DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116898

E-mail:  ikulumawasiliano@yahoo.com

              press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

 

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

 

Rais Jakaya Mrisho Kikwete leo (Jumatano, Aprili 16, 2008) amekuwa na siku yenye shughuli nyingi za kidiplomasia katika ziara yake ya siku mbili katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, mjini New York, Marekani.

 

Kwenye siku ambako amehudhuria mkutano kati ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) na Umoja wa Afrika (AU) kujadili jinsi gani taasisi hizo zinaweza kushirikiana kutatua matatizo ya Afrika, Rais Kikwete alikutana kwa faragha na viongozi wapatao watano.

 

Na moja ya mambo makuu ambayo yalitawala mikutano mingi lilikuwa ni suala la Zimbabwe na kucheleweshwa kutangazwa kwa matokeo ya urais kutokana na Uchaguzi Mkuu uliofanyika nchini humo Machi 29, mwaka huu, siku 18 zilizopita.

 

Mkutano wake wa kwanza leo asubuhi, hata kabla ya kuingia katika masuala ya migogoro ya Afrika ulikuwa kati yake na Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown. Kama ilivyotarajiwa suala la Zimbabwe ndilo lilikuwa mazungumzo makuu katika mkutano huo wa nusu saa.

 

Mkutano huo ulifuatiwa na mwingine kati ya Rais Kikwete na Waziri Mkuu wa Italia, Romano Prodi ambaye anamaliza kipindi chake. Prodi anatarajiwa kuachia ngazi kati ya Mei 5 na 15.

 

Katika mkutano huo, Rais alitumia muda wake kumshukuru Prodi kwa mambo ambayo amelifanyia Bara la Afrika, na Tanzania, wakati wa uongozi wake.

 

Prodi amemwambia Rais kwa utani, “naachia uwaziri mkuu, lakini sifi, kwa hiyo ni dhahiri kuwa tutakutana na kuendelea kufanya kazi pamoja katika nafasi nyingine.”

 

Baada ya kuwa amemaliza mkutano huo, Rais Kikwete alikutana na Rais wa Somalia, Abdullahi Yusuf Ahmed.

 

Jambo kubwa katika mazungumzo kati ya viongozi hao ni kwamba Rais Kikwete alitaka kujua jinsi gani AU inaweza kusaidia kutatua zahama ya siasa katika Somalia, nchi ambayo imekuwa ikiendelea kwa zaidi ya miaka 15 sasa.

 

Rais Ahmed alimwomba Kikwete kutumia uwezo wake katika nafasi yake ya AU kuhakikisha kuwa nchi zilizoahidi kuchangia jeshi la kulinda amani katika nchi hiyo zinapeleka majeshi yao katika Somalia.

 

Rais huyo wa Somalia, amemweleza Rais Kikwete kuwa mpaka sasa wamepokea vikosi viwili kutoka Uganda na kimoja kutoka Burundi, lakini bado wanasubiri askari kutoka Nigeria, Ghana na Malawi ambazo ziliahidi kutoa askari wao kusaidia amani katika Somalia.

 

Rais Kikwete pia amekutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshughulikia masula ya Afrika, Jendayi Fraser, mkutano ambao umefanyika katika Hoteli ya Intercontinental The Barclays, ambako Rais na ujumbe wake wamefikia.

 

Suala kubwa katika mkutano huo lilikuwa ni hali ya Zimbabwe na jinsi AU na Marekani zinavyoweza kuchangia katika kuhakikisha kuwa zoezi la uchaguzi katika nchi hiyo linakamilika kwa kutangazwa matokeo ya urais nchini humo.

 

Wakati wa jioni, Rais amekutana na Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki Moon katika mkutano uliofanyika ofisini kwa Katibu Mkuu huyo.

 

Masuala ya msingi yaliyojadiliwa katika mkutano huo ni hali ya Zimbabwe, Somalia, Comoro, Burundi, DRC na hasa hali katika eneo la Kivu, na Darfur katika Sudan.

 

Katika mazungumzo hayo, Ban Ki Moon amesema kuwa UN haitaki kushuhudia yale ambayo dunia iliyashuhudia katika Kenya yakitokea katika Zimbabwe kufuatia uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.

 

Katibu Mkuu huyo amemweleza Rais Kikwete kuhusu juhudi ambazo UN inafanya kuhakikisha kuwa majeshi ya kulinda amani katika eneo hilo la Sudan yanapelekwa huko.

 

Amesema kuwa nchi za Misri na Ethiopia zimekubali kuongeza kikosi kimoja kimoja kwa ajili ya jeshi la pamoja la UN na AU la kulinda amani katika eneo hilo.

 

Amesema kuwa vikosi vya kwanza vya nchi hiyo vitapelekwa Darfur mwezi na ujao na vikosi vya pili vitakwenda Septemba, mwaka huu.

 

Amesema kuwa vikosi vya nchi hizo mbili zikiungana na vikosi kutoka Nepal na Thailand ili kuanza kujenga jeshi ambalo ifikapo mwisho mwa mwaka huu litakuwa na idadi iliyopangwa ya askari 26,000.

 

Usiku, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo.

 

Katika mkutano huo, Rais alitaka kujua hali ilivyo katika nchi hiyo na jinsi gani AU inaweza kusaidia kama nchi hiyo inahitaji msaada wowote.

 

Mwisho.

 

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais na Habari

NEW YORK.

 

17.04.2008