UNITED REPUBLIC OF
TANZANIA
DIRECTORATE OF
PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
|
Telephone: 255-22-2114512, 2116539 E-mail: press@ikulu.go.tz Website: www.mawasilianoikulu.go.tz Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S
OFFICE, THE STATE HOUSE, P.O. BOX
9120, DAR ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, jioni ya leo,
Alhamisi, Oktoba 13, 2011 ameungana na waombolezaji
kumzika mwanahabari mkongwe, Ndugu Juma Fugame Penza katika makaburi ya Kisutu, mjini
Dar es Salaam.
Ndugu Juma Penza alifariki dunia usiku wa kuamkia leo kwenye Hospitali
ya Hindu Mandal, Dar es Salaam akiwa na umri wa
miaka 63.
Marehemu Penza ambaye amekuwa katika tasnia ya
habari kwa karibu miongo minne
iliyopita na miongoni mwa walioshiriki
mazishi yake katika makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam ni pamoja
na viongozi waandamizi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) alichokifanyia kazi kwa zaidi
ya miaka 20.
Katika salamu za rambirambi
ambazo Mheshimiwa Rais Kikwete amempelekea
Katibu Mkuu wa CCM, Mheshimiwa Wilson Mukama na kupitia
kwake kwa familia na ndugu
wa marehemu, Mheshimiwa Rais amemwelezea Hayati Penza kama mwandishi wa habari aliyefanya
kazi zake kwa weledi na
uzalendo akiongozwa na misingi imara
ya taaluma yake na uzalendo
kwa nchi yake.
“Nilimfahamu binafsi Ndugu Penza wakati tulipofanya kazi pamoja katika Chama cha Mapinduzi. Hakuna shaka kuwa Marehemu
Penza aliitumia taaluma yake ipasavyo, akiongozwa na
weledi wa kazi hiyo na
uzalendo kwa nchi yake. Kamwe,
hakupata kutumia ujuzi wa
kazi yake kugawa wananchi kwa misingi ya
aina yoyote ile.”
Katika maisha yake, marehemu
Juma Fugame alishikilia nafasi za uandamizi katika
vyombo mbalimbali vya habari ikiwa
ni pamoja
na kuwa Kaimu
Mhariri wa Mazageti ya Serikali
ya Daily na Sunday News, Kaimu Mkuu wa
Shirika la Habari Tanzania
(SHIHATA) kabla ya kujiunga na utumishi
wa CCM.
Katika utumishi huo, Marehemu
Penza alipata kuwa Mwandishi wa Habari
wa Katibu Mkuu wa CCM, Mzee
Rashid Mfaume Kawawa ambaye pia ni
marehemu, Mwandishi wa Habari wa
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Mzee John Malecela, Mkurugenzi wa Redio Uhuru
na Afisa Mwandamizi wa masuala
ya habari na vyombo vya
habari katika makao makuu ya
Chama.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano
ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
13
Oktoba, 2011