UNITED
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
|
Telephone: 255-22-2114512, 2116539 E-mail: press@ikulu.go.tz Website: www.mawasilianoikulu.go.tz Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S OFFICE, THE STATE HOUSE, P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA KWA MHARIRI WA GAZETI LA UHURU
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete atakuwa
miongoni mwa viongozi wa nchi wanachama wa Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika (SADC) watakaohudhuria mkutano wa dharura wa wakuu wa nchi hizo
unaofanyika kesho, Ijumaa, Mei 20, 2011.
Rais
Kikwete na ujumbe wake wameondoka nchini jioni ya leo, Alhamisi, Mei 19, 2011,
kwenda Namibia, Windhoek, kuhudhuria mkutano huo wa siku moja.
Mkutano
huo utakaofanyika chini ya uenyekiti wa Rais wa Nambia, Mheshimiwa Hifikepunye
Pohamba ambaye pia ni mwenyekiti wa sasa wa SADC utajadili ajenda nne.
Ajenda
hizo ni pamoja na kujadili hali ya kisiasa na kiusalama ya Jamhuri ya
Madagascar ambayo ni nchi mwanachama wa SADC.
Nchi
hiyo imekuwa katika mzozo mkubwa wa kisiasa kufuatia mapinduzi ya uongozi
yaliyomwondoa Rais Marc Ravalomanana madarakani. Mapinduzi hayo yaliongozwa na
meya wa zamani wa jiji la Antananarivo, Mheshimiwa Andry Rajoelina akisaidiwa
na jeshi la nchi hiyo na ambaye anatawala nchi hiyo kwa sasa.
Mkutano
huo pia utajadili hali ya kisiasa na kiusalama ya nchi nyingine mwanachama wa
SADC, Jamhuri ya Zimbabwe, ambayo nayo imekuwa inakumbwa na mzozo wa kisiasa
tokea mwanzoni mwa mwaka 2000.
Pande
zinazovutana katika Zimbabwe zilikubaliana kutia saini makubaliano ya Global
Political Agreement (GPA) iliyounda Serikali ya Kitaifa baina ya vyama vitatu
vikuu vya siasa nchini humo Septemba 2008. Vyama hivyo ni ZANU-PF, MDC-T na MDC-M lakini
katika siku za karibuni, Serikali hiyo imeanza kukumbwa na vikwazo mbalimbali.
Viongozi
hao pia watapokea na kujadili ripoti ya kikosikazi cha mawaziri wa nchi za SADC
kuhusu uwezekano wa kuundwa kwa eneo moja kubwa huru la biashara katika nchi
wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), COMESA na SADC.
Aidha,
wakuu hao watapokea na kujadili ripoti ya mawaziri wa Sheria na Wanasheria
wakuu wa nchi za SADC kuhusu Baraza la Usuluhishi la SADC.
SADC
ina nchi wanachama 15 ambao idadi ya wakazi wake inakadiriwa kufikia milioni
257.7. Nchi hizo ni Tanzania, Angola,
Botswana, Lesotho, Afrika Kusini, Mozambique, Malawi, Madagascar, Namibia,
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Mauritius, Swaziland, Seychelles,
Zambia na Zimbabwe.
Imetolewa na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR
ES SALAAM.
19
Mei, 2011