UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116539

E-mail: press@ikulu.go.tz

Website:  www.mawasilianoikulu.go.tz  

Fax: 255-22-2113425

 

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Msimamo wa Tanzania juu ya Ivory Coast ni wazi, Rais Kikwete amemwambia Ban Ki Moom

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, jana, Jumatano, Januari 26, 2011, amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa Ban Ki Moon.

Aidha, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID), Mheshimiwa Dkt. Rajiv Shah kwenye Hoteli ya Intercontinental mjini Geneva, Uswisi, ambako Rais Kikwete amefikia.

Rais Kikwete yuko mjini Geneva kuhudhuria na kuendesha Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Kimataifa Kuhusu Afya ya Akinamama na Watoto ambako yeye ni mwenyekiti mwenza na Waziri Mkuu wa Canada, Mheshimiwa Stephen Harper. Mkutano huo wa siku moja, umefanyika mjini Geneva jana vile vile.

            Mheshimiwa Ban Ki Moon alikuwa mjini Geneva kwa ajili ya ufunguzi wa Mkutano wa Tume hiyo inayoongozwa kwa pamoja na Rais Kikwete na Waziri Mkuu Harper wakati Dkt. Shah ni kamishna katika Tume hiyo yenye makamishna 30.

Katika mkutano wake na Mheshimiwa Ban Ki Moon, viongozi hao wawili wamejadili masuala mbali mbali kuhusu jinsi ya kufanikisha mchakato wa Tume ya Kimataifa Kuhusu Afya ya Akinamama na Watoto, ambayo imechanguliwa na Umoja wa mataifa kupitia Shirika la Afya Duniani (WHO).

Mheshimiwa Ban Ki Moon amemshukuru na kumsifia Rais Kikwete kwa uongozi wake katika suala zima la afya ya akinamama na watoto na kumweleza kuwa anayo matumaini makubwa kwake kuwa atafanikisha malengo ya Tume hiyo.

Viongozi hao wawili pia wamejadili hali ya kisiasa katika Ivory Coast ambako Rais anayekubaliwa kimataifa kuwa alishindwa uchaguzi mkuu wa Novemba mwaka jana katika nchi hiyo Bwana Laurent Gbagbo amekataa kukabidhi madaraka ya kuongoza nchi hiyo kwa Mheshimiwa Alassane Quattara ambaye anakubaliwa kimataifa kuwa alishinda uchaguzi huo kwa asilimia tisa.

Mheshimiwa Ban Ki Moon ametaka Umoja wa Afrika (AU), Umoja wa Mataifa (UN) na Umoja wa Kiuchumi wa Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) kushirikiana katika kuhakikisha kuwa demokrasia inadumishwa katika Ivory Coast.

Mheshimiwa Kikwete amemwambia Katibu Mkuu huyo wa UN kuwa msimamo wa Tanzania ni wazi kabisa kwamba haikubali mgombea ambaye kila ushahidi unaonyesha kuwa alishindwa uchaguzi kuendelea kushikilia madaraka.

Naye Mheshimiwa Ban Ki Moon alisema kuwa vitendo na maamuzi ya Bwana Gbagbo tokea kushindwa uchaguzi wa nchi hiyo vinahujumu mamlaka, madaka na nafasi ya Umoja wa Mataifa katika kulinda na kutetea demokrasia na haki duniani.

Inawezekana vipi, ushindi wa asilimia tisa wa Quattara ukabadilishwa na kuwa ushindi wa asilimia moja wa Gbagbo?” ameuliza Mheshimiwa Ban Ki Moon katika mazungumzo hayo.

Katika mazungumzo yake na Dkt. Shah, viongozi hao wawili wamejadili jinsi Marekani ilivyo tayari kuisaidia Tanzania katika kuhakikisha kuwa inajitegemea katika usalama na uzalishaji wa chakula na pia kuhakikisha kuwa nchi hiyo inapiga maendeleo ya haraka zaidi kuelekea katika kuwa nchi yenye uchumi na kipato cha kati kwa wananchi wake.

Dkt. Shah amemweleza jinsi gani Rais wa Marekani Mhesimiwa Barack Obama amedhamiria kuendeleza kilimo katika baadhi ya nchi zinazoendelea duniani kama njia ya kujenga urafiki na ushirikiano wa muda mrefu kati ya Marekani na nchi hizo.

Dkt. Shah pia ameonya kuwa uchunguzi na habari za uhakika ambazo USAID inazo ni kwamba bei za chakula na mazao mengine ya kilimo duniani inaweza kuongezeka tena katika miezi sita ijayo.

Rais Kikwete na Dkt. Shah pia wamejadili jinsi Marekani itakavyosaidia katika kuunga mkono jitihada za kuinua kilimo katika mipango ya SAGCOT na Feed the Future.

Mwisho.

Imetolewa na:

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,

Safarini, GENEVA.

26 Januari, 2011