DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116898

E-mail: press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

 

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

Rais Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatano, Februari 11, 2009, amekutana na kufanya mazungumzo na Kaimu Balozi wa Marekani katika Tanzania, Larry E Andre Jr. kuhusu masuala mbalimbali ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili na masuala mengine ya kimataifa.

 

Katika mkutano huo uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete na Balozi huyo wamezungumzia maandalizi ya kutekelezwa kwa miradi iliyoko chini ya Millennium Challenge Compact (MCC). ambako Tanzania itapokea mamilioni ya dola za Marekani kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya miundombinu.

 

Balozi Andre Jr amemwambia Rais Kikwete kuwa maandalizi yote yanakwenda vizuri na hatua zote muhimu katika utekelezaji wa MCC zinaendelea kufikiwa kwa wakati.

 

Rais Kikwete pia amemwambia Balozi Andre Jr. kuwa kama litakuwapo pengo lolote katika fedha za kugharimia miradi hiyo kwa sababu ya kupanda kwa gharama za vifaa vya ujenzi tokea MCC ilipotiwa saini mwaka jana wakati wa ziara ya Rais George W. Bush nchini, basi Tanzania itakuwa tayari kuziba pengo hilo.

 

Balozi huyo wa Marekani pia amemkabidhi Rais Kikwete ripoti ya mwisho ya milipuko ya mara kwa mara kwenye Mlima wa Oldonyo Lengai katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha.

 

Hivi karibuni, ubalozi wa Marekani katika Tanzania ulimkabidhi Rais Kikwete ripoti ya awali ya uchunguzi kuhusu milipuko kwenye mlima huo. Uchunguzi huo umefanywa na wataalam wa Marekani baada ya kuwa wameombwa na Tanzania.

 

Balozi Andre Jr. pia amemweleza Rais Kikwete kuhusu ujizo wa Meli USS Robert G Bradley ya Jeshi la Majini la Marekani yenye kuegeshwa katika bandari ya Mayport, Jimbo la Florida. Meli hiyo yenye maofisa 17 na askari 198, imepangwa kuwasili nchini Februari 21.

 

Miongoni mwa shughuli nyingine, meli hiyo itashiriki katika kuweka mikakati ya kupambana na uharamia katika pwani ya Mashariki mwa Afrika ambao umepamba moto hasa katika eneo la Bahari ya Hindi la Somalia. Meli hiyo itaondoka katika Bandari ya Dar es Salaam Februari 27.

 

Rais Kikwete na Balozi huyo pia wamezungumzia masuala ya Zimbabwe na Umoja wa Afrika, Rais Kikwete akimwomba Balozi huyo kuishauri Serikali yake kuunga mkono Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini humo.

 

Imetolewa na:

 

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

 

11 Februari, 2009