PRESS SECRETARY TO THE PRESIDENT

OF THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

 

 

 

 

                                                      

                                           The State House,

Tel: 255-22-2116539/2116913                                                    P.O. Box 9120,

Fax. No. 255-22 2113425                                                           DAR ES SALAAM.

E-mail:  press@ikulu.go.tz                                                           Tanzania.

              ikulupress@yahoo.com

 

 

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

 

Premi Kibanga,

Maswa, Shinyanga,

26.Aug, 07

 

 

Serikali imetenga Tshs 950 milioni  kwa ajili ya kukarabati bwawa la maji la Niusola wilayani Maswa ili kuwarejeshea haraka wananchi huduma ya maji kutokana na bwawa hilo kubomolewa na mvua zilizozidi kiasi.

 

Tulitoa ahadi wakati wa kampeni kwamba tutaimarisha huduma za maji wilayani hapa, tumeshaanza lakini kwa bahati mbaya mvua zimebomoa bwawa, hata hivyo tutalijenga na kurudisha huduma ya maji na  kuiboresha zaidi ili wananchi wengi wapate maji salamaRais amesema.

 

Kubomoka kwa bwawa hilo kumewaletea kero kubwa wananchi wilayani Maswa na kusababisha huduma ya maji ipatikane kwa asilimia kumi tu (10%) tofauti na awali ambapo asilimia 48.8 (48.8%) ya wananchi wamekuwa wakipata huduma ya maji.

 

Rais Jakaya Kikwete ametembelea Bwawa hilo na kuwaagiza viongozi na mkandarasi kuharakisha ujenzi wa bwawa hilo katika kipindi cha mwezi mmoja na nusu kabla mvua zingine kubwa hazijaanza mwezi Oktoba mwaka huu.

 

Mbali na hilo serikali imetoa Tsh 50 milioni kwa ajili ya kujenga visima virefu viwili (2) ambavyo tayari vimeisha chimbwa na sasa vinafanyiwa majaribio ili kutoa huduma ya maji kwa vijiji kumi wilayani Maswa.

 

Serikali pia imetoa Tsh milioni 75.42 kwa Halmashauri kwa ajili ya kutoa huduma za haraka kwa wananchi kwa kujenga visima vifupi kumi na moja ambavyo vitatoa huduma ya maji kwenye shule za sekondari, huku kukiwa na mpango mkubwa wa kusambaza maji safi na salama wilayani kote.

 

Katika kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM ya kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanapata nafasi kutoka elimu ya awali hadi chuo kikuu, Rais ameelezea kufurahishwa kwake kwa wananchi kuitikia wito wa kujenga shule na kuhakikisha kila kata ina sekondari angalau moja.

 

Wilaya ya Maswa, kama wilaya zingine mkoani Shinyanga, imefanikiwa kuingiza sekondari watoto wote waliofaulu mtihani wa kumaliza darasa la saba.

 

Rais ameingia wilaya ya Maswa akitokea wilaya ya Meatu ambako nako alitembelea miradi mbalimbali ya Maji.

 

Tunao mpango wa kupunguza matatizo ya maji na hatimaye kumaliza kabisa tatizo hili la maji kama tulivyoahidi wakati wa kampeni. Tunaanza na vijiji 10 na baadaye tutaongeza vingine kumi hadi tatizo litokomee kabisaamesema na kueleza kuwa wilaya ya Meatu nayo imetengewa Tsh 658 milioni kwa ajili ya maji.

 

Akiwa katika wilaya hizi mbili Rais, ameelezea azma ya serikali ya kuongeza tija katika kilimo.

 

Serikali itatoa ruzuku kwa wakulima ili walime vizuri zaidi, tutaajiri wataalamu na wasomi wapatao elfu mbili mia tano (2500) na kuwapeleka katika kila tarafaRais amesema.

 

Ahadi zingine ambazo ziko katika hatua ya kati ni kutengeneza barabara katika wilaya za mkoa huu wa Shinyanga ambazo zitaunganisha mkoa na mikoa mingine jirani.

 

Akiwa Mkoani Shinyanga Rais anaendelea kusisitiza na kuwahamasisha wananchi kuwa makini na kuchukua tahadhari kubwa kuepukana na ugonjwa wa Ukimwi.

Rais ataondoka Maswa tarehe 27 Agosti, 2007 kuelekea wilaya ya Bariadi ambapo pia anatarajiwa kuzindua bwawa la maji na baadaye kufungua kiwanda cha kuchambulia pamba na kuongea na wananchi.

 

Rais yuko Mkoani Shinyanga kufuatilia na kuangalia shughuli mbalimbali za wananchi na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa ilani ya CCM kama alivyowaahidi wananchi wakati wa kampeni ya kutafuta Urais.

 

Mwisho.