DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
UNITED
|
Telephone: 255-22-2114512, 2116898 E-mail: press@ikulu.go.tz Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S OFFICE, THE
STATE HOUSE, P.O. BOX 9120, DAR ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
Rais Jakaya Mrisho Kikwete
anatarajiwa kutoa mada juu ya umuhimu wa shughuli za
uziduaji na uwazi katika mapato
ya madini katika mkutano wa Kimataifa wa
Tasnia ya Uziduaji, (Global Extractive Industries Transparency
Initiative -EITI), ambayo ina malengo ya kuongeza
uwazi na uwajibikaji katika mapato yatokanayo na uchimbaji wa
madini, mafuta na gesi asilia.
Mkutano huo wa siku
mbili unaanza kesho, Jumanne, Machi 2, 2011 jijini Paris, Ufaransa, na Rais
Kikwete anaondoka nchini leo asubuhi
kwenda kuhudhuria mkutano huo.
Tanzania iliomba
na kupewa
uanachama wa muda wa EITI tangu
mwaka 2009. Tanzania
itaweza kupata uanachama kamili baada ya kuwa
imekamilisha na kutimiza vigezo vya kuwa mwanachama
kamili na kuweka misingi ya utoaji taarifa hizo muhimu kwa
umma juu ya malipo ya
kodi kutoka makampuni mbalimbali yaliyopo nchini.
Lengo kuu la kujiunga na EITI ni
kuongeza uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za
madini, mafuta na gesi asilia
kwa kutangaza hadharani malipo yanayotokana na rasilimali zake kwa manufaa ya
wananchi wake.
Utaratibu huu utaweka uwazi na kuondoa usiri ambao
unaweza kuwa mwanya wa kuficha
mapato halisi ya makampuni husika.
Baada ya kumaliza mkutano
huo wa
Paris, Ufaransa, Rais Kikwete atasafiri kwenda moja kwa
moja Nouakchott, Mauritania kwa
ajili ya kikao cha marais wa Afrika wanaotafuta
suluhisho la tatizo la kisiasa katika Ivory Coast.
Katika Mauritania, Rais Kikwete atajiunga
na marais wa Mauritania, Afrika Kusini, Burkina Faso, Chad, Nigeria na
Equatorial Guinea pamoja na
wawakilishi wa Jumuia ya Uchumi
ya Afrika Magharibi (ECOWAS), Mwenyekiti wa Tume ya
Umoja wa Afrika (AU) Balozi Jean Ping na Mwakilishi wa
Umoja wa Mataifa (UN).
Katika kikao hicho, viongozi
hao watafikia uamuzi wa
AU kuhusu mzozo huo na kupendekeza
namna gani ya kuutatua mzozo
huo uliolipuka kufuatia raundi ya pili ya
upigaji kura katika Uchaguzi Mkuu wa Ivory Coast Novemba 28, mwaka jana, 2010.
Matokeo yake, nchi hiyo
imegawanyika katika sehemu mbili, moja
ikimuunga mkono aliyekuwa waziri mkuu wa nchi
hiyo, Mheshimiwa Alassane Quattara na nyingine ikimuunga
mkono Rais aliyekuwa anatetea kiti chake katika
uchaguzi huo, Mheshimiwa Laurent Gbagbo.
Kila mmoja kati ya
wanasiasa hao amejitangaza kuwa Rais na kila mmoja ameunda
na kutangaza Serikali katika nchi hiyo ya
Afrika Magharibi.
Wiki iliyopita,
viongozi hao wa Afrika
walikutana mjini Nouakchott
na baadaye wakaenda Abidjan, Ivory Coast ambako
walikutana na viongozi hao wawili
nchini humo katika jaribio la kutafuta suluhisho la mzozo huo.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR
ES SALAAM
01
Machi, 2011