PRESS
SECRETARY TO THE PRESIDENT
OF
THE UNITED

The State House,
Tel:
Fax. No. 255-22 2113425 DAR ES SALAAM.
E-mail: press@ikulu.go.tz Tanzania.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI
Na Maura Mwingira
5/9/2007
MPWAPWA
Rais Jakaya
Kikwete amezitaka Wizara za Maendeleo ya Mifugo na Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa kuhakikisha kwamba wanafunzi 86 wanaomaliza mafunzo
yao katika Chuo cha Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Mifugo wanapata ajira
serikalini.
Ametoa
agizo hilo leo wakati alipoitembelea Taasisi hiyo ya Taifa ya Utafiti wa
Mifugo iliyopo Wilayani Mpwapwa, Mkoani Dodoma kukagua shughuli za Taasisi hiyo
ambayo pia inatoa mafunzo ya ngazi ya diploma na cheti katika maeneo ya
tiba za mifugo na uzalishaji wa mifugo.
Mkuu
wa Chuo hicho ambacho kilianzishwa mwaka 1935 , Dkt. Jerome Bahami,
alimweleza Rais kwamba, kwa mwaka huu chuo hicho kina wanafunzi 86 wa
mwaka wa pili na wa mwisho, na robo tatu yao wakiwa wanajilipia wenyewe,
na kwamba wengi wao hawana uhakika wa ajira baada ya kumaliza
masomo yao.
“Kwa nini
hawa wakose ajira wakati tuna uhaba mkubwa wa wataalam” akahoji Rais na
kuendelea “Huku tunasema tunataka kufanya mageuzi katika kilimo na ufugaji,
hivi kinachokwamisha hawa wasijariwe ni nini, hata kama wamelipiwa na wazazi
wao, lakini mzazi anapomlipia mwanae matumaini yake si apate ajira baada
ya kumaliza masomo yao. Fanyeni utaratibu wa kuwaajiri hawa” akasema Rais huku
akimwelekea Naibu Waziri wa Mifugo, Dkt Charles Mlingwa.
Pamoja na
kuangiza wizara husika kuwaajiri wahitimu hao, Rais pia ameshauri
kufanyiwa marekebisho au kufutwa kabisa kwa Sheria Namba Nane.
Amesema
Sheria hiyo ni kikwazo katika utoaji wa ajira hasa kwa wataalamu wa kada
maalum ambao mahitaji yao ni makubwa lakini ni wachache.
“Nchi ina shida
kubwa ya wataalamu, leo hii kwa mfano Wizara au Halmashauri inatangaza
nafasi za wataalamu wa mifugo, na wataalamu hao wako 10, halafu mnasema
ni lazima wahojiwe na madiwani, madiwani wenye elimu yao ni ya chini kuliko
wataalamu hao, hivi jamani tunakwenda wapi, sheria hii ifanyiwe marekebisho ni
ucheleweshaji wa muda tu na kuwapa watu posho,” akasema Rais.
Ameongeza
kwamba zinapojitokeza nafasi za ajira kwa kada maalum, badala ya
kuzitangaza nafasi hizo magazeti, wahusika waende moja kwa moja vyuoni na
kuwatambua watu wanaowataka, na wakimaliza masomo yao na kuthibishwa na vyuo
vyao kwamba wamefaulu vizuri basi waajiriwe.
“Haiwezekani,
wataalamu mbalimbali wakakosa ajira serikalini, kwa vile tu eti sheria
namba nane inataka kila nafasi ya ajira itangazwe kwa sababu tu wakubwa fulani
wamesema huu ndio utaratibu wa uwazi, hapana lazima tufikie mahali maamuzi
mengi tuyabadilishe tu” akasisitiza Rais
Chuo hicho
cha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo mwaka huu kinatarajiwa kuchukua wanafuzi 210
ambao watalipiwa na serikali kwa asilimia 100 na baada ya kumaliza masomo yao
wataajiliwa na serikali.
Akiwa
kwenye taasisi hiyo, Rais Kikwete alitembelea mashamba ya mifugo na kujionea
ng’ombe aina ya Mpwapwa wanaozalishwa katika taasisi hiyo, pamoja na
mbuzi aina ya Malya ambao nao huzalishwa hapo.
Rais aliwataka
wataalamu hao, kuongeza kasi ya uzalishaji wa madume ya kisasa kwa kutumia
teknolojia ya chupa, kwa lengo la kupata madume mengi ya kisasa ili kubadili
aina ya ng’ombe waliopo ambao hawazalishi nyama ya kutosha, maziwa na hata
ngozi bora.
Akasema
serikali itakafanya kila lilo ndani ya uwezo wake, kuisaidia Taasisi hiyo
na chuo chake ambavyo amesema ni muhimu sana katika utekelezaji wa
mageuzi ya sekta ya mifugo nchini.
Awali
Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Dkt Regnald Mbwile, amemweleza Rais kwamba
Taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 1905 na Wajerumani. Wakati huo ikiwa kama
kliniki ya kutibu magonjwa ya mifugo.
Amefafanua
kwamba, Tasisi hiyo ambayo ina josho la kuoshea mifugo likiwa ni la
kwanza Afrika Mashariki, lilijengwa mwaka 1905 na hadi leo hii linafanya
kazi, pia kuna vituo vya utafiti wa mifugo vitatu ambavyo ni vya
mabuki kiliochopo kanda ya Ziwa, kituo cha Utafiti wa Mifugo Uyole kilichopo
kanda ya Nyanda za Juu Kusini na kituo cha utafiti wa malisho Kongwa.
Aidha ameyaeleza malengo ya Taasisi ni kuchangia
katika kujitosheleza kwa chakula na
maendeleo ya kiuchumi kwa kufanya
tafiti sahihi na endelevu ambazo
zinalenga kuongeza tija katika mifugo
kwenye kanda mbalimbali za kilimo
nchini.
Akieleza zaidi shughuli za Taasisi
hiyo, Dkt. Mbwile amesema, Taasisi inaendeleza uzalishaji wa ng’ombe
wa aina ya
Mpwapwa ambao ni chotara kwa
ajili ya nyama na maziwa,
ambapo ng’ombe mmoja huweza kutoa
hadi lita tisa za maziwa
kwa siku na kilo 230 za nyama.
“Mhe. Rais shughuli zenu nyingine
ni uendelezaji na uzalishaji wa
mbuzi wa aina ya Malya
au Blended Goat kwa ajili ya nyama na
maziwa, kuchagua na kukoosafu mifugo
ya asili, kushirikiana na wadau wengine wanaojishughulisha
na uendelezaji wa mifugo na
uzalishaji na usambazaji wa mifugo
yenye tija vijijini” akasema Dkt Mbwile.
Taasisi ya Taifa ya Utafiti
wa Mifugo pia hujishughulisha na kufanya tathimini na kuboresha
vyakula vya mifugo, kutathimini na uboreshaji wa
malisho na nyanda za malisho,
utoaji wa habari kuhusu teknolojia
zilizopo na kufanya tafiti zinazohusu masuala mtambuka kama vile mtizamo wa jinsia,
athari za ukimwi, matumizi ya ujuzi asilia
na hifadhi ya mazingira.
Mwisho.