UNITED
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
|
Telephone: 255-22-2114512, 2116539 E-mail: press@ikulu.go.tz Website: www.mawasilianoikulu.go.tz Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S OFFICE, THE STATE HOUSE, P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
ametuma salamu za rambirambi kwa
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji
Tanzania (TBC), Bwana Clement Mshana kuomboleza kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi wa Radio Tanzania Bwana David Wakati.
Mzee Wakati aliaga dunia
jana, Alhamisi,
Desemba Mosi, 2011 kwenye Hospitali ya Regency kwa matatizo ya ugonjwa
wa sukari.
Katika salamu za rambirambi,
Mheshimiwa Rais Kikwete amesema kuwa amesikitishwa na kuhuzunishwa na habari za
kifo cha Mzee Wakati kwa sababu
marehemu alikuwa mtangazaji hodari, mzalendo, mwenye mapenzi mengi kwa
nchi yake na aliyetumia taaluma
yake kwa ujenzi wa nchi
yake.
“Nilimfahamu binafsi Mzee David Wakati. Alikuwa kielelezo cha utangazaji ulio bora katika nchi yetu
na hata
nje ya mipaka
ya nchi yetu.
Alikuwa mwana-taaluma hodari na
aliyetumia taaluma yake vizuri kwa
weledi na uzalendo katika ujenzi wa nchi
hiyo. Ametoa mchango mkubwa kwa
nchi hiyo na ameacha pengo
kubwa kwa taaluma ya utangazaji.”
“Nakutumia wewe rambirambi, na kupitia
kwako natuma rambirambi kwa wanafamilia, ndugu na jamaa wa
marehemu pamoja na wadau wote
wa taaluma ya utangazaji. Napenda kuwahakikishieni nyote kwa
dhati ya moyo wangu kuwa
naelewa machungu yenu katika kipindi
hiki kigumu lakini yote ni
mapenzi ya Mwenyezi Mungu,” amesema Rais Kikwete
katika salamu zake kwa Bwana Mshana.
Amemalizia Rais Kikwete: “Aidha, napenda kuwahakikisheni kuwa moyo wangu uko
nanyi katika wakati huu wa
maombolezo, na msiba wenu ni
msiba wangu. Naungana nanyi katika kumwomba
Mwenyezi Mungu aiweke pema peponi
roho ya marehemu
Wakati. Amen.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR
ES SALAAM.
02
Desemba, 2011