UNITED
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
|
Telephone: 255-22-2114512, 2116539 E-mail: press@ikulu.go.tz Website: www.mawasilianoikulu.go.tz Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S
OFFICE, THE STATE HOUSE, P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI
Bunduki haiwezi kumaliza matatizo yetu – JK
Malabo, Equatorial Guinea
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameziambia Sudan na Sudan Kusini
kuwa bunduki haiwezi kutoa majawabu ya mvutano kati ya pande hizo ambazo
zitatengana na kuwa nchi mbili tofauti Julai 9, mwaka huu, 2011, wakati Sudan
Kusini itakapokuwa Taifa Huru.
Mheshimiwa Kikwete amesema kuwa
njia pekee ya kupata majawabu sahihi ya mvutano kati ya pande hizo ni kwao
kuendelea kuzungumza na kutafuta suluhisho la amani la matatizo yao kwa njia ya
majadiliano.
Rais Kikwete ameyasema hayo
leo, Alhamisi, Juni 30, 2011, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na
Makamu wa Pili wa Rais wa Sudan, Mheshimiwa Ali Osman Mohammed Taha wakati wa
Mkutano wa 17 wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU) unaofanyika katika
Kijiji cha kisasa kabisa cha AU cha Sipopo nje ya mji wa Malabo katika Kisiwa
cha Bioko, Equatorial Guinea.
Katika mazungumzo hayo, Rais
Kikwete amewaambia kiongozi huyo wa Sudan: “bunduki haiwezi kuwa jibu kwa
sababu hata mkipigana hatimaye mtalazimika kuzungumza. Hivyo, kama mnaweza
kuzungumza na kukubaliana bila kupigana basi hilo ni bora sana.”
Kwenye mazungumzo hayo,
kiongozi huyo wa Sudan amemwambia Rais Kikwete juu ya hatua ambazo zimekuwa
zinachukuliwa kumaliza mzozo wa kisiasa na kiusalama ambao ulizuka kufuatia
tukio la karibuni katika Jimbo la mpakani la Abyei ambalo mpaka sasa halitakuwa
sehemu ya eneo la Sudan ama Sudan Kusini ifikapo Julai 9 na litabakia eneo
linalojitegemea.
Katika mzozo huo, majeshi ya
pande zote mbili yalipigana yakasababisha upotevu wa maisha na mali na kulazimisha
mamia ya watu kukimbia eneo la mapigano, hatua ambayo ilizusha wasiwasi kuwa
hali hiyo ingeweza kusababisha kuvunjika kwa Makubaliano ya Kuleta Amani katika
Sudan ya Comprehensive Peace Agreement (CPA).
Katika mazungumzo ya leo,
Makamu huyo wa Rais wa Sudan amemhakikishia Rais Kikwete kuwa Sudan itaheshimu
makubaliano ya CPA ya kuiwezesha Sudan Kusini kuwa Taifa Huru ifikapo Julai 9,
mwaka huu, 2011.
Kiongozi huyo wa Sudan amesema
kuwa matatizo mengi ya mvutano kati ya pande hizo mbili yamepatiwa majawabu
isipokuwa suala la mgawanyo wa mapato ya mafuta kati ya pande hizo mbili ambako
pande hizo hazijafikia mwafaka.
Katika Sudan, mafuta huchimbwa
katika eneo la Kusini mwa Sudan lakini husafirishwa kwa mabomba yanayopitia
Sudan kwenda kwenye Bandari ya Port Said iliyoko eneo litakalobakia Sudan baada
ya Julai 9.
Imetolewa
na:
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
Safarini,
Malabo,
Equatorial Guinea.
01 Julai, 2011