UNITED
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
|
Telephone: 255-22-2114512, 2116539 E-mail: press@ikulu.go.tz Website: www.mawasilianoikulu.go.tz Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S OFFICE, THE STATE HOUSE, P.O. BOX 9120, DAR ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Heshimuni
ahadi zetu kwa masikini, Rais Kikwete aziambia nchi tajiri
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, amezitaka
nchi zilizoendelea na tajiri duniani kuheshimu ahadi ya nchi hizo ya kuchangia
kiasi cha dola bilioni 40 katika jitihada za kupunguza vifo vya akinamama na
watoto duniani kwa kuhakikisha zinatoa fedha hizo na kwa wakati ili kupunguza
vifo vya mamilioni ya akinamama na watoto.
Aidha,
Rais Kikwete amezitaka nchi masikini na zinazoendelea duniani kuhakikisha kuwa
endapo fedha hizo zinapatikana na kutolewa basi zitumiwe vizuri na nchi
zinazopewa fedha hizo kwa ajili ya shughuli iliyokusudiwa ya kuokoa maisha ya
watoto na akinamama hasa katika nchi masikini na zinazoendelea.
Rais
Kikwete ametoa miito hiyo jana, Jumatano, Januari 26, 2011, wakati anafungua na
kuendesha Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Umoja wa Mataifa Kuhusu Afya ya
Akinamama na Watoto ambayo anaiongoza kwa ushirikiano na Waziri Mkuu wa Canada,
Mheshimiwa Stephen Harper.
Katika
ujumbe wake mzito zaidi katika hotuba yake ya ufunguzi ambao ameurudia katika
majadiliano, katika ufungaji wa mkutano na katika mkutano na waandishi wa
habari ambavyo vyote vimefanyika mjini Geneva, Uswisi, Rais Kikwete amewaambia
makamishna na waalikwa katika mkutano huo:
“Tunazitaka
nchi zilizoendelea kuheshimu ahadi yake ya kutoa zaidi ya dola bilioni 40 ili
kugharimia mpango kakati wa kuboresha afya ya akinamama na watoto duniani
katika miaka mitano iyajo.”
Rais
Kikwete ameongeza: “Ni matumaini yangu vile vile kuwa utakuwepo uwajibikaji mkubwa zaidi
kwa wadau wote watakaopokea fedha hizo zikiwamo Serikali, taasisi za kimataifa,
mashirika yasiyokuwa ya kimataifa (NGO’s) katika matumizi ya fedha hizo na raslimali
nyingine ambazo watapata katika kupambana na vifo hivyo,”
Tume
inayoongozwa na Rais Kikwete na Waziri Mkuu Harper inalenga kuongeza kasi ya
kuokoa maisha ya akinamama na watoto duniani kwa kuhakikisha Malengo ya
Maendeleo ya Milenia Duniani hasa yake malengo yanayohusika na afya yanafikiwa
kama ilivyopangwa, yaani mwaka 2015.
Kikao cha jana
pia kilihutubiwa na Mheshimiwa Harper mwenyewe na makamu wenyeviti wenza ambao
ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Margaret Chan na
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano ya Simu Duniani, Dkt. Hamadoun Toure.
Tume hiyo itatoa ripoti yake ya mwisho mwezi Mei mwaka huu.
Mwisho.
Imetolewa na:
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
Safarini, GENEVA.
27 Januari, 2011