DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116898

E-mail: press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

 

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

 

Na Mwandishi Maalum

 

 

Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameliambia Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kuwa hali ya ukame katika baadhi ya sehemu za Tanzania ni suala linalotia wasiwasi.

 

Amelitaka Shirika hilo kujiandaa kuisaidia Tanzania endapo madhara ya ukame huo yatakuwa makubwa kuliko uwezo wa Tanzania kuyabeba peke yake.

 

Aidha, Rais Kikwete amesifia mfumo mpya wa Umoja wa Mataifa wa Delivering as One ambako shughuli za Umoja huo zinafanyika kwa pamoja baina ya mashirika mbalimbali ya Umoja huo na kusema kuwa mfumo huo una manufaa kwa UN yenyewe na nchi wanachama wa Umoja huo.

 

Akizungumza leo, Jumanne, Novemba 3, 2009, na Bwana Alberic Kacom, Mratibu wa Shughuli za Umoja wa Mataifa mpya katika Tanzania, Rais Kikwete amesema kuwa kwa mwaka wa tatu mfululizo mwaka huu, baadhi ya sehemu za Tanzania zinaweza kukabiliwa na ukame.

 

Mwaka huu, kuna dalili kuwa hatutapa mvua za kutosha katika baadhi ya sehemu za nchi yetu. Kwa kawaida mvua huanza Oktoba na wakati huu nchi inakuwa imelowa maji. Na kwa kweli tukikosa mvua za vuli, hali itakuwa mbaya,” amesema Rais.

 

 

Ameongeza: “Kwa miaka miwili iliyopita, tumekuwa na matatizo ya mvua na katika baadhi ya maeneo ya nchi yetu ukame unazidi kuwa mkali zaidi.”

 

Hali hii inatia wasiwasi sana na lazima kwa pamoja tuanze kujiandaa kupambana na hali hiyo. Ukame unazidi kutia wasiwasi katika mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga. Mwaka 2005 wakati tunaingia madarakani nchi yetu ilikabiliwa na ukame na tukalazimika kutoa chakula kwa kiasi cha watu milioni 3.7,” Rais amemwambia Bwana Kacom ambaye ni raia wa Ivory Coast.

 

Kuhusu mfumo mpya wa UN, Rais amesema kuwa mfumo huo wa Delivering as One umethibitika kuwa ni mfumo mzuri na unaofaa kuanza kutumiwa katika nchi zote duniani. Mfumo huo umekuwa ukifanyiwa majaribio katika nchi nane duniani, ikiwamo Tanzania.

 

Kuhusu matatizo ya sasa ya mgao wa umeme, Rais Kikwete amesema kuwa matatizo ya sasa ya umeme ni ya muda tu na kuwa Serikali yake inachukua kila hatua kuyamaliza.

 

Amesema kuwa kwa hakika, upo umeme wa kutosha kuondokana na mgao wa sasa na ndio maana amechukua hatua za kuhakikisha kuwa mitambo ya kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) inawashwa, ili kuziba pengo la sasa katika Gridi ya Taifa.

 

Imetolewa na:

 

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

 

03 Novemba, 2009