PRESS
SECRETARY TO THE PRESIDENT

The State House,
Tel:
Fax. No. 255-22 2113425 DAR ES SALAAM.
E-mail:
press@ikulu.go.tz
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais Jakaya Kikwete leo amekuwa na mazungumzo na
ujumbe wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) ulioongozwa na Bw. Zhang De Jiang, mjumbe wa Kamati ya
Siasa ya Kamati Kuu ya CPC akiwa pia
ni Katibu wa Kamati ya Chama ya Jimbo la
Guandong.
Katika mazungumzo hayo, Rais na mgeni wake
walijadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu namna Tanzania na China
zinavyoweza kuongeza kasi ya ushirikiano hususani katika sekta za biashara na
uchumi.
Bw. Zhang De Jiang alimweleza Rais kwamba ziara yake hapa nchini ina malengo ya kukuza na kuendeleza uhusiano wa kibiashara
na kiuchumi kati ya Tanzania na jimbo
hilo la Guangon, jimbo ambalo ni moja
kati ya majimbo yanayofanya vizuri kiuchumi
na kuchangia katika pato la taifa la China. GDP ya jimbo hilo ni dola za
Kimarekani 330 milioni kwa mwaka na inachangia moja ya nane ya pato la China.
Bw. Zhang De Jiang amesema, pamoja na kwamba katika ziara yake hii
imefuatana na wajasiriamali 200, ambao
kesho watakutana na wajasiriamali wa Tanzania na kubadilishana nao uzoefu,
atatumia ujumbe mwingine wa wafanyabiashara utakaoongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Jimbo hilo.
Amefafanua kwamba kazi ya ujumbe huo itakuwa ni
kuchambua sera na vivutio vya uwekezaji vilivyopo hapa nchini ambavyo kwayo
vitatumika katika kutoa maamuzi ya maeneo ya kuja kuwekeza hapa nchini.
Kiongozi huyo wa ujumbe wa CPC, amesema
Tanzania chini ya uongozi wa Rais Jakaya
Kikwete inayo mazingira na fursa nzuri ya kuendelea kiuchumi, kibiashara na
kijamii.
Amesema hali ya amani na utulivu
iliyopo nchini, ni moja ya vivutio vikubwa vya uwekezaji hasa uwekezaji wa
kutoka nje.
Aidha amebainisha kwamba uadilifu wa
Watanzania, uhodari wao wa kazi, uwingi wa raslimali ni moja ya mambo ambayo yanawavutia wawekezaji
kuja Tanzania.
Bw. Zhang De Jiang pia amemweleza Rais
kwamba, ikiwa Tanzania itafungua zaidi milango ya uwekezaji kutoka nje, kama lilivyofanya jimbo hilo ambalo yeye ndiye
kiongozi wake, si tu kutachangia katika ukuaji wa uchumi, lakini pia
kutaiwezesha reli ya Tazara kufufuka na
kufanya kazi kwa ufanisi na tija.
Amesema China imeweza kufanya vizuri katika
mageuzi yake ya kiuchumi baada ya kufanya marekebisho makubwa na kufungua milango ya uwekezaji kutoka nje,
huko jimbo hilo la Guandong likiwa la kwanza katika utekelezaji wa mageuzi hayo
na kuvutia wawekezaji kutoka nje.
Amefafanua kwamba China imefika hapo ilipo na kuwa moja ya mataifa yanayo
kuja juu kwa kasi kwa ukuaji wa uchumi
baada ya kupitia vikwazo vingi na machungu mengi lakini ambayo baadaye
yamekuja kuipatia neema nchi hiyo.
Dhumuni jingine la ujio wa Ujumbe huo wa CPC ni kukidhibitishia uhusiano na
ushirikiano endelevu kati yake na Chama cha Mapinduzi.
Kwa upande wake Rais Kikwete ameeleza kufurahishwa kwake na uamuzi wa jimbo hilo la Guandong la
kuleta nchini wafanyabiashara na kutaka kupanua kuwa na uhushirikiano endelevu wa kibiashara
na uchumi kati yake na Tanzania.
Amesema Tanzania inayo mengi ya kujifunza kutoka
China, na kuongeza kuwa kupitia mipango mathubuti, sera nzuri na utekelezaji makini wa maamuzi mbalimbali, Tanzania pia
inaweza kuondoka katika umaskini wake na kuwa nchi iliyoendelea kama ilivyofanya
china.
Amesema serikali inaukaribisha ujumbe huo wa
wafanyabishara na kuhakikisha kwamba utapewa
ushirikiano wa kila hali ili
hatimaye, waweze kuwekeza na kufanya biashara na Watanzania.
Rais aliainisha mambo kadhaa yakiwamo
mazingira mazuri ambayo serikali imeyaandaa kwa ajili ya kuvutia
wawekezaji wa ndani na nje.
Mazungumo kati ya Rais na ujumbe huo wa CPC pia ulihudhuriwa na viongozi wa
Chama cha Mapinduzi wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama, Bw. Jaka Mwambi
Mwisho.
Ikulu
Dar es Salaam.
11 Juni 2007