UNITED
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
|
Telephone: 255-22-2114512, 2116539 E-mail: press@ikulu.go.tz Website: www.mawasilianoikulu.go.tz Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S OFFICE, THE STATE HOUSE, P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais Kikwete aombwa kuendelea kuongoza ALMA
Malabo,
Equatorial Guinea
Viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa
Afrika (AU) wamemwomba Rais Jakaya Mrisho
Kikwete kuendelea kuongoza umoja wa wakuu hao
unaopambana na ugonjwa wa malaria – African
Leaders Malaria Alliance (ALMA) wakati wanajiandaa na kuangalia jinsi ya kumpata kiongozi
mwingine wa umoja huo.
Rais Kikwete amekubali ombi hilo, lakini kwa
masharti kuwa anaendelea kuwa Mwenyekiti wa ALMA kwa miezi sita
tu ijayo hadi mwenyekiti mpya atakapokuwa amechaguliwa wakati wa Mkutano wa
18 wa Wakuu wa Nchi Wanachama
wa AU uliopangwa kufanyika Januari, mwakani, 2012, katika makao makuu wa
AU mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Rais Kikwete amekuwa mwenyekiti wa ALMA tokea kuanza
kwake miaka miwili iliyopita na alitarajiwa kukabidhi nafasi hiyo kwa kiongozi
mwingine wa Afrika wakati wa
Mkutano wa 17 wa Viongozi wa
Nchi Wanachama wa AU ulioanza leo, Alhamisi, Juni 30, 2011 kwenye mji mkuu wa
Equatorial Guinea wa Malabo ulioko
katika Kisiwa cha Bioko.
Ombi hilo limetolewa kwa niaba ya viongozi
wa Afrika na Rais wa
Liberia Mama Ellen Johnson Sirleaf wakati wa mkutano
wa kazi wakati
wa chakula cha mchanauliofanyika kwenye Mgahawa wa La Gaviota
ulioko ndani ya kijiji cha Umoja
wa Afrika cha Sipopo ambako uko
ukumbi wa Palace of
Conferences ambako unafanyika
mkutano wa wakuu wa AU.
Ombi hilo lilitolewa na Mama Sirleaf hata baada ya
Rais Kikwete kuwa amewashukuru na kuwaaga wakuu
wenzake wa AU ambao walimchagua kuwa mwenyekiti mwanzilishi wa umoja huo miaka
miwili iliyopita baada ya kuundwa
kwa umoja huo.
“Mkutano huu unanifikisha mahali pa kukabidhi uenyekiti kwa kiongozi
mwingine ambaye tutamchagua. Namtakia mwenyekiti mpya kila la heri na
namhakikishia ushirikiano wangu usiokuwa na kifani,” Rais
Kikwete amewaambia viongozi wenzake na kuongeza:
“Wakati nafikia mwisho wa
uongozi wangu wa ALMA, ningependa kuwashuruku kwa moyo mkunjufu kwa
imani yenu kwangu, ushirikiano wenu na kuniunga
mkono kwa moyo mmoja. Imekuwa
na heshima
kubwa kwangu na kwa kweli
nimefurahi kupata nafasi ya kutumikia
bara letu kama mwenyekiti mwanzilishi wa ALMA.”
Mara
baada ya Rais Kikwete kuwa
amemaliza .hotuba yake ambako
aliorodhesha mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Bara la Afrika katika miaka miwili
iliyopita katika mapambano dhidi ya malaria, Rais Sirleaf ambaye pia ni Makamu
Mwenyekiti wa Alma, ameingia kati na
kuwaambia wenzake:
“Hakuna shaka kuwa
tumepata mafanikio makubwa katika ALMA katika miaka miwili
iliyopita kwa
sababu ya uongozi imara na
thabiti wa Rais Kikwete. Tunakuomba Mheshimiwa
Mwenyekiti uendelee kuongoza Umoja wetu mpaka tutakapoweza
kumpata mwenyekiti mwingine.”
Rais Kikwete amesita kwa
kama dakika moja tu na
hatimaye amesema: “Nakubali ombi la kuendelea na uenyekiti
huu lakini kwa muda wa
miezi sita tu ijayo. Nitakuwa
mwenyekiti wa
muda. Lakini lazima tuweze kumpata
mwenyekiti mpya wakati wa mkutano
wetu ujao, Januari, mjini Addis
Ababa.”
Viongozi wote waliozungumza kwenye mkutano huo wa kazi wamempongeza na kumsifia Rais
Kikwete kwa mafanikio makubwa ambayo yamepatikana wakati wa uongozi
wake wa miaka miwili.
Miongoni mwa viongozi waliozungumza
kwenye mkutano huo ni Rais
Yoweri Museveni wa Uganda, Rais Armando Guebuza wa Mozambique, Rais Ellen Johnson Sirleaf, Naibu Katibu Mkuu
wa Umoja wa Mataifa, Dkt.
Asha Rose Migiro na Rais wa
Visiwa vya Sao Tome na Principe.
Kiongozi wa Sao Tome na Principe ametoa hadithi iliyowatia simanzi wajumbe wa mkutano
huo wakati aliposema kwake yeye kupambana na ugonjwa wa
malaria ni kazi atayoifanya hadi mwisho wa maisha
yake kwa sababu mkewe ni
mmoja wa wananchi wa nchi
yao waliopoteza maisha kwa ugonjwa
wa malaria.
Kiongozi huyo pia amesema
kuwa itakuwa kazi ngumu sana kutokomeza ugonjwa wa malaria katika Afrika ifikapo
mwaka 2015 kwa sababu mbali mbali
hasa kwa kuwa mapambano ya malaria yanahusisha kila mtu.
“Ni kazi kubwa kweli kweli. Katika nchi yangu
kwa mfano kuna aina 3,000 za mbu na
hatujuia ni mbu gani ni
hatari kwa maana ya kusambaza
magonjwa ni ni aina gani
ina manufaa kwa tabianchi,” amesema huku akishangiliwa
na wajumbe wa mkutano huo.
Imetolewa na:
Mkurugenzi wa Mawasiliano
ya Rais,
Safarini,
Malabo,
Equatorial Guinea.
01
Julai, 2011