DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116898

E-mail: press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

 

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Millennium Challenge Corporation (MCC) ya Marekani imeonyesha dhamira ya kuendelea kusaidia juhudi za Tanzania za kujiletea maendeleo baada ya kugundua kuwa nchi hii imetimiza vigezo vya MCC kwa mwaka 2009.

 

Bodi hiyo ilitangaza msimamo huo hivi karibuni Jijini Washington baada ya kupitia utendaji wake kwa mujibu wa sera yake kwa mwaka uliopita, 2008.

 

Katika barua iliyotumwa kwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa MCC, Balozi John Danilovich pamoja na mambo mengine anasema:

 

Kwa niaba ya Taasisi ya Millenium Challenge Corporation (MCC), ninafurahi kukujulisha wewe kuwa Bodi ya Wakurugenzi hivi karibuni ilipitia utendaji wa Tanzania na ilionekana kuwa Tanzania imetimiza vigezo vya kukubalika vya MCC kwa mwaka 2009.”

 

Kwa viwango, MCC inazitaka nchi washiriki kuendeleza na kuonyesha nia ya kuboresha utendaji kila mwaka.  Kwa vile Bodi ya MCC haichagui tena nchi zinazotimiza vigezo kwa kila mwaka wakati wa kipindi chake, MCC inaendelea kufuatilia na kutathmini utendaji wa nchi washirika kwa mwaka mzima na kwa mwaka wakati wa mkutano wa uchaguzi.

 

Tanzania ilifanikiwa kuidhinishwa kwenye MCC mwaka 2007 na wakati wa ziara yake ya kihistoria ya siku nne kuitembelea Tanzania mwezi Februari mwaka jana, Rais wa Marekani anayemaliza muda wake, Geroge W. Bush na Rais kikwete walisaini makubalinao ya mpango huo kwenye hafla iliyofana iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

 

Chini ya mpango huo, Serikali ya Marekani itaipatia Tanzania karibu Dola za Marekani 700 milioni ambazo zitaelekezwa zaidi kwenye miradi mikubwa ya miundombinu.

 

Katika barua yake, Balozi Danilovich anaitia moyo Tanzania kuboresha zaidi mageuzi na utendaji wake, vitu ambavyo ni muhimu katika kupunguza umaskini na kutoa msukumo kwa ukuaji wa uchumi.

 

Anasisitiza kuwa kuboreshwa kwa utendaji ni muhimu kwa matarajio ya Tanzania ya kufanikiwa tena kuingizwa kwenye awamu ya pili ya MCC miaka ijayo.

 

Ninaishauri Serikali kuendelea kufanya jitihada kuendeleza na kuboresha utendaji wake na kuendelea kufikia vigezo vya MCC”, anasema Balozi Danilovich katika barua yake kwa Rais Kikwete.

 

Mageuzi yanayoendelea ni muhimu kwa jitihada za Serikali katika kupunguza umaskini na chachu kwa ukuaji wa uchumi, na kufikia vigezo vinavyohitajika ni jambo muhimu kwa matarajio ya Serikali katika kufanikiwa kuingia kwenye awamu ya pili ya MCC miaka ijayo”, anasema Balozi Danilovich na kuongeza:

 

“MCC na washirika wake wote katika Serikali ya Marekani wako tayari kusaidia jitihada za Serikali zinazoendelea katika kufanya mageuzi.  Sisi katika MCC tunatarajia kuendeleza ushiriki wetu na uwekezaji kwa siku zijazo nchini Tanzania.”

 

 

Imetolewa na:

 

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

 

15 Januari, 2009