UNITED
REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
|
Telephone: 255-22-2114512, 2116539 E-mail: press@ikulu.go.tz Website: www.mawasilianoikulu.go.tz Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S OFFICE, THE STATE HOUSE, P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
leo, Jumanne, Januari 24, 2012, amekutana na kufanya mazungumzo
na Mkurugenzi wa Masula ya
Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara katika Wizara ya
Mambo ya Nchi za Nje ya
Cuba, Bwana Alberto Velazco San Jose.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete na
Bwana San Jose wamezungumzia masuala
yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na Cuba, masuala ya kanda ya
Afrika na masuala mbalimbali ya kimataifa likiwamo
lile la vikwazo ambazo Marekani iliiwekea Cuba tokea miaka ya 1960 na
inaviendeleza.
“Uhusiano mzuri, wa karibu
na wa miaka
mingi ni kielelezo halisi cha jinsi nchi mbili
ndogo na zinazoendelea zinavyoweza kushirikiana na kusaidiana kama ndugu,” Rais Kikwete
amesema katika mazungumzo hayo na kuongeza, “Nipende
pia kuishukuru Cuba na wananchi wa
Cuba kwa kuunga mkono jitihada za maendeleo za
nchi yetu miaka yote hii
pamoja na kwamba mmeendelea kupambana na vikwazo
vikubwa vya kila aina.”
Kwa miaka mingi, Tanzania na Cuba zimekuwa
zinashirikiana katika masuala mengi na
kusaidiana katika masuala ya kimataifa,
na Cuba imeunga mkono jitihada za maendeleo ya
Tanzania katika nyanja mbalimbali zikiwamo za afya, elimu
na michezo.
Bwana Alberto Valazco
San Jose amemjulisha Rais Kikwete kuhusu mageuzi ya kiuchumi
ambayo nchi hiyo inayafanya kwa kufungua
uchumi wake kutoka uchumi wa dola
na kuuelekeza kwenye uchumi wa
soko ambako watu binafsi wanapata
nafasi kushiriki katika uchumi wa
nchi yao.
“Tunafanya mageuzi makubwa katika uchumi wetu kwa
kuutoa kwenye uchumi wa dola
na kuruhusu sekta binafsi kushiriki
kwenye ujenzi wa uchumi huo. Tunafanya mageuzi lakini hatuna haraka kwa
sababu hatutaki kufanya makosa katika jambo hili,”
amesema Mkurugenzi huyo.
Naye Rais Kikwete ametumia
nafasi hiyo kumjulisha Mkurugenzi huyo kuhusu jitihada
za Serikali yake katika kujenga
mazingira ya kuwaletea maisha bora Watanzania kwa kumweleza jitihada za Serikali kupambana
na ugonjwa wa malaria, kuongeza uzalishaji wa sukari,
kuongeza uzalishaji wa umeme, kupanua
na kuboresha elimu na kuongeza
upatikanaji wa huduma ya maji
kwa wananchi.
Cuba ni moja ya mataifa
yanayoongoza duniani kwa uzalishaji wa sukari, na
imekuwa inajenga kiwanda cha dawa ya kuua mbu
katika jitihada zake za kuisaidia
Tanzania kukabiliana na ugonjwa wa malaria.
Rais Kikwete pia amemweleza
mgeni huyo kuhusu jitihada za Serikali yake
katika kuboresha miundombinu nchini kwa kuboresha usafiri
wa reli, kukabiliana na matatizo katika usafiri wa anga,
upanuzi na uboreshaji wa bandari
za Tanzania na uendelezaji wa ujenzi wa barabara
za lami nchini.
Bwana Alberto Valelazco
San Jose yuko katika ziara za nchi
za Afrika akiwa njiani kwenda
Addis Ababa, Ethiopia kuhudhuria Mkutano
wa Wakuu
wa Nchi za
Umoja wa Afrika (AU) utakaofanyika Januari 29-30 mwaka huu.
Wakati huo huo, Rais
Kikwete amekutana na kufanya
mazungumzo na ujumbe wa Kundi
la Makampuni ya Frontline
Development Partners ya Dubai inayotaka
kuwekeza katika masuala ya maji,
kilimo cha miwa na uzalishaji wa
sukari, usafirishaji wa reli na
uzalishaji wa umeme.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano
ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
24
Januari, 2012