PRESS SECRETARY TO THE PRESIDENT OF THE
UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

The State House,
Tel: 255-22-2116539/2116913 P.O. Box 9120,
Fax. No. 255-22 2113425
DAR ES SALAAM.
E-mail:
press@ikulu.go.tz TANZANIA.
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
TAARIFA YA MHE. JAKAYA MRISHO
KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KUHUSU MAZUNGUMZO YA MUAFAKA
KATI YA CUF NA CCM
Tarehe
7 Agosti, 2007, Mwenyekiti wa Chama cha Civic
United Front (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alitoa tamko la kuelezea
kukwama kwa mazungumzo ya muafaka kati ya Chama chake na Chama cha Mapinduzi
(CCM). Katika tamko hilo, Profesa Lipumba alielezea nia yake na ya Chama chake ya
kujiondoa katika mazungumzo hayo ifikapo tarehe 15 Agosti 2007.
Napenda
kukumbusha kwamba chimbuko la mazungumzo yanayoendelea sasa ni ahadi niliyoitoa
kwa Watanzania wakati nilipohutubia Bunge tarehe 30 Desemba, 2005. Niliahidi kuwa nitakuwa tayari kuchukua hatua
za kutafuta ufumbuzi wa mpasuko wa kisiasa Zanzibar. Kwa ajili hiyo, nilielezea nia yangu ya
kusaidia kuanzisha na kuwezesha mjadala juu ya mustakabali wa kisiasa Zanzibar.
Ahadi
hiyo niliitoa kwa dhati ya moyo wangu nikiamini kwamba hakuna tofauti zozote za
kisiasa na kijamii katika nchi yetu au baina yetu au katika jamii zetu ambazo
haziwezi kumalizwa kwa njia ya mazungumzo. Imani hiyo bado ninayo leo na
nitaendelea kuwa nayo daima.
Ilichukua
muda kwa mazungumzo baina ya CCM na CUF kuanza.
Hii ilisababishwa na haja ya kufanya mashauriano mapana baina na
miongoni mwa wadau wa pande zote husika ndani ya Chama cha Mapinduzi na wenzetu
wa CUF. Mashauriano haya yalichukua muda
kidogo zaidi ndani ya CCM kwa sababu utamaduni na mfumo wetu wa demokrasia
ndani ya Chama cha Mapinduzi unatuwajibisha kuwa na mashauriano mapana na ya
kina katika ngazi mbalimbali za uongozi na vikao vya Chama. Nafurahi kuwa kazi hiyo ilikamilika vizuri na
tukafikia maelewano ya dhati kuwa CCM ifanye mazungumzo na CUF.
Baada
ya hapo, Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ilimuagiza Katibu Mkuu wa CCM kuwasiliana
na Katibu Mkuu wa CUF na kumuomba akubali kushiriki katika mazungumzo baina ya
vyama vyetu. Tulifarijika sana kwamba
baada ya maombi hayo ya CCM wenzetu wa CUF walikubali kukaa pamoja nasi katika
meza ya mazungumzo.
Tarehe
17 Januari, 2007, Makatibu Wakuu wa vyama vya CUF na CCM wakakutana na mchakato
wa mazungumzo ukaanza. Baada ya kikao
hicho cha mwanzo, kila upande ukaunda timu yake ya kushiriki katika mazungumzo
hayo. Tarehe 01 Februari, 2007 Kamati
yetu ya Pamoja ilifanya mkutano wake wa kwanza
ambapo walikubaliana kuwa jambo la mwanzo la kufanya ni kwa kila upande
kutengeneza mapendekezo yake ya mambo unayotaka yazungumzwe, yaani yawe kwenye
Ajenda ya Mazungumzo. Baada ya hapo
yalifanyika majadiliano mazuri na katika mazingira ya kidugu, ajenda ya pamoja
ya mazungumzo ikatengenezwa. Ajenda hiyo
ilikuwa na mambo matano makubwa kama ifuatavyo:
1. Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa
Oktoba 30, 2005 na taathira zake;
2. Usawa na haki katika
kuendesha siasa;
3. Masuala ya utawala ya
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;
4. Njia za kuimarisha mazingira
ya maelewano ya kisiasa na uendeshaji wa uchaguzi huru na wa haki Zanzibar; na,
5. Utaratibu wa kutekeleza
Programu ya Utekelezaji wa Makubaliano yatakayofikiwa katika mazungumzo haya.
Tangu
mazungumzo haya yaanze mwezi Januari mwaka huu, Kamati yetu ya Pamoja imefanya
vikao 12 na wametumia siku 43 za mazungumzo.
Pia Makatibu Wakuu nao wamekutana mara mbili kutafuta ufumbuzi wa yale
mambo yaliyohitaji kufanywa nao. Tulikubaliana
kuwa mazungumzo ya msingi yatafanywa na Kamati lakini pale ambapo Kamati
itakwama Makatibu Wakuu waingilie kati kutoa mwongozo. Ukweli kwamba wamekutana mara mbili tu ni
dalili kwamba mambo yanakwenda vizuri.
