DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
UNITED
|
Telephone: 255-22-2114512, 2116898 E-mail: press@ikulu.go.tz Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S OFFICE, THE
STATE HOUSE, P.O. BOX 9120, DAR
ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mambo makuu katika Hotuba
ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe Jakaya Mrisho Kikwete kwa Taifa kutoka
Ukumbi wa Kilimani, Dodoma, – jumatano, Juni 10, 2009.
1.
Rais ameelezea
hali ya mtikisiko wa uchumi duniani, chimbuko la
mtikisiko huo na athari za hali hiyo kwa uchumi wa Tanzania. Athari hizo ni
kama ziafuatazo:
(a) Bei na mahitaji ya bidhaa
za Tanzania kwenye masoko ya kimataifa
yamepungua. Mifano ni mazao ya
pamba, kahawa, karafuu,mwani na mazao mengine
(b) Mahitaji na bei za madini ya
vito ya Tanzania pia vimepungua kwenye masoko ya
kimataifa
(c)
Mahitaji ya mazao ya
kilimo ya Tanzania kama vile maua na mboga yamepungua
pia na mauzo
yake nchi za nje yameshuka
kwa asilimia 25
(d) Viwanda vya ngozi, nguo, nyuzi na
mavazi pia vimeathirika na hivyo kuathiri pia upatikanaji wa ajira nchini
(e)
Sekta ya utalii ambayo
ndiyo kubwa kwa uingizaji wa
fedha za kigeni pia imeathirika
kwa watalii wanaokuja nchini kupungua
(f)
Mapato ya Serikali pia
yamepungua na hivyo kuathiri mapato ya ndani
na mapato ya fedha za
kigeni
(g) Uwekezaji kutoka nje umepungua pia na baadhi ya makampuni yaliyokuwa
yanataka kuja kuwekeza Tanzania, ama yameahirisha ama yamefuta mipango yao ya uwekezaji.
Mifano ni mradi wa uwekezaji
katika nickel pale Kabanga,
Ngara, Kagera na miradi ya
umeme, saruji, mbolea na aluminium
smelter mkoani Mtwara
(h) Hali ya ajira nchini imekuwa mbaya zaidi kwa
sababu ya matatizo hayo ya
uchumi na hadi Aprili, mwaka
huu, kiasi cha watu 48,000 walikuwa wamepoteza ajira
(i)
Vile vile kasi ya
kukua kwa uchumi wa Tanzania inakadiriwa kuwa itapungua kutoka kwenye asilimia 7.4 kama ilivyobashiriwa mwaka huu hadi
kufikia asilimia 5 hadi 6
2.
Kutokana na hali hiyo, Rais Kikwete
ametangaza mkakati wa kuhami na kunusuru uchumi wa Tanzania kwa malengo makuu manne yafuatayo:
(a)
Kulinda ajira
na vipato vya wananchi
(b)
Kuhakikisha
upatikanaji wa chakula
(c)
Kulinda uwekezaji
muhimu katika miradi ya maendeleo, hususan miundombinu
(d)
Kulinda programu muhimu za kijamii
3.
Kutokana na hali hiyo, Rais ametangaza
hatua zifuatazo katika kutekeleza mkakati huo wa kuunusuru uchumi (rescue
package):
(a)
Serikali
imeamua kufidia hasara waliyopata wanunuzi wa mazao
kwa msimu uliopita wa 2008/2009. Hasara hiyo ni kiasi cha bilioni 21.9 na
Serikali italipia hasara hiyo ambayo imetokana na kushuka ghafla kwa bei ya
mazao ya Tanzania kwenye soko la kimataifa
(b)
Serikali itatoa
udhamini kwa kuahirisha mikopo ya walioathirika ambao ni pamoja na viwanda,
utalii, kilimo na sekta nyingi za uchumi kwa muda wa miaka miwili. Serikali
imeyataka mabenki kutokutoza riba kwenye mikopo hiyo katika miaka hiyo miwili
(c)
Serikali itatoa
mitaji ya uendeshaji (working capital) kwa riba nafuu na itayakopesha mabenki kwa riba ndogo ya
asilimia mbili na mabenki hayo yatatakiwa kuwakopesha wahitaji kwa riba ndogo
zaidi kuliko ilivyo sasa.
(d)
Serikali
imedhamiria kuboresha mifuko ya dhamana ikiwa ni pamoja na mifuko ya kukopesha
biashara ndogo ndogo kwa kuiongezea fedha zinazoweza kukopwa na wananchi
(e)
Serikali
imeamua kuongeza kasi ya uzalishaji chakula kwa kutoa mikopo ya thamani ya bilioni
20 kupitia Benki ya TIB, na pia kutoka kiasi kingine cha sh bilioni 20 kwa
ajili ya mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya ununuzi wa zana za kilimo kupitia
taasisi za karadha, na kuongeza idadi ya wakulima watakaopata mbolea ya ruzuku
na kiasi cha bilioni 90 kwa ajili ya mboleo hiyo. Vile vile, Serikali imeamua kuanza
kuutumia Mfuko wa Hifadhi ya Chakula (SGR) kupunguza bei ya vyakula kwa
wananchi na hifadhi hiyo itaongezewa fedha za kununulia chakula zaidi
(f)
Serikali
imeamua kukwamua mradi wa kusambaza umeme mkoani Mtwara na pia kuboresha Reli
ya Kati kwa kiasi cha dola za Marekani milioni 43.
(g)
Serikali
imeamua kuhakikisha kuwa programu zote za kijamii kama maji, elimu na afya kama
vile ya kupambana na magonjwa ya ukimwi, kifua kikuu na malaria haziathiriki
kwa sababu ya msukosuko wa sasa wa kiuchumi.
(h)
MPANGO wote huu utaigharimu Serikali kiasi cha sh bilioni
1, 692.5 (karibu sh trilioni 1.7). Fedha hizo zimetengwa katika Bajeti ya
Serikali ya mwaka 2009/2010
inayoanza Julai Mosi, 2009.
Sehemu kubwa ya fedha hizo ni za ndani ya nchi ingawa
kutakuwapo na michango ya wabia wa maendeleo kama Benki ya Dunia, Shirika
la Fedha Duniani (IMF), Serikali ya India na Umoja wa Ulaya (EU).