DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
UNITED
REPUBLIC OF TANZANIA
TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI
JK: Kweli uchumi unakua,
lakini sisi bado masikini
Na Mwandishi Maalum,
PAMOJA na kupokea pongezi za China kuhusu kukua vizuri na
haraka kwa uchumi wa Tanzania, Rais Jakaya Mrisho Kikwete
amesema kuwa bado Tanzania
ni nchi masikini
mno na maisha
ya wananchi bado ni magumu.
Amesema kuwa kupanda mno
kwa bei
za mafuta katika miaka ya
karibuni pia kumechangia kuzidisha ugumu wa maisha
kwa wananchi.
“Ni kweli Tanzania ni nchi ya amani na
isiyoyumba. Uchumi wetu umekuwa unakua
kwa wastani
wa asilimia saba kwa miaka
kadhaa sasa. Lakini bado maisha
ya wananchi wetu ni magumu. Bado yetu
ni nchi masikini,”
Rais Kikwete ameuambia ujumbe wa Chama cha Kikomunisti
cha China
leo (Alhamisi, Septemba 18, 2008) na kuongeza:
“Pato la wastani ya wananchi
wetu ni
dola za Marekani
500 tu, na ongezeko la bei la mafuta katika miaka
ya karibuni limeyafanya maisha ya wananchi wetu
kuwa magumu zaidi.”
Rais Kikwete alikuwa anazungumza na
ujumbe wa Chama cha Kikomunisti cha China wakati
alipokutana nao kwenye Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA). Rais Kikwete alikuwa
njiani kurejea Dar es Salaam baada ya kumaliza ziara
ya Mkoa wa Manyara.
Ujumbe huo uliokuwa katika
ziara ya siku tatu ya
Tanzania kwa mwaliko wa Chama cha Mapinduzi (CCM) umeondoka mara tu baada ya
mazungumzo hayo kwenda Uganda
kuendelea na ziara yake katika
Afrika. Uliwasili nchini kutokea Afrika Kusini juzi
(Jumanne, Septemba 16,
2008), na baada ya Uganda unakwenda Gabon na Nigeria.
Rais Kikwete ametoa ufafanuzi huo kuhusu
tafsiri ya uchumi wa
Tanzania baada
ya kiongozi wa ujumbe huo,
He Yong, ambaye ni Katibu wa Sekretariati
ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti kuimwagia sifa nyingi Tanzania, uchumi wake na uongozi wa Rais
Kikwete.
Amesema He Yong: “Yenu ni jamii
iliyotulia, isiyoyumba. Tanzania
ni moja
ya nchi zenye
chumi zinazokua haraka kwenye Bara hili. Yote hayo yametokana
na uongozi wako imara ambao
umeongeza uwezo wa utawala bora
wa nchi yenu.”
Ameongeza: “Ni jambo la kutia moyo na kufurahisha
kwamba kwa miaka 10 sasa, uchumi wenu umekuwa
unakua haraka na kwenda mbele.
Tunapenda kuelezea husuda yetu kwa uongozi
wako ambao umepelekea mafanikio haya yote.”
He Yong amesema kuwa ziara hiyo
inalenga kuongeza nguvu nyingine katika kuimarisha uhusiano wa
miaka 44 kati ya Tanzania,
na kuwa ujumbe
wake umepokewa vizuri na kufanya mazungumzo
yenye tija na wenyeji wao,
yaani Chama cha Mapinduzi.
Mbali na kufanya
mazungumzo na CCM, ujumbe huo pia
umetembelea mji wa Bagamoyo, kijiji
cha Mwenge cha Dar es
Salaam na Makao Makuu ya Reli
ya Tanzania
na Zambia
(TAZARA), iliyojengwa kwa mkopo kutoka China.
Kwa upande wa
Tanzania,
mazungumzo hayo ya leo yamehudhuriwa
pia na Makamu
Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa pamoja na
Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Mary Nagu.
Rais Kikwete pia ametumia
nafasi ya mazungumzo hayo kumweleza kwa
undani hali ya kiuchumi nchini,
na hasa hatua
zipi Tanzania
inastahili kuzichukua kuongeza kasi ya
kukua kwa sekta ya kilimo,
ambayo alisema ndiyo itakuwa mkombozi
wa kweli kweli wa Mtanzania.
Rais pia amemwelezea He Yong kuhusu hali ya
TAZARA akisema kuwa reli hiyo imekuwa
inakabiliwa na
matatizo mengi kwa sababu ya
menejimenti isiyoridhisha.
“Kwa kweli tumeiendesha
vibaya TAZARA. Kabla ya kifo cha Rais
wa Zambia tulikuwa tumepanga kukutana kuzungumzia hili. Lakini sasa
nitakutana na
Makamu wa Rais kutafuta namna
ya kuimarisha uongozi wa TAZARA,” amesema Rais na
kuongeza:
“Karibuni, kama umesikia tumekodisha Reli ya Kati hapa
kwetu. Ni mawazo yangu kuwa tufanye
hivyo hivyo na TAZARA. Ni mawazo yangu vile vile kupata kampuni
ya China
kusaidia kuiendesha reli hiyo. Wakati huo ukifika bila
shaka mtatusaidia kutafuta kampuni ya namna hiyo.”
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
18 Septemba, 2008