DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
UNITED
|
Telephone: 255-22-2114512, 2116898 E-mail: ikulumawasiliano@yahoo.com Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S OFFICE, THE STATE HOUSE, P.O. BOX
9120, DAR
ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
RAIS
wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
leo, Alhamisi, Februari 10, 2011, ametembelea na kukagua Shule
ya Sekondari ya Wama-Nakayama iliyoko Kijiji cha Nyamisati, Kata ya Salale, Wilaya
ya Rufiji, Mkoa wa Pwani.
Shule hiyo inayomilikiwa na kuendeshwa na
Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA) ambayo mwenyekiti
wake wa Bodi ni Mama Salma Kikwete,
inatoa elimu ya sekondari bure
bila malipo yoyote kwa watoto
wa kike yatima, waliokulia katika maisha hatarishi na wale ambao wazazi
wao hawana uwezo kabisa wa kuwasomesha watoto wao.
Katika maelezo yake kwa
Mheshimiwa Rais, Katibu wa WAMA, Bwana Daudi Nasibu amesema kuwa shule hiyo
iliyoanza kujengwa mwanzoni mwa mwaka
2008 kwa msaada wa kuanzia kutoka
Taasisi ya Nakayama ya Japan sasa inao
wanafunzi 82 ambao wako kidato cha pili na cha tatu.
Wanafunzi wa
kidato cha kwanza kwa mwaka huu wataanza
masomo keshokuwa, Jumamosi, Februari 12, mwaka huu.
Rais Kikwete ameambiwa kuwa ujenzi kwenye
shule hiyo bado unaendelea na makusudio
ni kuiwezesha shule hiyo kuwa
na uwezo wa kuwa na
wanafunzi 510 kwa wakati mmoja.
Bw. Nasibu amesema kuwa shule hiyo
yenye walimu wanane chini ya
Mwalimu Mkuu, Twaha A Twaha siyo
tu kwamba inatoa elimu bure
kwa wanafunzi
lakini pia inalipia mahitaji yote ya wanafunzi
ikiwa ni pamoja na nauli
ya kuwasafirisha kutoka nyumbani hadi shule na
kurejea makwao wakati wa likizo.
Bw. Nasibu pia amemweleza
Mheshimiwa Rais baadhi ya changamoto
zinazoikabili shule hiyo ikiwa ni
pamoja na ukosefu wa maji
na umeme wa kutosha, ukosefu
wa zahanati na usafiri wa
uhakika kwa ajili ya wanafunzi
wa shule hiyo iliyoko kiasi
cha umbali wa kilomita 156 kutoka Dar Es Salaam,
na umbali wa kilomita 42 kutoka kwenye Barabara
Kuu ya kutoka
Dar es Salaam kwenda Lindi.
Akisalimiana kwa ufupi tu
na wanafunzi wa shule hiyo
na wanakijiji cha Nyamisati waliofika shuleni hapo kumpokea
na kumsikiliza, Rais Kikwete ameipongeza
Bodi ya WAMA kwa wazo na
uamuzi wa busara wa kujenga
shule hiyo, akawapongeza walimu wa shule hiyo
kwa kazi nzuri, na akawapongeza wanakijiji waliotoa ardhi ambako shule
hiyo imejengwa.
Kwa wanafunzi, Rais amesema: “Nyie hamna tatizo la ada ya shule,
hamna tatizo la nauli ya kuwafikisha
shule, hamna tatizo la chakula. Katika hali hiyo
mnabakia na ada moja: kusoma kwa bidii
na uwezo wenu nyote,”
Ameongeza:
“Kusoma kwa bidii sana ndilo
tumaini letu. Ndiyo tumaini ya
ndugu zenu kwa sababu
nyie mkishakusoma mtasaidia kuwatoa ndugu zenu kwenye
umasikini.”
Baadaye Rais Kikwete alisimama
kwa muda
kwenye bandari ndogo ya Nyamisati
na kusikiliza kero za wananchi
kwenye kijiji hicho. Rais amerejea
Dar es Salaam leo
jioni.
Mwisho.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar
es Salaam.
10
Februari, 2011