UNITED
REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
|
Telephone: 255-22-2114512, 2116539 E-mail: press@ikulu.go.tz Website: www.mawasilianoikulu.go.tz Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S OFFICE, THE STATE HOUSE, P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
leo, Jumatano, Machi 9, 2011, anaungana na marais wenzake
wa Afrika waliopewa jukumu la kutafuta suluhu ya mgogoro wa
kisiasa katika nchi ya Afrika
Magharibi ya Ivory Coast, katika hatua za
mwisho za jitihada za kujaribu
kumaliza mgogoro huo.
Rais Kikwete na
marais wenzake wanakutana mjini Addis Ababa,
Ethiopia, katika jitihada mpya za kutafuta
jawabu la mzozo huo uliolipuka mwishoni mwa mwaka
jana kufuatia matokeo ya raundi
ya pili ya
uchaguzi wa Rais wa nchi
hiyo uliofanyika Novemba 28, 2011.
Katika mkutano huo wa siku mbili,
marais hao wanatarajiwa kukabidhi ripoti yao kwa
Kamati ya Amani na Usalama
ya Umoja wa Afrika (AU), ili kuuwezesha Umoja huo kuchukua
uamuzi kamili wa jinsi ya
kumaliza mgogoro huo.
Ripoti hiyo ni matokeo ya mikutano
ya marais hao mjini Addis Ababa, huko Mauritania ambako walikutana mara mbili, na mjini
Abidjan, Ivory Coast. Marais hao waliteuliwa
na Kikao
cha Wakuu wa Nchi Wanachama wa AU katika mkutano
wao wa Januari
mwaka huu.
Rais Kikwete ameondoka nchini leo asubuhi
kwenda Ethiopia kwa kikao hicho cha siku mbili ambako
ataungana na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini,
Rais Idriss Deby wa Chad, Rais
Blaise Campaore wa Burkina Faso na Rais Mohamed Abdel Aziz ambaye ni mwenyekiti wa
kundi hilo.
Wengine wanaotarajiwa kushiriki katika kikao hicho
ni Mwenyekiti
wa Kamisheni ya Umoja wa
Afrika (AU) Bwana Jean Ping na
wawakilishi wa Jumuia ya Uchumi
ya Afrika Magharibi (ECOWAS) na Umoja wa Mataifa
(UN).
Mzozo wa Ivory Coast ulianza
baada ya taasisi mbili zinazosimamia
uchaguzi nchini humo kutangaza matokeo tofauti ya washindi wa
raundi hiyo ya pili ya
upigaji kura kati ya Mheshimiwa
Laurent Gbagbo, aliyekuwa anatetea kiti chake
na mpinzani wake mkuu, Mheshimiwa Alassane Quattara.
Tume ya Uchaguzi ya
nchi hiyo ilimtangaza Quattara kuwa mshindi wa uchaguzi huo kwa asilimia
tisa, lakini siku nne baadaye,
Baraza la Katiba la nchi hiyo lilimtangaza
Gbagbo kuwa mshindi kwa asilimia
moja.
Baraza hilo lilimtangaza
Gbagbo mshindi baada ya kuwa
limefuta matokeo katika majimbo saba aliyokuwa ameshinda Quattara, kaskazini mwa nchi
hiyo ambako ndiko ngome kuu
yake ya kisiasa.
Kwa kufuta matokeo katika majimbo hayo, Baraza
lilimpunguzia Quattara kura 600,000.
Tokea wakati huo, viongozi
hao wawili wote wamejitangaza marais na
kila mmoja kuunda Serikali yake. Nchi hiyo
sasa imetumbukia katika mgogoro kamili wa
kisiasa na vita ya wenyewe kwa
wenyewe ambako yamekuwepo mauaji ya watu na
uharibifu mkubwa wa mali nchini
humo.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano
ya Rais,
Ikulu
DAR
ES SALAAM
09
Machi, 2011