DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116898

E-mail: press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

 

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

 

04 Machi, 2009

 

Mkurugenzi Mtendaji,

Kituo cha Televisheni,

ITV/Radio One,

S.L.P. 4374,

DAR ES SALAAM.

 

Ninakujulisha kuwa nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana na taarifa za kifo cha mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha ITV, Rehema Mwakangale kilichotokea siku ya Jumanne tarehe 03 Machi, 2009 katika Hospitali ya Mission Mikocheni Jijini Dar es Salaam alikokuwa amelazwa akisumbuliwa na maradhi ya kifua.

 

Binafsi nilimfahamu marehemu Mwakangale kutokana na uchapakazi wake na umakini katika fani ya utangazaji ambayo ilimwezesha kuwafikishia wananchi habari mbalimbali za kiuchumi na kijamii kupitia Kituo cha Televisheni cha ITV.  Kifo chake ni pigo kubwa kwa Watanzania wote na hasa wanataaluma wenyewe wa Uandishi wa Habari hapa nchini.

 

Kutokana na msiba huo mkubwa, ninakutumia salamu zangu za rambirambi kwa kumpoteza mmojawapo wa wafanyakazi muhimu katika kituo chako.  Aidha, kupitia kwako, natuma salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Rehema Mwakangale.  Nawaombeni nyote muwe na moyo wa ujasiri na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.

 

Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu Rehema Mwakangale mahali pema peponi.

 

 

 

 

Jakaya Mrisho Kikwete

RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA