DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116898

E-mail:  ikulumawasiliano@yahoo.com

              press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

 

Coat of Arms

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

SALAMU ZA RAMBIRAMBI ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE

 

 

            Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimwia Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mheshimiwa Abbas Kandoro kufuatia vifo vya watu 16 vilivyotokea tarehe 17 Mei, 2011 baada ya mabasi mawili kugongana uso kwa uso mkoani Mwanza.

 

            Ajali hiyo iliyotokea katika Kijiji cha Chibingo wilayani Geita ilihusisha mabasi makubwa mawili ya abiria; basi la Bunda Express lililokuwa likitokea Mwanza kwenda Karagwe mkoani Kagera ambalo liligongana uso kwa uso na basi lingine la Sheraton lililokuwa likitokea Bukombe Mkoani Shinyanga likielekea Mwanza.

 

            Kufuatia ajali hiyo, ninakutumia salamu za rambirambi wewe Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Abbas Kandoro kutokana na msiba huo mkubwa.  Pia kupitia kwako, natuma salamu za rambirambi kwa familia na watu wote waliopoteza ndugu zao katika ajali hiyo mbaya”, amesema kwa masikitiko Rais Kikwete katika salamu zake hizo, na kuongeza,

 

            Ninamuomba Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema azipokee na kuziweka mahali pema peponi roho za marehemu wote.”

 

            Aidha Rais Kikwete amewahakikishia wafiwa wote kuwa yupo pamoja nao katika kuomboleza vifo vya wapendwa wao huku akiwaomba wawe na moyo wa uvumilivu, ujasiri na subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.

 

            Kwa upande mwingine Rais Kikwete anawaombea kwa Mola wote waliojeruhiwa katika ajali hiyo waweze kupona haraka na kurejea katika hali zao za kawaida ili hatimaye waungane tena na familia, ndugu, jamaa na marafiki zao.

 

            Rais kikwete amezitaka mamlaka na vyombo vyote vinavyohusika na usimamizi wa Sheria ya Usalama Barabarani kutekeleza kikamilifu wajibu wao, kwani, amesema kuwajibika kwao kuna mchango mkubwa katika kudhibiti na hata kutokomeza kabisa ajali za barabarani zinazotokana na uzembe wa baadhi ya madereva hususan wa mabasi ya abiria wasioheshimu Sheria ya Usalama Barabarani.

 

 

Imetolewa na:

 

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

 

18 Mei, 2011