PRESS SECRETARY TO THE PRESIDENT

 

 

Fax. No. 255-22 2113425                                                  The State House,                        

Tel: 255-22-2116539/2116913                                           P.O. Box 9120,

                                                                                           DAR ES SALAAM.

E-mail:  press@ikulu.go.tz

 

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

 

 

PREMI KIBANGA,

RUVUMA,

10.10.2006

 

 

Rais Jakaya Mrisho Kikwete leo ametembelea kituo cha umeme cha masista wa Benedictine walioko Chipole katika wilaya ya Songea vijijini, mradi ambao unatumika kwa matumizi ya kuendesha shughuli za kituo cha masista hao zikiwemo shule, nyumba zao za kuishi na kituo cha afya.

 

“Matatizo yenu nitayashughulikia kwa vitendo, nitachangia katika shughuli zenu ili mfanikiwe kwani mkifanikiwa nami nimefanikiwa” Rais amesema wakati wa kujibu risala ya  mama mkuu Maria Shukran Mkonde, mama mkuu wa kituo cha masista aliyemtaka Rais kuwasaidia kuendeleza mradi huo wa umeme na kuupanua zaidi kuweza kusaidia hata vijijini vilivyo jirani.

 

Kulingana na taarifa za mradi huo, mradi unaweza kuendelezwa na kutoa huduma kwa maeneo ya jirani wilayani hapo ambayo kwa sasa hayana huduma za umeme.

 

Kituo cha mradi wa umeme cha Masista cha Benedictine kimeanzishwa kwa nguvu za mhisani kutoka Uswisi mwanzoni mwa mwaka 2000 ambaye ameshafariki dunia kabla ya kuendeleza mradi huo zaidi ambao una uwezo wa kuzalisha kilowatts 400 kutokana na maji ya Mto Lupilo.

 

Jana (9.10.06) Rais alitembelea kituo cha kuzalisha miche na vikonyo vya kahawa isiyoshambuliwa na maradhi wala wadudu cha Ugano.

 

Tanzania ni kati ya nchi tatu duniani inayozalisha kahawa ya kundi la Colombian Mild Arabicas na kahawa ya Tanzania ya Robusta ina ubora wa juu kuliko Robusta nyingine duniani, na hii ni nafasi nzuri kwa  Tanzania kwenye soko la dunia.

 

Mara baada ya kuwasili mkoani hapa, Jumapili tarehe 8.10.06, Rais alipokea taarifa ya mkoa na chama na baadaye kuzindua jengo la SACCOS , kituo cha Afya cha Mjimwema na kutembelea makao makuu ya Brigedi ya 401, iliyoko Chandamali ambapo alizungumza na wapiganaji.

 

Katika ziara yake hiyo tangu kuwasili hapa mkoani, Rais pia ametembelea hosteli ya masista ya Mbamba Bay na kutembelea mradi wa umwagiliaji maji mashamba ya mpunga yaliyoko Lundo pamoja na kufanya mikutano ya hadhara katika sehemu mbalimbali ambapo amewashukuru wananchi kwa kumpa kura zilizomwezesha kuwa Rais wa nchi hii.

 

‘Serikali inafanya mageuzi katika kilimo kwani ndiyo shughuli kubwa ya wananchi na ndiyo inayoweza kuwaondolea umaskini, tunataka kufikia mahali ambapo shughuli zenu hizi za kilimo zitawaongezea mapato yenu mara mbili ya mnavvopata sasa’ Alisema Rais.

 

Pia amesema katika mageuzi haya ya kilimo serikali itawapa shughuli  ya kufanya wale wasio nazo kwa sasa kwa  kuongeza matumizi ya maji, yaani kilimo cha kumwagilia ambapo wananchi watakuwa na uhakika wa kuvuna, kuhamasisha matumizi ya mbegu bora na za kisasa, na matumizi ya mbolea ambapo mpaka sasa matumizi yameongezeka mara tatu zaidi ya hapo awali.

 

Pia serikali inafanya mpango wa kuweka umeme katika wilaya za mkoa huu pamoja na kutengeneza barabara kwa kiwango cha lami.

 

“Tutatengeneza barabara ya Ruvuma -Mtwara na Mbaba Bay hadi kiwango cha lami na baada ya muda mfupi tutakuwa na uhakika wa barabara ya Masasi-Tunduru na baadaye Tunduru-Matemanga-Songea hadi Mbaba Bay” amesema wakati akizungumza na wananchi waliofika kumlaki wakati wa kuzindua shule ya sekondari ya kata ya Magagura.

 

Rais pia amewaasa wananchi wa mkoa wa Ruvuma na wilaya zake kuwa makini zaidi na ugonjwa hatari wa ukimwi kwani pamoja na kwamba kuna dalili za ugonjwa huo kupungua katika baadhi ya maeneo, kuna maeneo mengine ugonjwa huo unaongezeka na hivyo kudhoofisha juhudi za kuleta maendeleo.

 

Kesho Rais ataelekea Mtwara ambapo pia atafanya ziara ya kutembelea wananchi na kuona maendeleo yao.

 

Mwisho