UNITED
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
|
Telephone: 255-22-2114512, 2116539 E-mail: press@ikulu.go.tz Website: www.mawasilianoikulu.go.tz Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S
OFFICE, THE STATE HOUSE, P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Malabo, Equatorial Guinea
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Alhamisi, Juni 30, 2011,
alikuwa miongoni mwa viongozi wa Serikali na nchi 53 za Afrika walioshiriki
katika ufunguzi wa Mkutano wa 17 wa Viongozi wa Nchi Wanachama wa Umoja wa
Afrika (AU) ulioanza katika mji mkuu wa Equatorial Guinea wa Malabo.
Kabla ya ufunguzi rasmi wa
mkutano huo wa siku mbili, viongozi hao wa nchi wanachama wa AU wameshiriki
katika halfa ya kupanda miti kwenye bustani za ukumbi wa kisasa kabisa wa
Palace of Conferences ulioko katika kijiji kipya na cha kisasa cha Sipopo, nje
kidogo ya Malabo, katika Kisiwa cha Bioko, ambako mkutano huo unafanyika kwa
kila kiongozi kupata mti katika nchi yenye misitu mingi na mikubwa ya eneo la Equator.
Kwenye sherehe hiyo ya ufunguzi
wa Mkutano huo wa 17 wa viongozi wa AU, washiriki wamesimama kimya kwa dakika
moja kwa kumbukumbu ya viongozi wawili wa Afrika ambao wamefariki dunia
karibuni akiwamo Rais Frederick Chiluba, kiongozi wa zamani wa Zambia na rais
wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Mkutano huo wa 17 pia
umewakaribisha kwa mara ya kwanza viongozi wapya wa baadhi ya nchi za Afrika
akiwamo Rais Mamadou Yusuf wa Niger, Rais Alasane Quattara wa Ivory Coast na
Mheshimiwa Iklilou Dhoinine wa Comoro ambao wameingia madarakani kufuatia
chaguzi za kidemokrasia katika nchi zao.
Miongoni mwa viongozi ambao wamezungumza
kwenye sherehe hiyo ya ufunguzi ni Meya wa Jiji la Malabo ambaye amewakaribisha
wajumbe wa mkutano huo katika jiji la Malabo pamoja na Mwenyekiti wa Tume ya
Afrika Mheshimiwa Jean Ping ambaye kwa ufupi ametoa ripoti ya mambo makuu
yaliyofanywa na AU katika miezi sita iliyopita tokea kikao cha mwisho
kilichofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia, ambako ndiko makao makuu ya AU.
Viongozi wengine waliozungumza
kwenye ufunguzi huo ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Mheshimiwa
Asha Rose Migiro, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu wa Arab League
na Mwenyeji wa mkutano huo Rais Theodoro Obing Nguema Mbagoso.
Mheshimiwa Ping pia amesema
kuwa mageuzi ambayo dunia imeyashudia katika baadhi ya mataifa ya Afrika
Kaskazini ni ushahidi wa kutosha kwa Afrika inahitaji kuongeza kasi yake ya mageuzi
na utekelezaji wa demokrasia kama kama inavyodaiwa na mazingira ya sasa ya
Afrika na yale ya dunia.
Rais Kikwete na ujumbe wake
ambao unamshirikisha Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete aliwasili mjini Malabo
usiku wa jana tayari kushiriki katika mkutano huo ambao mada kuu yake itakuwa “Jinsi
ya Kuharakisha Uwezeshaji wa Vijana kwa Ajili ya Maendeleo Endelevu.”
Rais Kikwete alitarajiwa baadaye leo jioni kuzungumza
katika kikao cha kujadili mada kuu ya mkutano huo kufuatia ufunguzi uliofanywa
na Mwenyekiti wa sasa wa AU ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Equatorial Guinea,
Mheshimiwa Theodoro Obiang Nguema Mbasogo.
Mbali na kushiriki katika mkutano huo muhimu, Rais
Kikwete pia ataendesha mkutano wa viongozi wa Afrika katika kupambana na
ugonjwa wa malaria wa ALMA (African Leaders Malaria Alliance katika nafasi yake
kama mwenyekiti wa kwanza wa umoja huo wa wakuu wa nchi za Afrika katika
kupambana na ugonjwa wa malaria.
Rais Kikwete pia atapata nafasi ya kukutana na
watu mbali kujadili masuala yanayohusu Tanzania akiwamo Mheshimiwa Andrew
Mitchel, Waziri wa Misaada ya Kimataifa ya Maendeleo wa Uingereza na Mheshimiwa
Antonio Guterres, Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi
(UNHCR).
Baadaye leo jioni, Rais Kikwete atajiunga na
viongozi wake wengine wa Afrika kwenye halfa ya chakula cha jioni iliyoandaliwa
kwa ajili ya viongozi hao wa Afrika na mwenyeji wao, Mheshimiwa Theodoro Obiang
Nguema Mbasogo.
Imetolewa
na:
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
Safarini,
Malabo,
Equatorial Guinea.
01 Julai, 2011