DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
UNITED
|
Telephone: 255-22-2114512, 2116898 E-mail: press@ikulu.go.tz Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S OFFICE, THE STATE HOUSE, P.O. BOX 9120,
DAR
ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
TUZO YA UONGOZI BORA
AFRIKA
Tanzania itakuwa mwenyeji wa sherehe ya kutoa Tuzo ya Uongozi Bora barani Afrika, ya mwaka huu itakayofanyika mwezi Novemba 2009, jijini Dar-Es-Salaam.
Mwenyekiti na mwanzilishi wa Tuzo hiyo Bwana Mo Ibrahim amemueleza Rais Kikwete katika mazungumzo yao leo katika Ikulu Ya Dar-Es-Salaam.
“Tunataka kuonyesha heshima na kuenzi mafanikio ya uongozi mzuri wa Tanzania, na hii ni njia moja wapo ya kuelezea mafanikio mazuri ya uongozi katika Afrika” amesema Bw. Ibrahim.
Sherehe hizo zinatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali duniani wakiwemo washindi wa tuzo mbalimbali duniani, mawaziri, waandishi mashuhuri wa vitabu, waandishi wa habari , wasomi na vyama vya kijamii.
Katika Ikulu ya Dar-Es-Salaam Rais Kikwete pia amekutana na Mwenyekiti wa Touch Foundation, shirika la Kimarekani ambalo linashirikiana na serikali ya Tanzania katika kuimarisha sekta ya Afya hapa nchini.
Katika mazungumzo hayo, wamejadili njia mbalimbali za kukusanya Pesa na misaada kwa ajili ya kuendeleza sekta ya Afya nchini ikiwemo kuimarisha Hospitali ya Bugando iliyoko Mkoani Mwanza na kuendeleza mafunzo kwa wahudumu, manesi na madaktari nchini.
Rais Kikwete pia amefanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Barrick Gold Tanzania Bw. Aron Regent.
Katika mazungumzo yao, mtendaji wa Barrick Gold amemueleza Rais Kikwete kuhusu changamoto kubwa ya kiusalama katika machimbo ya Mara kaskazini (North Mara). Rais pia amechukua nafasi hiyo kumweleza mtendaji huyo kuwa sheria mpya ya madini imefika katika hatua ya mwisho na hivi karibuni itasomwa Bungeni.
Wakati huo huo, jana jioni Rais Kikwete amekutana na Waziri wa fedha wa Morocco Mheshimiwa Salaheddine Mezour na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia Bi Ngozi Okonjo-Iweala ambao wamekuwa nchini kuhudhuria mkutano uliokuwa unazungumzia uhusiano kati ya Shirika la fedha Duniani (IMF) na Afrika.
Katika mazungumzo yao Waziri wa Fedha wa Morocco ameelezea nia ya nchi yake ya kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Morocco ili kuleta maendeleo katika sekta mbalimbali za biashara, uchumi na elimu.
“Tunahitaji kujenga mahusiano baina ya nchi zetu kwani kuna manufaa mengi zaidi hasa katika elimu ya ufundi, kilimo, madini na viwanda na hili tunataka kulifanya sasa na kuhamasisha wawekezaji wengi kutoka Morocco” ameongezea.
Nae Mkurugenzi wa Benki ya Dunia amemueleza Rais Kikwete kuwa benki ya Dunia inaliangalia tatizo la kifedha linaloikumba dunia kwa sasa kwa makini na uangalifu mkubwa.
“Katika matatizo haya tumekuwa tukiangalia tufanye nini, nchi gani tuongeee nazo na tusaidieje huku tukiwa tayari tumeweka mikakati ya kusaidia nchi mbalimbali” amesema
Rais Kikwete pia ameitaka Benki ya Dunia kusaidia zaidi katika sekta ya Kilimo kwani ndiyo inayotegemewa na zaidi barani Afrika na kwamba mapinduzi ya Kilimo ndiyo njia nzuri ya kufikia kiini cha tatizo na kuweza kupunguza umaskini barani kote.
MWISHO.
Imetolewa na Premi Kibanga,
Mwandishi wa Rais Msaidizi,
Ikulu-Dsm
12 Machi, 2009