Hatua
kubwa imefikiwa na mafanikio ya kuridhisha yamepatikana. Kuna mambo kadhaa makubwa na ya msingi ambayo
pande hizi mbili zimekwishakubaliana. Katika
ajenda tano za mazungumzo, ajenda tatu, yaani ajenda ya Usawa na Haki katika Kuendesha
Siasa, Masuala ya Utawala ya Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, na Njia za Kuimarisha Mazingira ya Maelewano ya Kisiasa
na Uendeshaji wa Uchaguzi Huru na wa Haki Zanzibar, zimejadiliwa na pande zote
mbili zimefikia maelewano mazuri.
Kwa
upande wa ajenda ya kwanza inayohusu Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 30,
2005 na Taathira Zake, mazungumzo yamefanyika na maelewano yamepatikana kwa
mambo kadhaa. Yapo mambo mawili matatu
ambayo bado maelewano hayajafikiwa. Hatuna
budi tuendelee kuyazungumza mpaka tutakapopata maelewano ya pamoja.
Jambo
moja kubwa ambalo wawakilishi wa vyama vyetu bado wanaendelea kujadiliana na
ambalo bado halijakamilika ni lile linalohusu namna ya kutengeneza mazingira
yatakayowezesha vyama vya siasa Zanzibar, hususan CUF na CCM, kuishi na kuendesha
shughuli zao kwa pamoja katika hali ya maelewano na mazingira ya amani na
utulivu.
Mazungumzo
kuhusu kipengele hiki yamechukua muda na muafaka bado haujafikiwa. Kwa maoni yangu imekuwa hivyo kwa sababu ya
umuhimu wake na umakini unaotakiwa katika uchambuzi wa hoja na kufikia uamuzi. Katika mazungumzo kuna mambo rahisi yanayochukua
muda mfupi kujadiliwa na kufikiwa makubaliano na kuna mambo magumu yanayochukua
muda mrefu. Huu ndiyo uzoefu wa vyama
vyetu katika mazungumzo tuliyofanya huko nyuma na hata kwa mazungumzo haya.
Kwa
sababu hiyo, sisi wa upande wa CCM, hatudhani kama tumefikia mahali pa kusema kuwa
mambo yameshindikana na hivyo mazungumzo yavunjike. Hatujafikia hatua hiyo hata kidogo. Ni maoni yangu na ya Chama cha Mapinduzi kuwa
tuendelee kuzungumza na kila upande uboreshe hoja zake za kuushawishi upande
mwingine. Tupo kwenye mazungumzo kwa
ajili hiyo. Tupo kufanya hivyo. Naamini kwamba, kama ambavyo tumepata
maelewano katika maeneo mengine ambayo yalikuwa magumu, hata kwa haya yaliyobakia
hatimaye tutaafikiana. Wahenga walisema:
“Penye nia pana njia”. Maadam sote nia tunayo, jawabu muafaka kwetu
sote na kwa nchi yetu tutalipata.
Nawasihi
wenzetu wa CUF wasijiondoe kwenye mazungumzo haya na badala yake tuendelee
kuzungumza. Tunazungumza kwa sababu tuna
tatizo tunalolitafutia ufumbuzi. Kuacha
kuzungumza si jawabu kwani tutakuwa tunaacha
kulipatia ufumbuzi tatizo linalotusibu sote. Tutarudi kule tulikokuwa, yaani kwenye uhasama,
shutuma zisizoisha, kubaguana, kutozikana na hata kutosalimiana au kuchekeana. Tutaendelea na utamaduni mbaya wa kuzifanya
tofauti zetu za kisiasa kuwa ni chanzo cha uadui, chuki na hivyo kuhatarisha amani,
utulivu na umoja wa taifa letu na watu wake.
Ni
kweli, mazungumzo ni lazima yawe na ukomo. Na sisi wote tungependa yafikie mwisho
wake mapema inavyowezekana. Lakini, ukomo wa mazungumzo ni lazima utokane na
ridhaa ya pamoja ya pande zote na hasa kwamba ajenda zote zimepata nafasi ya
kujadiliwa kwa kina na maelewano yamefikiwa. Ukomo wa mazungumzo
usiotokana na hayo ni kuahirisha tatizo
litakalokuja kujitokeza na kutudhuru wote siku za usoni. Shabaha yetu katika mazungumzo haya ni kupata
ufumbuzi wa kudumu na endelevu kwa matatizo yanayotukabili katika uwanja wa
kisiasa nchini. Tunafanya yote hayo ili
kujihakikishia amani, utulivu, mshikamano na umoja wa taifa letu na watu wake
vinaendelea kuwepo daima dumu.
Napenda
kumaliza kama nilivyoanza kwa kukumbusha kwamba mazungumzo haya yametokana na
ahadi yangu na ya CCM. Ahadi hiyo ni ya
dhati na niliitoa kwa kujiamini na kwa kuamini kuwa hii ndiyo njia pekee iliyo
bora kuliko zote ya kushughulikia tofauti zetu.
Kwa msingi huo, ningependa na CCM ingependa kuona mazungumzo haya
yanaendelea na yanazaa matunda tunayoyatarajia sote. Nawasihi wenzetu wa CUF tuungane kuhakikisha tunafanikiwa.
Tusikubali mazungumzo yavunjike kwani gharama ya kuvunjika kwa mazungumzo haya
ni mbaya na haina maslahi kwa taifa letu na watu wake. Itahatarisha
amani na utulivu wa nchi yetu.
Ikulu
Dar es Salaam
14 Agosti, 2007