UNITED
REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
|
Telephone: 255-22-2114512, 2116539 E-mail: press@ikulu.go.tz Website: www.mawasilianoikulu.go.tz Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S OFFICE, THE STATE HOUSE, P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
leo, Jumanne, Januari 10, 2012, amepokea hati za utambulisho
kutoka kwa mabalozi watano ambao wataziwakilisha nchi zao katika
Tanzania.
Katika shughuli fupi iliyofanyika
Ikulu, Dar es Salaam, Rais amepokea hati
za utambulisho wa Balozi
wa Denmark Mheshimiwa
Johnny Flentoe, Balozi wa Malawi Mheshimiwa Mama Flossie
Asekanao Gomile-Chidyaonga,
Balozi wa Umoja wa Ulaya
Mheshimiwa Filiberto Cerian Sibregondi, Balozi wa Burundi Mheshimiwa Issa Ntambuka na Balozi
wa Uturuki Mheshimiwa Ali Davutoglu.
Katika mazungumzo na
Balozi Flontoe wa Denmark, Rais Kikwete ameishukuru nchi hiyo kwa
misaada mingi na ya miaka
mingi ya maendeleo ambayo nchi hiyo imekuwa
inatoa kwa Tanzania. “Tumenufaika sana
na uhusiano mzuri baina ya
nchi zetu na kiwango cha maendeleo yetu kimechangia vizuri na Denmark,” amesema.
Rais Kikwete na kuongeza: “Tunafurahi pia Tanzania ilikaribishwa kushiriki na kutoa mchango
katika Kamisheni ya Afrika iliyoangalia
fursa za ajira kwa vijana
katika Afrika. Changamoto kubwa kwetu sasa ni namna ya kutengeneza ajira za kutosha
kwa maelfu ya vijana wanaomaliza
shule kila mwaka kutokana na upanuzi mkubwa
wa nafasi za elimu katika
Tanzania.”
Rais Kikwete alikuwa Kamishna katika Tume hiyo iliyoundwa
na aliyekuwa
Waziri Mkuu wa Denmark Mheshimiwa Anders Fogh Rasmussen na iliyotoa ripoti yake iitwayo Africa Commission: Realising the Potential of Africa’s Youth mwezi Mei 2009.
Katika mazungumzo na
Rais Kikwete, balozi mpya wa
Malawi Mheshimiwa Balozi Gomile-Chidyaonga ameishukuru
Tanzania kwa kuendelea kutoa njia ya
Malawi kupitishia bidhaa zake.
“Uchumi wetu katika Malawi umechangiwa kwa
kiasi kikubwa na Tanzania kuendelea kuiruhusu Malawi kutumia Bandari ya Dar es Salaam na kutumia
barabara zake kupitishia bidhaa zetu,”amesema mama huyo.
Naye Rais Kikwete amemwambia
mama huyo: “Nchi zetu zina uhusiano
mzuri na
wa karibu sana. Watu wetu
ni wamoja
na tutaendelea kuimarisha uhusiano huo na kushirikiana
zaidi. Kama unavyojua,
unaweza kuchagua rafiki lakini huwezi
kuchagua jirani.”
Katika mazungumzo na Balozi
Sibregondi wa Umoja wa Ulaya,
Rais Kikwete amezungumzia umuhimu wa jinsi Tanzania na Umoja huo
kushirikiana katika kukamilisha ujenzi wa Barabara ya
Manyoni-Kigoma ili kuwezesha Tanzania kuunganishwa kwa barabara ya
lami na nchi
jirani ya Burundi.
“Tunahitaji kuendelea na
ujenzi wa miundombinu na hasa ujenzi wa
barabara kati ya Manyoni na
Kigoma ili kufungua ushoroba wa magharibi mwa
Tanzania.”
Rais Kikwete amemhakikishia Balozi Ntambuka wa Burundi kuwa
Tanzania itaendelea kufungua
ardhi na njia zake kwa
ajili ya kupitishia bidhaa za Burundi. “Burundi ni
nchi rafiki, ni nchi jirani,
uhusiano wetu ni mzuri na
tunashirikiana pia kupitia Jumuia ya Afrika Mashariki.
Nataka kukuhakikishia kuwa Bandari za
Tanzania na ardhi yake vitaendelea
kuwa wazi kwa matumizi ya
Burundi.”
Naye Balozi Ntambuka ameishukuru Tanzania kwa
mchango wake wa kutafuta amani katika Burundi. “Hakuna sababu ya kurudia
historia, lakini wenyewe tunajua tulipotoka na
tunajua waliotusaidia. Bado wachanga, na ni muhimu Tanzania kuendelea kutulea na kutusaidia.”
Rais Kikwete na
Balozi Davutoglu wa Uturuki wamekubaliana
kuelekeza nguvu zaidi katika kujenga
na kukuza uhusiano wa kibiashara
na kiuchumi kati ya nchi
hizo mbili. “Uhusiano wetu wa kidiplomasia ni mzuri sana,
uhusiano wa kiuchumi na kibiashara
ndio unaanza. Tunahitaji kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kuongeza uhusiano
wa kiuchumi,” amesema Rais Kikwete.
Balozi Davutoglu pia ameishukuru
Tanzania kwa kutoa ardhi ambako
Uturuki itajenga chuo kikuu.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
10
Januari, 2012