DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116898

E-mail: press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

 

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

 

UJERUMANI imeihakikishia Tanzania kuwa itaendelea kutimiza ahadi zake za misaada kwa Tanzania pamoja na matatizo makubwa ya kiuchumi na kifedha yanayozikabili chumi za nchi mbali mbali duniani, ikiwamo Ujerumani yenyewe.

 

Nchi hiyo pia imempongeza Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa jitihada na mchango wake mkubwa katika kuleta amani katika Bara la Afrika, na hasa katika eneo la Maziwa Makuu.

 

Ujerumani imetoa uhakikisho huo kwa Tanzania na pongezi hizo kwa Rais Kikwete leo, Alhamisi, Februari 19, 2009, wakati wabunge wa Kamati ya Fedha ya Bunge la Ujerumani walipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Kikwete.

 

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam, Rais Kikwete amewahakikishia wabunge hao kuwa Tanzania inaendelea kuunga mkono jitihada za Ujerumani kupata kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN).

 

Rais Kikwete pia ameishukuru Ujerumani kwa misaada ambayo wamekuwa wanatoa kwa Tanzania, akiwahakikishia kuwa misaada hiyo inatumika kama ilivyokusudiwa.

 

Rais pia amewaelezea wabunge hao kuhusu jitihada zinazofanywa na Serikali katika kujenga nidhamu zaidi katika matumizi ya fedha za umma.

 

Pia, Rais amewaeleza wabunge hao juu ya jitihada zinazofanywa kuimarisha Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kuweza kusimamia vizuri matumizi ya Serikali na kuweza kufanya ukaguzi wa kuthibitisha kuwa thamani ya miradi nchini inalingana na fedha inayotumika kwenye miradi hiyo.

 

Nao wabunge hao wamesisitiza msimamo wa Ujerumani wa kuendelea kuunga mkono jitihada za Afrika katika kupata kiti kimoja ama viwili vya kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

 

Mwisho

 

 

Imetolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais

Ikulu

Dar es Salaam.

19 Februari, 2009