UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116539

E-mail: press@ikulu.go.tz

Website:  www.mawasilianoikulu.go.tz  

Fax: 255-22-2113425

 

Coat of Arms

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

Rais wa Jamhuriya Muunganowa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa misaada ya Marekani kwa Tanzania inachangia kwa kiasi kikubwa kujenga Tanzania ijayo na kuokoa maisha ya maelfu kwa maelfu ya Watanzania.

 

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa misaada hiyo ya Marekani kwa Tanzania inasaidia kupunguza shinikizo kwenye bajeti ya Serikali ambayo katika hali ya kawaida ingetumia fedha yake katika kutoa huduma kwenye maeneo yanayo saidiwa na Marekani.

 

Rais Kikwete ameyasema hayo leo, Alhamisi, Mei 5, 2011, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ya Marekani anayeshughulikia Menejimenti na Raslimali, Bwana Thomas Nides na ujumbe wake.

 

Rais Kikwete yuko Afrika Kusini kuhudhuria Mkutano wa 21 wa Uchumi Duniani wa World Economic Forum – Africa wakati Bwana Nides yuko katika ziara ya nchi za Afrika na amewasili mjini Cape Town akitokea Mozambique.

 

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika kwenye Hoteli ya One & Only mjini Cape Town ambako Rais Kikwete amefikia, Rais Kikwete amemshukuru Naibu Waziri huyo akisema:

 

Misaada ya Marekani imesaidia sana kuokoa maisha ya maelfu kwa maelfu ya wananchi wetu na pia kutoa huduma muhimu kwa wananchi na kuchangia uchumi wetu. Tunawashukuru sana kwa sababu mnasaidia kujenga misingi imara ya maendeleo imara ya nchi yetu.”

 

Marekani imekuwa mmoja wa wabia wakubwa wa maendeleo ya Tanzania ikisaidia katika sekta muhimu kama vile elimu, afya na miundombinu.

 

Katika eneo la elimu, kwa mfano, Marekani inasaidia kugarimia uchapaji wa vitabu vya sayansi kwa ajili ya shule za sekondari nchini.

 

Katika eneo la afya, Marekani kupitia Mpango Maalum wa Afya wa Rais wa Marekani uitwao PEPFAR, imechangia sana katika kupambana na magonjwa ya malaria na Ukimwi ikiwa ni pamoja na kutoa dawa za kusaidia kurefusha maisha ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi.  Katika eneo la miundombinu, Marekani kupitia mpango wake wa MCC inasaidia ujenzi wa barabara muhimu nchini, na miradi mingine muhimu kama vile ya umeme, ujenzi wa viwanja vya ndege, na miradi ya maji ambayo yote imeanza kutekelezwa.

 

Katika eneo la malaria na ukimwi, kwa mfano, Marekani imechangia mno kuokoa maisha ya wananchi wetu. Kule Tanzania Visiwani, malaria sasa imeanza kuwa historia na kwa upande wa Tanzania tumepunguza malaria kwa asilimia 40,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

 

Katika ukimwi, maelfu kwa maelfu ya watu wetu wanapata dawa za kurefusha maisha na kiasi cha  Watanzania milioni 13 wamekwisha kupima ukimwi katika mpango unaosaidiwa na Marekani.”

 

          Rais Kikwete pia amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais na Meneja Mkuu wa Dunia wa Kampuni ya Intel, Bwana John Davies.

 

Jana usiku, Rais Kikwete pia alikutana na kufanya mazungumzo na Naibu Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Erasto Mwencha na pia alikutana na Mtendaji Mkuu wa NEPAD Ibrahim Mayaki.

 

          Mwisho.

 

Imetolewa na:

 

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,

Safarini,

Cape Town, Afrika Kusini

 

5 Mei, 2011