UNITED
REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF
PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
|
Telephone: 255-22-2114512,
2116539 E-mail: press@ikulu.go.tz Website: www.mawasilianoikulu.go.tz Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S
OFFICE, THE STATE HOUSE, P.O. BOX
9120, DAR ES
SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI
RAIS KIKWETE
AKATISHA MAPUMZIKO KUWAJULIA HALI WALIOKUMBWA NA MAFURIKO DAR
Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
leo, Alhamisi, Desemba 22, 2011, amekatisha mapumziko yake ya sikukuu kurejea
Dar es Salaam kujionea mwenyewe madhara na uharibifu wa
mafuriko pamoja na kutoa mkono
wa pole kwa waliopoteza ndugu zao, kuumia ama
kuharibiwa nyumba zao na mafuriko
hayo.
Mara baada ya kuwasili kwenye
Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu
Julius K Nyerere akitokea kwenye Mbuga ya
Wanyama ya Serengeti, mkoani Mara, ambako alikuwa anapumzika, Rais alilakiwa na mawaziri na
viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa
wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Said Mecky Sadiq.
Mheshimiwa Sadiq amemweleza Mheshimiwa Rais kuhusu hali halisi
ya mafuriko katika Mkoa wa Dar es Salaam na madhara yake
akisema kuwa mpaka sasa watu
20 wamethibitishwa kupoteza
maisha na watu wengine 68, wakiwamo wakazi 66 wa Wilaya ya
Ilala, wamejeruhiwa kutokana na mafuriko
hayo.
Mkuu huyo wa Mkoa pia amemweleza
Rais Kikwete kuwa watu 4,909 wamepatiwa hifadhi ya muda katika
sehemu mbalimbali, hasa katika shule
za msingi na sekondari, baada
ya nyumba zao kuharibiwa katika mafuriko hayo yaliyotokana na mvua zilizoanza
kunyesha tokea usiku wa kuamkia
Jumatatu, Desemba 19, mwaka huu hadi
leo.
Amemwambia Rais Kikwete kuwa
kata zote 30 katika wilaya zote tatu
za Mkoa wa Dar es Salaam zimeathiriwa na mafuriko hayo na
kuwa wengi wa watu ambao
nyumba zao zimeharibiwa na kubomolewa katika mafuriko hayo wamehifadhiwa
na wanapatiwa huduma na Serikali.
Mara baada ya kupatiwa maelezo
hayo, Rais Kikwete amepanda helikopta kukagua maeneo yote yaliyoathiriwa
na mafuriko
hayo hasa yale yaliyoko katika
Bonde la Mto Msimbazi na baada
ya ukaguzi huo alikwenda kuwapa
mkono wa pole na kuwajulia hali
wananchi waliopewa hifadhi katika Shule ya Msingi
ya Mchikichini katika Wilaya ya
Ilala.
Kuna kiasi
cha watu 1,900 katika shule hiyo na akizungumza nao, Rais Kikwete
amesema kuwa alikuwa amefika kuwapa pole kwa matatizo yaliyowafika. “Nimekuja kuwapeni pole na maafa yaliyowafika.
Nimekuja kuwahakikisheni kuwa tupo, tuko
nanyi na
tutahakikisha kuwa mnapata huduma zote za msingi
za chakula, za afya, za
usafi kwa maana ya kila
aliyeko hapa kupatiwa godoro, blanketi na chakula.”
Rais Kikwete pia ametumia
nafasi hiyo kuwaagiza wote wanaohusika na
mipango ya miji na usalama
wa wananchi kuhakikisha kuwa wanatafuta na kupata
majawabu ya kudumu ya watu
kuathiriwa mara kwa mara na
mafuriko kwa sababu ya kujenga
na kuishi katika maeneo ya
mabonde.
“Fanyeni uamuzi wa
kutokujenga tena ama kutokurejea tena katika maeneo
ya mabonde. Fanyeni uamuzi wa kutokuishi
katika mazingira ya mashaka ya
usalama wenu na wa familia
zenu kila mvua inaponyesha. Hasara mnaijua zaidi nyie,
hasara za kujenga upya, hasara
za kusafisha tope, hasara za kununua
samani mpya kila mvua inaponyesha,”
Rais Kikwete amewaambia wananchi hao.
Rais
amewaagiza maofisa wanaohusika kuwasaidia watu wanaoishi mabondeni kuhamia sehemu nyingine. “Napenda kuwahakikishieni kuwa tutawapatia maeneo ya kuishi
nje ya mabonde
na maofisa
wote wanaohusika wako hapa wamenisikia.”
Rais Kikwete pia amesimama
kwa muda
kwenye Barabara ya Morogoro na
kuwajulia hali walioathiriwa na mafuriko katika eneo hilo ambao
wameweka makazi yao kwenye miti
iliyoko barabarani hapo baada ya
nyumba zao kuzingirwa na kuharibiwa
na maji katika
eneo hilo.
Kwa mujibu wa uongozi
wa Mkoa wa
Dar es Salaam eneo la ekari 200 na lenye
uwezo wa kutoa viwanja 2,800 limeainishwa katika eneo la Mbopo, Wilaya ya Kinondoni,
kwa ajili ya kutoa viwanja
kwa walioathiriwa na mafuriko hayo
baada ya wenye viwanja hivyo
kulipwa fidia.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano
ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
22
Desemba, 2011