UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116539

E-mail: press@ikulu.go.tz

Website:  www.mawasilianoikulu.go.tz  

Fax: 255-22-2113425

 

Coat of Arms

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

Chama cha Wanasheria cha Afrika Mashariki (EALS) kimempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Serikali yake kwa kuanzisha na kuruhusu mjadala wa sasa wa nchi nzima kuhusu mabadiliko ya Katiba katika Tanzania.

 

Aidha, chama hicho kimeipongeza Tanzania kwa kuwa nchi pekee katika Afrika na ya nne katika Bara la Afrika kwa kupitisha utekelezaji na kuruhusu watu binafsi uhuru wa kuutumia Mkataba wa Afrika na Wananchi wa Afrika wa Haki za Binadamu.

 

Pongezi hizi zimetolewa leo, Jumanne, Aprili 5, 2011, na viongozi wa chama hicho wakiongozwa na Rais wa EALS, Dk. Wilbert B Kapinga wakati viongozi hao walipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Ikulu, Dar es Salaam.

 

Viongozi hao wa kamati mpya ya uongozi ya EALS iliyochaguliwa Novemba 19, mwaka jana, katika Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika Bujumbura, Burundi, wanatoka katika nchi zote wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi. Pia uongozi huo unashirikisha viongozi kutoka Tanzania Visiwani.

 

Katika taarifa yake iliyosomwa mbele ya Mheshimiwa Rais Kikwete na Dk. Kapinga, EALS imesema: “Tunapenda kuupongeza sana uongozi wako na Serikali yako kwa kuruhusu mjadala mpana wa sasa kuhusu mabadiliko ya Katiba ya Tanzania.”

 

Katika taarifa hiyo, viongozi hao pia wamwomba Rais Kikwete kuwasaidia kupata kiwanja vya kujenga makazi ya kudumu ya chama hicho mjini Arusha yalipo makao makuu cha chama hicho.

 

Aidha, viongozi hao wamemwomba Rais Kikwete kuangalia jinsi ya kusaidia kukiwezesha chama hicho kuweza kuingiza nchini kwa urahisi zaidi maofisa wake kutoka nchi jingine wanachama wa EALS  wanaopata kazi kwenye makao makuu mjini Arusha.

 

Rais Kikwete ameahidi kuwa atayafuatilia mambo hayo mawili kuona jinsi gani chama hicho kinavyoweza kusaidiwa bila kukwazika kupita kiasi.

 

Wakati huo huo, Rais Kikwete amepokea ujumbe maalum kutoka kwa Rais Paul Kagame wa Rwanda. Ujumbe huo umewasilishwa na Waziri wa Sheria na Mwanasheria Mkuu wa Rwanda, Mheshimiwa Tharcisse Karugarama ambaye pia ni mjumbe maalum wa Rais Kagame.

 

Mheshimiwa Karugarama ameandamana na Balozi wa Rwanda katika Tanzania, Mheshimiwa Fatuma Ndangiza.

 

Imetolewa na:

 

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

 

04 Aprili, 2011