UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116539

E-mail: press@ikulu.go.tz

Website:  www.mawasilianoikulu.go.tz  

Fax: 255-22-2113425

 

Coat of Arms

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

Anzisheni mashamba ya kunenepesha ng’ombeRais Kikwete

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametaka kutengwa kwa maeneo makubwa ya kutosha kila mkoa ili kuanzisha mashamba ya kunenepesha ng’ombe kama moja ya njia za haraka za kuwatoa wafugaji katika umasikini, kuandaa mazingira mwafaka ya uwekezaji katika sekta ya mifugo na kudhibiti uzururaji na mifugo na wachungaji.

 

Aidha, Rais Kikwete ametaka kuanzishwa kwa mageuzi ya sekta za mifugo na uvuvi na kusisitiza kuwa taifa la Tanzania haliwezi kuendelea na ufugaji wa asili usiokuwa na tija na wenye kujenga mazingira ya mfugaji kutumikia ng’ombe badala ya ng’ombe kumtumikia mfugaji.

 

Vile vile Rais ameelekeza zichukuliwe hatua haraka za kuwasaidia wachungaji mifugo wa Tanzania kuweza kubadilika na kuwa wafugaji.

 

Rais Kikwete ametoa maelekezo hayo leo, Jumatano, Machi 30, 2011, wakati alipotembelea na kuzungumza na viongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na taasisi zake katika mwendelezo wa ziara zake kutembelea Wizara mbalimbali za Serikali kufuatilia utekelezaji wa maamuzi ya Serikali.

 

Mashamba ya kunenepesha ng’ombe ndio eneo ambako mageuzi yetu katika sekta ya mifugo yanapoanzia. Na hili ndilo jambo ambalo nitalidai kwa bidii kutoka kwa Wizara hii na viongozi wake,” amesema Rais Kikwete katika kusisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa mashamba hayo (feed lots ama pasture development) na kuongeza:

 

Tafuteni ardhi ya kutosha katika kila mkoa, kuanzia kiasi cha hekta 100 kwa ajili ya kuwasaidia wananchi kuanzisha mashamba ya mbegu za malisho na kunenepesha ng’ombe.  Hili litasaidia watu kuacha uzururaji nchi nzima kutafuta malisho kwa ajili ya mifugo yao kwa sababu kimsingi kama watu wanapo mahali pa kulisha mifugo yao hawatahama tena. Na isitoshe, iko siku kutakuwa hakuna mahali ya kuhamia kila kukicha.”

 

Amesema kuwa mashamba hayo pia yatachochea uwekezaji katika sekta ya mifugo.Hakuna mtu atakayewekeza katika kiwanda cha nyama kama hana uhakika wa kupata ng’ombe wa kuchinja na wenye ubora na kiwango kinachokubaliwa. Jibu la kupata viwanda katika sekta hiyo kwa hiyo ni kuanzisha mashamba ya kuzalisha malisho ya ng’ombe. Nataka mpango wa kuanzisha unenepeshaji wa ng’ombe nchi nzima na kazi hiyo ifanyike katika muda mfupi. Nataka tuianze kazi hii haraka sana kwa sababu sekta ya mifugo haiwezi kuendelea kubakia katika hali ya ujima.”

 

Rais ametoa mfano wa nchi ya Botswana ambayo imepata mafanikio makubwa katika mashamba ya kunenepesha ng’ombe.

 

“Botswana ina ng’ombe kiasi cha milioni 1.8  na uuzaji wa nyama nje ya nchi unaiingizia nchi hiyo zaidi ya dola za Marekani milioni 20 kwa mwaka. Sisi tunao ng’ombe kiasi cha milioni 20 na tunapata nini katika fedha za kigeni? Hata maofisa wa serikali katika Botswana wameanzisha mashamba ya kunenepesha ng’ombe.”

 

Kwa mujibu wa wataalamu, ng’ombe anayenenepeshwa huongeza uzito wake kwa kilo mbili kila siku na anakuwa tayari amepata uzito wa kutosha wa kuingia sokoni kwa bei nzuri katika muda wa miezi mitatu. “Kazi hii ya kunenepa haiwezi kufanywa na ng’ombe aneyetembea kila saa na kila siku.  Hii shughuli ni ya ng’ombe aliyekaa na kutulia.”

 

Katika mazungumzo yake, Rais Kikwete pia ameelezwa baadhi ya kero zinazoikabili sekta ya uvuvi na ameahidi kusaidiana na viongozi wa Wizara hiyo kumaliza kero hizo.

 

Imetolewa na:

 

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

 

30 Machi, 2011