UNITED
REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF
PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
|
Telephone: 255-22-2114512,
2116539 E-mail: press@ikulu.go.tz Website: www.mawasilianoikulu.go.tz Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S
OFFICE, THE STATE HOUSE, P.O. BOX
9120, DAR ES
SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu
wa Mkoa wa
Dar es Salaam Mheshimiwa
Said Meck Sadiq kuomboleza vifo vya watu 13 ambao
wamepoteza maisha katika mafuriko makubwa yaliyotokana na mvua ambazo
zimekuwa zinanyesha tokea jana, Jumanne,
Desemba 20, 2011.
Aidha, Rais Kikwete amempa
pole Mkuu huyo wa Mkoa kutokana na uharibifu
mkubwa wa nyumba, makazi na mali nyingine
za wananchi uliosababishwa na mvua hizo ambazo
pia zimesababisha uharibifu wa miundombinu.
Rais Kikwete pia ameuelekeza
uongozi wa Mkoa wa Dar es
Salaam kwa kusaidiana na taasisi na
vyombo vyenye uzoefu wa maafa
kushirikiana katika kuendelea kuokoa maisha ya watu,
kusaidia waliozingirwa na mafuriko na
kuwahifadhi na kuwasaidia wale wote waliopoteza nyumba na makazi kutokana
na mafuriko hayo.
Katika salamu zake, Rais
Kikwete amemwambia Mheshimiwa Sadiq: “Nimepokea kwa
masikitiko habari za vifo vya
wenzetu 13 vilivyotokana na mafuriko yaliyosababishwa
na mvua kubwa
ambayo sote tumeishuhudia katika Mkoa wa Dar es
Salaam tokea jana. Nakutumia wewe rambirambi zangu kutokana na vifo hivyo, na kupitia
kwako kwa familia, ndugu na jamaa waliopoteza
wapendwa wao katika balaa hili
la mafuriko. Wajulishe kuwa msiba wao
ni msiba
wangu, naelewa machungu yao na
niko nao katika hali ya
sasa ya maombolezo.
Mungu aziweke pema peponi roho za
marehemu wote.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Napenda pia kupitia
kwako kutoa pole zangu nyingi kwa
wote walioumia ama kupoteza mali
zao katika mafuriko haya. Wajulishe kuwa moyo wangu
uko nao wakati
huu wa mazingira
magumu.”
“Chini ya usimamizi wako,
ningependa kuona uongozi wa Mkoa
kwa kushirikiana na taasisi na
vyombo vyenye ujuzi na uzoefu
wa kupambana na majanga na
dharura za namna hii, kuhakikisha
kuwa tunaendelea kuokoa watu ambao
bado wamezingirwa na mafuriko, tunawapa
matibabu wale walioumia katika mafuriko hayo, na tunawahifadhi
na kuwapa huduma za kibinadamu
wote waliopoteza nyumba na makazi
yao katika mafurikio hayo.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano
ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
21
Desemba, 2011