UNITED
REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
|
Telephone: 255-22-2114512, 2116539 E-mail: press@ikulu.go.tz Website: www.mawasilianoikulu.go.tz Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S OFFICE, THE STATE
HOUSE, P.O.
BOX 9120, DAR ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Tanzania na Kenya zimekubaliana
kukomesha biashara ya miaka mingi ya magendo ya chakula kwenye mpaka wa nchi
hiyo kwa kuamua kuuziana chakula rasmi kwa njia halali kuanzia sasa.
Kwa kuanzia, Tanzania imekubali
kuiuzia Kenya tani 10,000 za mahindi ili kuiwezesha nchi hiyo kukabiliana na
baa la njaa linalowakabili mamilioni ya wananchi wa Kenya hasa katika eneo la kaskazini
mwa nchi hiyo.
Makubaliano hayo ya aina yake
baina ya nchi za Afrika yamefikiwa leo, Ijumaa, Septemba 9, 2011, mjini
Nairobi, Kenya wakati wa mkutano kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Rais Mwai Kibaki wa Kenya.
Mkutano kati ya Rais Kikwete na
Rais Kibaki umefanyika pembeni mwa mkutano wa siku mbili wa kimataifa wa
kujadili zahama ya ukame na baa la njaa katika nchi za Pembe ya Afrika
uliomalizika leo mjini Nairobi.
Rais Kikwete aliwasili Nairobi
jioni ya jana, Alhamisi, Septemba 8, 2011, kuhudhuria mkutano huo ambao kwa leo
umewakutanisha wakuu wa nchi za eneo hilo kwenye eneo la Umoja wa Mataifa,
Gigiri, nje kidogo ya Nairobi.
Katika mazungumzo yao, Rais
Kikwete na Rais Kibaki, wametafakari faida za kuanzisha biashara rasmi ya
kuuziana chakula baina ya nchi hizo mbili na umuhimu wa kukomesha magendo ya
chakula ambayo imekuwa inafanyika kwa miaka mingi katika mpaka wa nchi hizo.
Katika miezi ya karibuni imekuwapo
magendo makubwa ya chakula, na hasa mahindi, kutoka Tanzania ambako makumi kwa
makumi ya malori ya chakula cha magendo yamekuwa yakivushwa mpaka kuingia Kenya
ambayo baadhi ya sehemu zake zinakabiliwa na baa la njaa.
Kiasi cha wananchi milioni 3.7
wa Kenya, wakiwamo wakimbizi 477,000 kutoka Somalia wanakadiriwa kukumbwa na
ukame na hivyo kuhitaji msaada wa chakula na misaada mingine ya kibinadamu
kaskazini mwa nchi hiyo.
Chini ya makubaliano kati ya
Rais Kikwete na Rais Kibaki, nchi ya Kenya itatakiwa kutathmini mara moja
mahitaji yake ya chakula na kuiarifu Tanzania ambayo kupitia Wizara ya Kilimo,
Chakula na Ushirika na hasa kupitia taasisi ya chakula cha akiba ya SGR
itafanya maandalizi ya kuuza chakula hicho kwa Kenya.
Ujumbe wa Kenya unatarajiwa
kuwasili nchini wiki ijayo ukiwa na takwimu za mahitaji yake tayari kwa
mazungumzo na maofisa wa Tanzania wanaoshughulika na masuala ya chakula na
biashara.
Katika mazungumzo hayo, maofisa
hao pia watakubaliana utaratibu wa kukisafirisha
chakula hicho, wasafirishaji wenyewe wa chakula na njia zitakazotumika katika
kukisafirisha kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania kukipeleka Kenya.
Miongoni mwa nchi wanachama wa
Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) Tanzania ni nchi pekee yenye akiba ya chakula,
na hasa mahindi, wakati nchi nyingine zilizobakia za jumuia hiyo zinakabiliwa
na njaa na ukosefu wa chakula kwa viwango vinavyotofautiana.
Tanzania imekuwa inajitosheleza
kwa chakula kwa miaka mitatu iliyopita bila kulazimika kuagiza chakula kutoka
nje na kimsingi hayo ni matokeo ya sera ya sasa ya Serikali ya kutoa ruzuku ya
mbegu, mbolea, dawa za kuulia wadudu na mahitaji mengine ya kilimo kwa
wakulima.
Ruzuku hiyo, kimsingi imekuwa
inatolewa kwa wakulima kwa mikoa inayozalisha chakula, na hasa mahindi, kwa
wingi. Ruzuku hiyo ilianza kutolewa kwa mikoa ya Iringa, Mbeya, Ruvuma na Rukwa
hata kama mikoa sita inayozalisha chakula kwa wingi inashirikisha pia mikoa ya
Morogoro na Kigoma.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES
SALAAM.
09 Septemba, 2011