hii isiyo rasmi.”

 

Amezitaja baadhi ya changamoto zilizo dhahiri kuwa ni watu kutokuwa na kinga, haki ya kuwakilishwa na hivyo kuwafanya wabaki katika hatari ya kudhulumiwa na kunyanyaswa na kuzidi kudidimia katika lindi la umaskini.

 

Rais ameipongeza ILO kwa kulibaini hilo na kupigania haki za wafanyakazi katika sekta isiyo rasmi na kutoa wito kwa wadau wote kuimarisha na kutafuta njia, kuweka mikakati dhabiti ya kutatua mapungufu hayo.

 

Tanzania ni miongoni mwa nchi za mwanzo barani kati ya 53 ambazo zimeridhia mikataba mikuu nane ya msingi ya shirika la kazi duniani na kasha kuziingiza katika sheria za kitaifa hivyo kujenga mazingira mazuri kwa sekta binafsi kufanya shughuli zao na kuwalinda wafanyakazi.

 

Hata hivyo Rais amebainisha kuwa utekelezaji wa  mikataba hii bado ni changamoto kubwa ambalo utaalamu na ujuzi wa shirika la kazi duniani unahitajika.

 

Mikataba iliyoridhiwa ni pamoja na ule unaohusu kima cha chini cha umri , marupurupu sawa, haki na uhuru wa kukusanyika, ajira za lazima, ajira za watoto, ubaguzi katika ajira na ule unaohusu wafanyakazi katika vyombo vya majini.

 

Ufunguzi wa mkutano huo umehudhuriwa pia na Rais Campaore wa Burkina Faso na Waziri Mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi, Rais wa Bunge la Afrika, Balozi Getrude Mongela, Mawaziri wanaohusika na Ajira barani Afrika, mabalozi wanaowakilisha nchi zao walioko Addis Ababa, Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya, NEPAD, ILO, Viongozi wa Vyama vya waajiri na waajiriwa barani na wadau wa ajira duniani na utahitimishwa tarehe 27 April, 07.

 

Rais Kikwete amerejea nchini leo alasiri.

 

Ends.